The chat will start when you send the first message.
1Ikawa Mfalme Astiage alipolala pamoja na baba zake, Koreshi, Mwajemi, aliupokea ufalme wake.
2Naye Danieli akakaa kwa mfalme akipewa heshima nyingi kuliko rafiki zake wote.
3Basi, watu wa Babeli walikuwa na sanamu iliyoitwa Beli, ambayo kila siku iligharimiwa pishi kumi na mbili za unga safi, na kondoo arubaini, na nzio sita za divai.[#Isa 46:1; Yer 51:44; #Dan 6:16-24]
4Naye mfalme alikuwa akiiheshimu sanamu hiyo, akienda kila siku kuiabudu. Bali Danieli alikuwa akimwabudu Mungu wake.
5Mfalme akamwambia, Mbona wewe humwabudu Beli? Akasema, Kwa sababu siwezi kusujudia sanamu zilizofanywa kwa mikono, ila namwabudu Mungu aliye hai, Muumba mbingu na nchi, aliye na mamlaka juu ya wote wenye mwili.
6Ndipo mfalme akamwambia, Wadhani Beli si mungu hai? Huoni jinsi anavyokula na kunywa sana kila siku?
7Danieli akacheka, akasema, Ee mfalme, usidanganyike; hiyo kwa ndani ni udongo tu, na kwa nje ni shaba. Haijala kitu kamwe, wala kunywa.
8Mfalme akaghadhibika, akawaita makuhani wake, akawaambia, msiponijulisha yu nani anayekula gharama hizo mtakufa. Lakini mkiweza kunihakikishia ya kuwa ndiye Beli azilaye, hapo Danieli atakufa kwa kuwa amemkufuru Beli.
9Danieli akamwambia mfalme, Na iwe hivyo kama ulivyosema. Nao makuhani wa Beli walikuwa watu sabini, bila wake zao na watoto wao.
10Mfalme akaingia pamoja na Danieli katika nyumba ya Beli.
11Makuhani wa Beli wakasema, Haya, tazama, sisi tutaondoka. Na wewe, Ee mfalme, pakua chakula, uchanganye divai na kuiandaa. Kisha, ufunge mlango kabisa, na kuutia mhuri kwa pete yako mwenyewe. Basi, utakapofika asubuhi, usipoona ya kuwa Beli amekula vyote, tutakufa. Ama sivyo, atakufa Danieli anayetusingizia kwa uongo.
12Wala hawakuogopa neno, kwa kuwa chini ya meza walikuwa wamefanya mlango wa kuingilia kwa siri, na humo walizoea kuingia kila mara kuvila vitu vile.
13Ikawa walipokwisha kutoka, mfalme aliviandaa vyakula mbele ya Beli.
14Lakini Danieli aliwaagiza watumsihi wake walete majivu na kuyatapanya hekaluni mwote, hali akiwamo mfalme peke yake. Kisha wakatoka, wakaufunga mlango, wakautia mhuri kwa pete ya mfalme, wakaenda zao.
15Hata usiku wakaja makuhani pamoja na wake zao na watoto wao, kama ilivyokuwa desturi yao, wakala na kunywa vyote.
16Asubuhi mfalme akaondoka mapema, na Danieli pamoja naye.
17Mfalme akasema, Je, Danieli, mhuri ni mzima? Akasema, Ndiyo, mfalme, ni nzima.
18Basi, mara alipoufungua mlango, mfalme alitazama mezani, akalia kwa sauti kubwa, Ee Beli, wewe mkuu, wala kwako hakuna udanganyifu!
19Ndipo Danieli alicheka, akamzuia mfalme asiingie ndani. Akasema, Tazama sakafuni, uziangalie nyayo hizi, ni za nani.
20Mfalme akasema, Naona nyayo za wanaume na wanawake na watoto.
21Ndipo mfalme akakasirika, akawachukua makuhani pamoja na wake zao na watoto wao, wakamwonesha ile milango ya siri ambayo waliingia na kuvila vyakula vilivyowekwa mezani.
22Basi, mfalme akawaua, akampa Danieli amri juu ya Beli, naye aliiharibu sanamu pamoja na hekalu lake.
23Ikawa mahali pale pale palikuwa na Dragoni kubwa ambalo watu wa Babeli walikuwa wakiliabudu.
24Mfalme akamwambia Danieli, Na hili pia utasema ni shaba? Tazama, li hai; hula, hunywa. Huwezi kusema ya kuwa si mungu hai. Basi, liabudu.
25Danieli akasema, Mimi nitamwabudu BWANA, Mungu wangu, maana Yeye ndiye Mungu hai. Lakini, mfalme, nipe ruhusa, nami nitaliua joka hili pasipo mkuki wala rungu.
26Mfalme akasema, Nakupa ruhusa.
27Basi, Danieli akachukua lami na shahamu na nywele, akavitokosa pamoja, akafanya madonge akayatia kinywani mwa joka. Dragoni likayameza, likapasuka katikati. Danieli akasema, Tazameni! Hii ndiyo miungu mnayoiabudu!
28Watu wa Babeli waliposikia habari hiyo walighadhibika sana, wakafanya shauri juu ya mfalme wakisema, Mfalme amekuwa Myahudi. Amemharibu Beli na kuliua Dragoni, na kuwachinja makuhani kwa upanga.
29Basi, wakamwendea mfalme wakasema, Tutolee huyu Danieli, ama sivyo tutakuharibu wewe pamoja na nyumba yako.
30Basi, mfalme alipoona ya kuwa wanamsonga sana na kumshurutisha, aliwatolea Danieli.
31Nao wakamtupa katika tundu la simba, na humo akakaa siku sita.
32Na katika tundu walikuwamo simba saba, ambao kila siku walipewa watu wawili na kondoo wawili. Ila wakati huo hawakupewa, ili makusudi wamle Danieli.
33Basi, huko Uyahudi alikuwa nabii Habakuki, naye alikuwa amepika chakula na kumega mkate katika bakuli, akawa anakwenda shamba kuwapelekea wavunaji.
34Lakini malaika wa BWANA alimwambia Habakuki, Nenda ukapeleke chakula ulicho nacho mpaka Babeli kwa Danieli, aliomo katika tundu la simba.
35Habakuki akasema, BWANA, sijafika Babeli hata siku moja, wala sijui tundu la simba liko wapi.
36Malaika wa BWANA akamshika utosini, akamwinua kwa nywele za kichwa chake, na kwa uvumi wa pumzi yake alimweka Babeli juu ya tundu la simba.[#Eze 8:3]
37Habakuki akapaza sauti yake akasema, Danieli! Danieli! Kitwae chakula Mungu alichokuletea.
38Danieli akasema, Ee Mungu, umenikumbuka, wala huwaachi wao wakupendao. Basi, Danieli akaondoka akala.
39Naye malaika wa BWANA akamrudisha Habakuki mahali pake mara.
40Siku ya saba mfalme akaja ili kumwombolezea Danieli. Alipofika penye tundu na kutazama ndani, kumbe, Danieli yumo, ameketi.
41Ndipo mfalme akapaza sauti yake akasema, Ee BWANA, Mungu wa Danieli, Wewe ndiwe uliye mkuu, wala hakuna mwingine ila Wewe.
42Akamtoa Danieli, akawatupa tunduni wale waliotaka kumwangamiza, nao mara wakaliwa pale pale mbele ya uso wake.