1 Samweli 2

1 Samweli 2

Ombi la Hana

1Naye Hana akaomba, akasema,[#Lk 1:46-55; Flp 4:6; Zab 9:14; 13:5; 20:5]

Moyo wangu wamshangilia BWANA,

Pembe yangu imetukuka katika BWANA,

Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu;

Kwa kuwa naufurahia wokovu wako;

2Hakuna aliye mtakatifu kama BWANA;[#Kut 15:11; Isa 6:3; 57:15; Kum 4:35; Zab 73:25]

Kwa maana hakuna yeyote ila wewe,

Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu.

3Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo;[#Mal 3:13]

Majivuno yasitoke vinywani mwenu;

Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa maarifa,

Naye huyapima matendo kwa mizani.

4Pinde zao mashujaa zimevunjika,

Na hao waliojikwaa wamepata nguvu.

5Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula,[#Lk 1:53; Zab 113:9; Isa 54:1; Gal 4:27]

Lakini waliokuwa na njaa sasa hawana njaa tena.

Naam, huyo aliyekuwa tasa amezaa watoto saba,

lakini aliye na watoto wengi amehuzunika.

6BWANA huua, naye hufanya kuwa hai;[#Kum 32:39; Ayu 5:18; Hos 6:1; Yn 5:25-29; 11:25,26; Ufu 1:18]

Hushusha hadi kuzimu, tena huleta juu.

7BWANA hufukarisha mtu, na hutajirisha;[#Ayu 1:21; 5:11; Zab 102:10; 75:7]

Hushusha chini, tena huinua juu.

8Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,[#Dan 4:17; Mwa 41:14; 1 Sam 15:17; Ayu 36:7; Yak 2:5; Ufu 1:6; 3:21; Ebr 1:3]

Humpandisha mhitaji kutoka jaani,

Ili awaketishe pamoja na wakuu,

Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu;

Kwa maana nguzo za dunia zina BWANA,

Naye ameuweka ulimwengu juu yake.

9Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake;[#Zab 91:11; 1 Sam 14:6]

Bali waovu watanyamazishwa gizani,

Maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda;

10Washindanao na BWANA watapondwa kabisa;[#Zab 96:13]

Toka mbinguni yeye atawapigia radi;

BWANA ataihukumu dunia yote;

Naye atampa mfalme wake nguvu,

Na kuitukuza pembe ya masihi wake.

Utovu wa wana wa Eli

11Kisha Elkana akaenda Rama nyumbani kwake. Na yule mtoto akamtumikia BWANA mbele yake Eli, kuhani.[#1 Sam 3:1]

12Basi, hao wana wa Eli walikuwa watu wasiofaa kitu; hawakumjali BWANA,[#Kum 13:13; Rum 1:28]

13wala haki ya makuhani ilivyokuwa kwa watu. Wakati huo mtu yeyote alipotoa dhabihu wakati wowote, ndipo huja mtumishi wa kuhani, nyama ilipokuwa katika kutokota, naye akawa na uma wa meno matatu mkononi mwake;

14naye huutia kwa nguvu humo chunguni, au birikani, au sufuriani, au chomboni; nyama yote iliyoinuliwa kwa huo uma kuhani huichukua mwenyewe. Ndivyo walivyofanya huko Shilo kwa Waisraeli wote waliokuja huko.

15Tena, kabla ya kuteketeza mafuta, huja mtumishi wa kuhani, akamwambia yule mwenye kuitoa dhabihu, Mtolee kuhani nyama ya kuoka; kwa kuwa hataki kupewa nyama iliyotokoswa, bali nyama mbichi.

16Tena, ikiwa mtu yule amwambia, Hawakosi wataichoma moto hayo mafuta kwanza, kisha utwae kadiri roho yako itakavyopenda; ndipo husema, Sivyo, lakini sharti unipe sasa hivi; la, hunipi, basi nitaitwaa kwa nguvu.

17Hivyo dhambi yao wale vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa BWANA; kwa maana hao watu walidharau sadaka ya BWANA.[#Mwa 6:11; Mal 2:8; Rum 2:24]

Mtoto Samweli akiwa Shilo

18Lakini Samweli alikuwa akitumika mbele za BWANA, naye alikuwa kijana aliyevaa naivera ya kitani.[#Kut 28:4]

19Tena mamaye alimshonea kanzu ndogo, na kumletea kila mwaka, hapo alipokwea pamoja na mumewe ili kutoa dhabihu kila mwaka.

20Naye Eli akambariki Elkana na mkewe, akasema, BWANA na akupe uzao kwa mwanamke huyu, wachukue mahali pa yule aliyemtoa kwa BWANA. Kisha wakarudi nyumbani kwao.

21Naye BWANA akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, watatu wa kiume na wawili wa kike. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za BWANA.[#Mwa 21:1; Lk 2:40]

Unabii juu ya nyumba ya Eli

22Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania.

23Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote.

24Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa BWANA.

25Mtu mmoja akimkosea mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosea BWANA, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu BWANA amekusudia kuwaua.[#Hes 15:30; Kum 2:30; Mit 15:10; Yn 12:39,40]

26Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa BWANA, na kwa watu pia.[#Lk 2:52; Mit 3:4; Lk 2:40; Mdo 2:47; Rum 14:18]

27Kisha mtu wa Mungu akamwendea Eli, akamwambia, BWANA asema hivi, Je! Mimi sikujidhihirisha nafsi yangu kwa nyumba ya baba yako, walipokuwa katika Misri, wakiitumikia nyumba ya Farao?[#1 Fal 13:1; Kut 4:14]

28Je! Sikumchagua yeye katika kabila zote za Israeli, ili awe kuhani wangu, apande madhabahuni kwangu; na kufukiza uvumba, na kuvaa naivera mbele zangu? Nami sikuwapa watu wa koo za baba yako dhabihu zote za wana wa Israeli zilizotolewa kwa moto?[#Kut 28:1-4; Law 7:35-36; 2:3]

29Kwa nini basi mnaipiga teke dhabihu yangu na sadaka yangu nilizoziamuru katika maskani yangu; ukawaheshimu wanao kuliko mimi, mpate kujinenepesha kwa sadaka zote za watu wangu Israeli zilizo njema?[#Kum 32:15; Mal 1:12; Kum 12:5]

30Kwa sababu hiyo, BWANA, Mungu wa Israeli, asema, Ni kweli, nilisema ya kuwa nyumba yako, na nyumba ya baba yako itakwenda mbele zangu milele; lakini sasa BWANA asema, Jambo hili na liwe mbali nami; kwa maana wao wanaoniheshimu nitawaheshimu, na wao wanaonidharau nitawadharau.[#1 Nya 15:2; Yer 18:9; Zab 18:20; 91:14; Yn 5:44; 12:26; 1 Pet 1:7; Hes 11:20; 2 Sam 12:9,10; Mal 2:9]

31Angalia, siku zinakuja, nitakapoukata mkono wako, na mkono wa watu wa ukoo wa baba yako, hata nyumbani mwako hapatakuwako mzee.[#1 Sam 4:11]

32Nawe utayatazama mateso ya maskani yangu, katika utajiri wote watakaopewa Israeli; wala nyumbani mwako hapatakuwako mzee milele.[#Zek 8:4]

33Tena mtu wako, ambaye sitamtenga na madhabahu yangu, atakuwa mtu wa kukupofusha macho, na kukuhuzunisha moyo; tena wazao wote wa nyumba yako watakufa watakapokuwa watu wazima.[#2:33 Tafsiri zingine zina ‘watauawa kwa upanga’.]

34Na yatakayowapata wana wako wawili, Hofni na Finehasi; ndiyo ishara itakayokuwa kwako; wote wawili watakufa siku moja.[#1 Sam 4:11]

35Nami nitajiinulia kuhani mwaminifu, atakayefanya kulingana na yale yaliyo katika moyo wangu na katika akili yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele ya masihi wangu milele.[#1 Fal 2:35; 1 Nya 29:22; Ebr 2:17; 7:26-28; 2 Sam 7:11; 1 Fal 11:38; Zab 2:2; #2:35 Au, mtiwa mafuta (tazama 1 Sam 2:10).]

36Kisha itakuwa, ya kwamba kila mtu atakayesalia katika nyumba yako atakwenda kumsujudia, apate kipande kidogo cha fedha, na mkate mmoja; na kumwambia, Tafadhali nitie katika kazi mojawapo ya ukuhani, nipate kula kipande kidogo cha mkate.[#1 Fal 2:27]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya