1 Samweli 19

1 Samweli 19

Yonathani amtetea Daudi

1Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi.[#Mit 27:4]

2Lakini huyo Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anakusudia kukuua; basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha;[#Mdo 23:16]

3na mimi nitatoka nje na kusimama kando ya babangu huko shambani ulipo wewe, nami nitazungumza na babangu habari zako; nami nikiona neno lolote nitakuambia.

4Naye Yonathani akamsifu Daudi kwa Sauli, babaye akamwambia, Mfalme asikose juu ya mtumishi wake, yaani, juu ya Daudi kwa maana yeye hakukosa juu yako, tena matendo yake kwako yamekuwa mema sana.[#Mit 31:8; Mwa 42:22; 1 Sam 2:25; 2 Nya 6:22; Zab 35:12; 109:5; Mit 17:13; Yer 18:20; 1 Kor 8:12; 1 Yoh 3:15]

5Kwa kuwa alihatarisha maisha yake, na kumpiga yule Mfilisti, naye BWANA akawatendea Israeli wote wokovu mkuu. Wewe mwenyewe uliona jambo hilo, ukafurahi; basi kwa nini kukosa juu ya damu isiyo na hatia, umwue huyo Daudi bure?[#Amu 9:17; 12:3; 1 Sam 28:21; Zab 119:109; 1 Sam 17:49; 11:13; 1 Nya 11:14; 1 Sam 20:32; Mt 27:4]

6Sauli akaisikiliza sauti ya Yonathani; naye Sauli akaapa, Aishivyo BWANA, yeye hatauawa.

7Basi Yonathani akamwita Daudi, naye Yonathani akamjulisha mambo hayo yote. Kisha Yonathani akamleta Daudi kwa Sauli, naye alikuwa akihudumu mbele yake, kama hapo awali.

Mikali amsaidia Daudi kumtoroka Sauli

8Baada ya hayo kulikuwa na vita tena; naye Daudi akatoka, naye akapigana na Wafilisti, naye akawaua kwa uuaji mkuu; nao wakakimbia mbele yake.

9Tena ikawa, roho mbaya kutoka kwa BWANA ilimjia Sauli, hapo alipoketi ndani ya nyumba yake, akiwa na mkuki wake mkononi mwake; naye Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake.[#1 Sam 16:14; 18:10]

10Sauli akajaribu kumpiga Daudi hadi ukutani kwa mkuki wake, ila yeye akaponyoka kutoka mbele ya Sauli, nao huo mkuki akaupiga ukutani; naye Daudi akakimbia, akaokoka usiku ule.[#Ayu 5:2; Zab 5:6; Mit 1:16; 29:10]

11Kisha Sauli akatuma wajumbe mpaka nyumbani kwa Daudi, ili wamvizie na kumwua asubuhi; naye Mikali, mkewe Daudi, akamwambia, akasema, Wewe usipojiponya nafsi yako usiku huu, kesho utauawa.[#Zab 59:1]

12Basi Mikali akamteremsha Daudi dirishani; naye akaenda akakimbia na kuokoka.[#Yos 2:15; Mdo 9:24,25; 2 Kor 11:32,33]

13Ndipo Mikali akakitwaa kinyago, na kukilaza kitandani, akatia na mto wa singa za mbuzi kichwani pake, na kukifunika kwa nguo.[#Mwa 31:19; Amu 17:5]

14Naye Sauli alipotuma wajumbe ili kumkamata Daudi, yeye alisema, Mgonjwa.

15Basi Sauli akawatuma hao wajumbe ili wamtazame Daudi, akisema, Mleteni kwangu juu ya kitanda chake, nipate kumwua.

16Nao wajumbe walipoingia, kumbe! Kuna kinyago kitandani, na mto wa singa za mbuzi kichwani pake!

17Sauli akamwambia Mikali, Mbona wewe umenidanganya hivi, na kumwacha adui yangu aende, hata ameniponyoka? Naye Mikali akamjibu Sauli, Yeye aliniambia, Niache niende zangu; kwa nini nikuue?[#2 Sam 2:22]

Daudi na Samweli wakiwa Rama

18Hivyo Daudi akakimbia, akajiponya, akamwendea Samweli huko Rama, akamwambia hayo yote Sauli aliyomtenda. Kisha yeye na Samweli wakaenda na kukaa katika Nayothi.[#Mit 17:17; Mal 2:7]

19Naye Sauli akaambiwa, Angalia, yule Daudi yuko katika Nayothi, huko Rama.

20Basi Sauli akatuma wajumbe ili kumkamata Daudi; nao hapo walipowaona jamaa ya manabii wakitabiri, na Samweli amesimama kama mkuu wao, Roho ya Mungu ikawajia wajumbe wa Sauli, nao pia wakatabiri.[#Yn 7:32,45; 1 Sam 10:5,6; 1 Kor 14:3,24,25; Hes 11:25; Yoe 2:28]

21Naye Sauli alipoambiwa, alituma wajumbe wengine, wao nao wakatabiri. Naye Sauli akatuma wajumbe tena mara ya tatu, na wao pia wakatabiri.

22Kisha yeye mwenyewe akaenda Rama, akafika kwenye kile kisima kikubwa kilicho huko Seku; akauliza, akasema, Je! Wako wapi Samweli na Daudi? Na mtu mmoja akajibu, Tazama, wako Nayothi, huko Rama.

23Basi akaenda Nayothi huko Rama, na Roho ya Mungu ikamjia yeye naye, akaendelea mbele, huku anatabiri, mpaka kufika Nayothi huko Rama.[#Mwa 31:24; Hes 23:5; 24:2; 1 Sam 10:10; Mit 21:1; Dan 4:35; Mt 7:22; Yn 11:51; 1 Kor 13:2]

24Naye akavua nguo zake, akatabiri mbele ya Samweli, akalala uchi mchana kutwa na usiku kucha siku ile. Kwa hiyo watu wakasema, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?[#1 Sam 10:11-12; Isa 20:2; 2 Sam 6:14,20; Mik 1:8; Mdo 9:21]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya