The chat will start when you send the first message.
1Hiki ni kitabu cha amri za Mungu[#Sira 24:23]
Na sheria idumuyo milele.
Wote waishikao wataona uzima,
Lakini waiachao watakufa.
2Rudi, Ee Yakobo, uishike;
uiendee nuru yake katika mwangaza wake.
3Usimpe mwingine utukufu wako,
Wala mataifa ya kigeni mafaa yako.
4Ee Israeli, tu heri sisi,
Maana mambo yampendezayo Mungu yamejulishwa kwetu.
5Jipeni moyo, watu wangu, Israeli mnaokumbukwa!
6Mliuzwa kwa mataifa, lakini hamkuangamia.
Kwa kuwa mlimtia Mungu ghadhabu
Mlitolewa kwa adui zenu.
7Mlimwasi Yeye aliyewaumba,
Mkitoa sadaka kwa pepo, si kwa Mungu.
8Mlimsahau Mungu wa milele aliyewalea,
Na Yerusalemu, mama yenu.
9Huyu mama aliiona ghadhabu ya Mungu
Iliyokuja juu yenu, akasema,
Enyi wa Sayuni, sikilizeni!
Mungu ameleta juu yangu huzuni kubwa.
10Nimeuona utumwa wa wanangu
Ambao Aliye wa Milele amewapatiliza.
11Kwa furaha niliwalea;
bali kwa kilio na maombolezo niliwaaga.
12Asisimange juu yangu mtu yeyote,
Mimi niliye mjane na kuachwa na watu.
Kwa sababu ya dhambi za wanangu nimeachwa ukiwa,
Kwa kuwa walikengeuka na kuiacha sheria ya Mungu.
13Hawakujali maagizo yake,
Wala kwenda katika njia za amri zake,
Wala kukanyaga njia za utii katika haki yake.
14Wakaao pande za Sayuni na waje,
Waukumbuke utumwa wa wana wangu na binti zangu
Ambao Aliye wa milele amewapatiliza.
15Maana ameleta juu yao taifa kutoka mbali,
Taifa lisilo na haya, lenye lugha ya kigeni,
Lisilojali mzee wala kuhurumia mtoto.
16Nao wamewahamisha mbali wana wapendwa wa mjane,
Na kumwacha pekee, amefiwa na binti zake.
17Nami nawezaje kuwasaidieni?
18Yeye aliyeyaleta mapigo haya juu yenu
Atawaponya mikononi mwa adui zenu.
19Nendeni zenu, wanangu, nendeni zenu;
nami nimeachwa ukiwa.
20Nimevua mavazi ya amani
Na kuvaa gunia la maombi yangu.
Nitamlilia Aliye wa Milele
Siku zangu zote.
21Jipeni moyo, wanangu, mlilieni Mungu,
Naye atawaponya katika nguvu na mkono wa adui.
22Maana nimemtumaini Aliye wa Milele awaokoe,
Na furaha imenijia kutoka kwake Aliye Mtakatifu.
Kwa sababu ya rehema itakayowajia upesi
Kutoka kwake Mwokozi wenu wa milele.
23Mimi niliwatoa kwa huzuni na kulia,
Lakini Mungu atawarejeza kwangu
Kwa furaha na shangwe hata milele.
24Kama wakaa Sayuni walivyouona utumwa wenu wa sasa,
Ndivyo watakavyouona upesi wokovu wenu
Utokao kwa Mungu wenu,
Utakaowajia kwa utukufu mwingi
Na mwangaza wake Aliye wa Milele.
25Wanangu, istahimili kwa saburi
Ghadhabu ya Mungu iliyowapata.
Adui zenu wamewatesa.
Lakini mtaona upesi maangamizo yao,
Na kuwakanyaga shingo.
26Wanangu wasio na nguvu wamepitia njia za kukwaruza,
Wakichukuliwa kama kondoo waliotekwa na adui.
27Jipeni moyo, wanangu, mlilieni Mungu!
Maana Yeye aliyewapatiliza mambo haya atawakumbuka.
28Kama ilivyokuwa nia yenu kumwasi Mungu,
Rudini sasa, mtafuteni mara kumi zaidi.
29Maana Yeye aliyeyaleta mapigo haya juu yenu
Atawarudishia furaha ya milele pamoja na wokovu wenu.
30Jipe moyo, Ee Yerusalemu!
Yeye aliyekuita kwa jina lako atakufariji.
31Ole wao waliokutesa
Na kuyafurahia maangamizo yako!
32Ole wa mji uliowatumikisha watoto wako!
Ole wake yeye aliyewachukua wana wako!
33Maana kama alivyokusimanga katika maanguko yako
Na kuufurahia uharibifu wako,
Ndivyo atakavyouhuzunikia ukiwa wake mwenyewe.
34Nitaondoa majisifu yake juu ya wingi wa watu wake,
Na majivuno yake yatageuka kuwa kilio,
35Kwa kuwa moto utamshukia kutoka kwake Aliye wa Milele,
Nao utadumu sana.
Naye atakaliwa na majini
muda wa siku nyingi.
36Ee Yerusalemu, tazama upande wa mashariki,
Uione furaha inayokujia kutoka kwa Mungu.
37Angalia! Wana wako wanakuja uliowaaga,
Wanajikusanya toka mashariki hata magharibi
Kwa neno lake Yeye Aliye Mtakatifu,
Wakiufurahia utukufu wa Mungu.