The chat will start when you send the first message.
1Kwa ndugu zetu Wayahudi katika Misri, salamu.
2Ndugu zenu, Wayahudi walioko Yerusalemu na katika nchi ya Uyahudi, wanakutakieni amani njema. Mungu awafadhili na kulikumbuka agano lake na Abrahamu na Yakobo, watumishi wake waaminifu.
3Awapeni nyote nia ya kumwabudu na kuyatimiza mapenzi yake kwa moyo mkamilifu na roho nyepesi.
4Aifunue mioyo yenu kwa sheria yake na amri zake na kuwapa amani.
5Ayasikilize maombi yenu na kupatanishwa nanyi, wala asiwaache wakati wa shida.
6Ndivyo tunavyowaombea hapa.
7Katika utawala wa Demetrio, mwaka wa mia moja sitini na tisa, sisi Wayahudi tumewaandikieni katika dhiki na taabu iliyotupata tangu miaka ile Yasoni na wafuasi wake waliofanya uasi juu ya nchi takatifu na ufalme,
8wakauteketeza mlango kwa moto na kumwaga damu isiyo na hatia. Tulimwomba BWANA, naye akatusikia. Tulitoa dhabihu na sadaka ya unga safi; tuliwasha taa na kuiandaa mikate ya wonyesho.
9Sasa tunawaandikieni mzishike siku za sikukuu ya vibanda katika mwezi wa Kislevu Mwaka mia moja themanini na nane.
10Watu wa Yerusalemu, na wale walioko Uyahudi, na wazee wa baraza, na Yuda, kwa Aristobulo, mwalimu wa mfalme Tolemayo, aliye wa ukoo wa makuhani waliopakwa mafuta; na kwa Wayahudi walioko Misri, salamu na afya.
11Tumeopolewa na Mungu katika hatari kubwa, kwa hiyo twamshukuru sana aliyejiweka upande wetu juu ya mfalme.
12Maana ndiye aliyewafukuza hata Uajemi wale waliojipanga juu ya mji mtakatifu.
13Mfalme alipofika Uajemi na lile jeshi lililodhaniwa kuwa halishindiki, waliangamizwa katika hekalu la Nanea kwa werevu wa makuhani wake.[#1 Mak 6:1-4; 2 Mak 9:1-10]
14Antioko, akajifanya anataka kumwoa Nanea, alikwenda huko pamoja na rafiki zake kudai sehemu kubwa ya hazina iwe ada ya arusi.
15Basi, makuhani wa hekalu la Nanea wakazitoa, naye na wafuasi wake wachache waliingia uani. Ikawa, akiisha kuingia hekaluni,
16walifunga milango; kisha wakafungua mlango wa siri katika mbao za darini wakatupa mawe, wakampiga mfalme na kumwangusha kama kwa radi. Wakawapiga wote kwa upanga, wakavikata vichwa vyao na kuvitupa kwa wale waliokuwa wakingoja nje.
17Na abarikiwe Mungu wetu katika mambo yote, aliyewatoa waovu wapate adhabu ya haki.
18Siku hizi tutaiadhimisha sikukuu ya kutakaswa hekalu katika mwezi wa Kislevu, siku ya ishirini na tano. Nasi tumeona vema kuwaarifu ili ninyi pia mwiadhimishe sikukuu ya vibanda. Basi, juu ya ule moto uliotokea Nehemia alipotoa dhabihu (akiisha jenga upya hekalu na madhabahu yake):
19Baba zetu walipokuwa karibu kuchukuliwa Uajemi, makuhani watakatifu wa zamani zile walichukua baadhi ya moto wa madhabahu wakauficha kwa siri katika tundu ndani ya kisima kisicho na maji. Wakasetiri jambo hilo sana, hata hakukuwa na mtu aliyepajua mahali hapo.
20Basi, baada ya miaka fulani, Mungu alipoona vema, Nehemia, aliyetumwa na mfalme wa Uajemi, alipeleka watu wa ukoo wa wale makuhani waliouficha ule moto kuutafuta. Walipoleta habari ya kuwa hawakuona moto, ila maji ya ute tu, aliwaagiza wateke kidogo wamletee.
21Basi, sadaka zikiisha wekwa tayari juu ya madhabahu, Nehemia aliwaagiza makuhani wanyunyize maji hayo juu ya kuni na juu ya sadaka.
22Wakafanya hivyo. Punde kidogo, jua likachomoza, ambalo mpaka wakati ule lilikuwa limefichwa na mawingu, na mara moto mkubwa ulilipuka, hata watu wote wakastaajabu.
23Dhabihu ilipokuwa ikiteketea makuhani walisali – makuhani na watu wote pamoja – Yonathani akiomba na wengine wakimwitikia, kama alivyofanya Nehemia.
24Sala ilikwenda hivi: Ee BWANA, Bwana Mungu, Muumba vitu vyote; wa kuogopwa; mwenye nguvu na haki na rehema. Wewe peke yako u mfalme, mwenye hisani,
25wewe peke yako huturuzuku; wewe peke yako u mwema, Mwenyezi, wa milele. Ndiwe umwokoaye Israeli na maovu yote; uliyewachagua baba zetu na kuwatakasa.
26Ikubali sadaka hii kwa ajili ya watu wako Israeli; uulinde urithi wako na kuuweka wakfu.
27Kusanya watu wetu waliotawanyika; uwaweke huru walio watumwa katikati ya mataifa, na kuwaangalia waliodharauliwa na kuchukiwa; mataifa na wajue ya kuwa ndiwe Mungu wetu.
28Uwatese wanaotuonea na kututenda jeuri.
29Uwapande watu wako katika mahali pako patakatifu, kama Musa alivyosema.
30Baada ya hayo makuhani waliimba nyimbo.
31Na sadaka ilipoteketezwa Nehemia aliwaagiza wayamwage maji yaliyobaki juu ya mawe makubwa.
32Walipofanya hivyo moto ulilipuka, lakini nuru yake ilipochanganyika na ile ya madhabahuni ilizimika.
33Walipoona hayo, walimwarifu mfalme wa Waajemi ya kuwa, katika mahali ambapo wale makuhani waliochukuliwa mateka waliuficha ule moto, yametokea maji haya yaliyotumiwa na Nehemia na wenzake kuitakasa sadaka.
34Mfalme akaichunguza habari hiyo akaithibitisha, akatoa amri mahali pale pawe kiwanja kitakatifu.
35Ndipo alibadilishana zawadi na wale aliotaka kuwafadhili.
36Nehemia na wenzake waliyaita Neftha, yaani utakaso; lakini watu wengine karibu wote huyaita Nefthai.