1 Samweli 23

1 Samweli 23

Daudi aokoa mji wa Keila

1Kisha wakamwambia Daudi, Angalia, Wafilisti wanapigana vita juu ya Keila na kuiba nafaka katika viwanja vya kupuria.[#Yos 15:44]

2Basi Daudi akamwuliza BWANA, Je! Niende nikawapige hao Wafilisti? Naye BWANA akamwambia Daudi, Nenda ukawapige Wafilisti, na kuuokoa Keila.[#Hes 27:21; Amu 1:1; 1 Sam 28:6; 30:8; 2 Sam 5:19,23; 1 Nya 10:14; 14:10; Zab 32:8; 37:5; Mit 3:5,6; Yer 10:23; Yak 1:5]

3Ila watu wake Daudi wakamwambia, Tazama, sisi tunaogopa hapa katika Yuda; je! Si zaidi tukienda Keila juu ya majeshi ya Wafilisti?

4Basi Daudi akamwuliza BWANA tena, Naye BWANA akamjibu, akasema, Ondoka, ukashukie Keila; kwa kuwa nitawatia hao Wafilisti mikononi mwako.

5Ndipo wakaenda Keila, Daudi na watu wake, wakapigana na hao Wafilisti, wakateka nyara ng'ombe zao, na kuwaua uuaji mkuu. Hivyo Daudi akawaokoa watu wa Keila.

6Ikawa Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipomkimbilia Daudi huko Keila, alishuka na naivera mkononi mwake.[#1 Sam 22:20; 23:6; Ayu 1:15-19]

7Kisha Sauli aliambiwa ya kwamba Daudi amefika Keila. Sauli akasema, Mungu amemtia mkononi mwangu; kwa maana amefungwa ndani, kwa vile alivyoingia katika mji wenye malango na makomeo.[#Kut 15:9; 1 Sam 24:4-6; 26:8,9; Zab 71:11]

8Basi Sauli akawaita watu wote waende vitani, ili waishukie Keila, na kumzingira Daudi na watu wake.

9Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, Lete hapa hiyo naivera.[#Hes 27:21; 1 Sam 30:7]

10Ndipo Daudi akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mimi mtumishi wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu.[#1 Sam 22:19; 2 Sam 20:20; Est 3:6; Zab 44:22]

11Je! Watu wa Keila watanitoa, nitiwe mkononi mwake? Je! Sauli atashuka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nakusihi, umwambie mtumishi wako. Naye BWANA akamjibu, Atashuka.

12Ndipo Daudi akasema, Je! Watu wa Keila watanitia mimi na watu wangu mkononi mwake Sauli? BWANA akasema, Watakutia.

13Basi Daudi na watu wake, ambao walikuwa kama mia sita, wakaondoka na kutoka Keila, wakaenda popote walipoweza kwenda. Kisha Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia toka Keila; akauacha mpango wake.[#1 Sam 22:2; 25:13]

14Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake.[#Zab 11:1; Yos 15:55; 1 Sam 27:1; Zab 54:3,4; Mit 1:16; 4:16; Kum 33:3; 1 Sam 2:9; Zab 32:7; 33:18; Mit 2:8; Rum 8:31; 2 Tim 3:11; 4:17,18]

Daudi amtoroka Sauli nyikani

15Daudi akaona ya kwamba Sauli ametoka nje ili kutafuta roho yake; naye Daudi akawako katika nyika ya Zifu, huko Horeshi.

16Ndipo Yonathani, mwana wa Sauli, akainuka akamwendea Daudi huko Horeshi, akamtia nguvu mkono wake katika Mungu.

17Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa makamu wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu.[#1 Sam 24:20]

18Na hao wawili wakafanya agano mbele za BWANA; Daudi naye akakaa huko Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani kwake.[#1 Sam 18:3; 20:16; 2 Sam 21:7]

19Ndipo wale Wazifi wakakwea kwa Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha kwetu ngomeni mwa Horeshi, kilimani pa Hakila upande wa kusini wa Yeshimoni?[#1 Sam 26:1]

20Basi sasa, Ee mfalme, ushuke, kama utakavyo nafsini mwako kushuka; na kazi yetu itakuwa kumtia mkononi mwa mfalme.

21Naye Sauli akasema, Na mbarikiwe ninyi na BWANA; kwa sababu mmenihurumia.

22Nendeni, nawasihi, mkazidi kupata hakika, mkajue na kuona mahali pake anapojificha, tena ni nani aliyemwona huko; maana nimeambiwa ya kwamba ana ujanja mwingi.

23Chunguzeni basi, mkayajue maficho yake yote anapojificha; kisha njoni kwangu, tena msikose, nami nitakwenda pamoja nanyi; tena itakuwa, akiwapo katika nchi, mimi nitamtafutatafuta katika maelfu yote ya Yuda.

24Nao wakaondoka, wakaenda Zifu kumtangulia Sauli; lakini Daudi na watu wake walikuwapo nyikani pa Maoni, katika Araba upande wa kusini mwa jangwa.[#Yos 15:55; 1 Sam 25:2]

25Basi Sauli na watu wake wakaenda kumtafuta. Watu wakamwambia Daudi; basi kwa hiyo akashuka mpaka mwambani, akakaa nyikani pa Maoni. Naye Sauli alipopata habari, alimwinda Daudi nyikani pa Maoni.

26Sauli akaenda upande huu wa mlima, na Daudi na watu wake wakaenda upande huu wa mlima; naye Daudi akafanya haraka sana ili amtoroke Sauli; kwa sababu Sauli na watu wake walikuwa wakiwazingira Daudi na watu wake ili kuwakamata.[#1 Sam 19:12; 20:38; 2 Sam 15:14; Zab 31:22; 2 Nya 20:12; Zab 17:9; 2 Kor 1:8]

27Lakini akaja mjumbe kwa Sauli, kusema, Njoo upesi, kwa kuwa Wafilisti wameishambulia nchi.[#Kum 32:36; 1 Sam 14:6; 2 Sam 22:1-51; 2 Fal 19:9; Zab 18:1-50; Isa 37:6-9; 59:1; Yer 15:20,21]

28Basi Sauli akarudi kutoka kumwinda Daudi, akaenda kupigana na Wafilisti; kwa hiyo wakapaita mahali pale, Selahamalekothi.[#23:28 Kwa maana ya Jiwe la Kutorokea.]

29Naye Daudi akakwea kutoka huko, akakaa katika ngome ya Engedi.[#2 Nya 20:2]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya