2 Timotheo 3

2 Timotheo 3

Uovu katika siku za mwisho

1Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.[#1 Tim 4:1]

2Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,[#Rum 1:29]

3wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,

4wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;[#Flp 3:19]

5walio na utaua kwa nje, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.[#Mt 7:15,21; Rum 2:20; Tit 1:16]

6Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za kila namna;[#Mt 23:14; Tit 1:11]

7wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli.[#2 Tim 2:25]

8Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.[#Kut 7:11,22; 1 Tim 6:5; 1:12]

9Lakini hawataendelea sana; maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile na upumbavu wa hao wanaume wawili ulivyokuwa dhahiri.[#3:9 katika Kigiriki hakuna ‘wanaume wawili’.]

Mausia ya Paulo kwa Timotheo

10Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, na makusudi yangu, na imani, na uvumilivu,

11na upendo, na subira; tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonio, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote.[#Mdo 13:14-52; 14:1-20; Zab 34:19]

12Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa.[#Mt 16:24; Mdo 14:22]

13Lakini watu waovu na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika.[#1 Tim 4:1]

14Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao;[#2 Tim 2:2]

15na ya kuwa tangu utotoni umeyajua Maandiko Matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu.[#Yn 5:39; Zab 119:99]

16Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki;[#2 Pet 1:19-21; Rum 15:4]

17ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.[#1 Tim 6:11]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya