The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa tatu wa kutawala kwake mfalme Belshaza maono yalinitokea mimi, naam, mimi Danieli, baada ya hayo yaliyonitokea hapo kwanza.
2Nami niliona katika maono; nilipokuwa natazama na nikajionea mwenyewe nikiwa huko Susa, Mji mkuu wa mkoa wa Elamu; nikaona katika maono, nami nilikuwa karibu na mto Ulai.[#Neh 1:1; Est 2:8; Mwa 10:22]
3Ndipo nikainua macho yangu nikaona, na tazama, mbele ya mto alisimama kondoo dume, mwenye pembe mbili; na pembe zile mbili zilikuwa ndefu; lakini moja ilikuwa ndefu kuliko ya pili, na ile iliyokuwa ndefu zaidi ilizuka mwisho.
4Nikamwona huyo kondoo dume akisukuma upande wa magharibi, na upande wa kaskazini, na upande wa kusini; wala hakuna mnyama yeyote awezaye kusimama mbele yake, wala hakuna mnyama yeyote awezaye kupokonya mkononi mwake; lakini alitenda kama alivyopenda mwenyewe, akajitukuza nafsi yake.[#Dan 11:3]
5Nami nilipokuwa nikifikiri, tazama, beberu akatoka upande wa magharibi, juu ya uso wa dunia nzima, bila kuigusa nchi; na beberu yule alikuwa na pembe mashuhuri kati ya macho yake.
6Naye akamwendea huyo kondoo dume mwenye pembe mbili, niliyemwona akisimama karibu na mto, akamshambulia kwa ghadhabu za nguvu zake.
7Nikamwona akimkaribia kondoo dume, akamwonea hasira kali, akampiga kondoo dume, akazivunja pembe zake mbili; na huyo kondoo dume alikuwa hana nguvu kusimama mbele yake; bali akamwangusha chini, akamkanyagakanyaga; wala hapakuwapo awezaye kumwokoa kondoo dume katika mkono wake.
8Na yule beberu akajitukuza sana; na alipokuwa na nguvu, pembe ile kubwa ilivunjika; na badala yake zikazuka pembe nne mashuhuri zilizoelekea pepo nne za mbinguni.[#Dan 7:6]
9Na katika moja ya pembe hizo ilitokea pembe ndogo, iliyokua sana, upande wa kusini, na upande wa magharibi, na upande wa nchi ya uzuri.[#Dan 11:25; Zab 48:2]
10Nayo ikakua, kiasi cha kulifikia jeshi la mbinguni; ikaangusha chini baadhi ya jeshi lile, na ya nyota, ikazikanyaga.[#Isa 14:13; Dan 11:28; Ufu 12:4]
11Naam, ikajitukuza hata juu yake aliye mkuu wa jeshi hilo, ikamwondolea sadaka ya kuteketezwa ya daima, na mahali pa patakatifu pake pakaangushwa chini.[#Yer 48:26; Dan 5:23; 2 The 2:4]
12Na jeshi likatolewa kwake pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya daima, kwa sababu ya makosa; nayo ikaiangusha kweli hata chini; ikatenda ilivyopenda, na kufanikiwa.
13Kisha nikamsikia mtakatifu mmoja akinena, na mtakatifu mwingine akamwuliza huyo aliyenena, Haya maono kuhusu habari ya sadaka ya kuteketezwa ya daima, na lile kosa liletalo ukiwa, yataendelea hata lini, kukanyaga patakatifu na jeshi?[#1 Pet 1:12]
14Akamwambia, Hata nyakati za jioni na asubuhi elfu mbili na mia tatu; ndipo patakatifu patakapotakaswa.
15Ikawa mimi, naam, mimi Danieli, nilipoyaona maono hayo, nilitafuta kuyafahamu, na tazama, alisimama mbele yangu mmoja mfano wa mwanadamu.
16Nikasikia sauti ya mwanadamu katikati ya mto Ulai, iliyoita na kusema, Gabrieli, mfahamishe mtu huyu maono haya.[#Dan 9:21; Lk 1:19,26]
17Basi alipakaribia mahali niliposimama; nami niliogopa alipokaribia, nikaanguka kifudifudi; lakini aliniambia, Fahamu, Ee mwanadamu, kwa maana maono haya ni ya wakati wa mwisho.[#Ufu 1:17]
18Basi alipokuwa akisema nami, nilishikwa na usingizi mzito na uso wangu uliielekea nchi; lakini alinigusa, akanisimamisha wima.
19Akaniambia, Tazama, nitakujulisha yatakayokuwa wakati wa mwisho wa ghadhabu; maana, ni ya wakati wa mwisho ulioamriwa.
20Yule kondoo dume uliyemwona, mwenye pembe mbili, hizo ndizo wafalme wa Umedi na Uajemi.
21Na yule beberu, mwenye manyoya mengi, ni mfalme wa Ugiriki; na ile pembe kubwa iliyo kati ya macho yake ni mfalme wa kwanza.
22Tena katika habari ya pembe ile iliyovunjika, ambayo badala yake zilisimama pembe nne, falme nne zitasimama kutoka katika taifa lile, lakini si kwa nguvu kama zake.
23Na wakati wa mwisho wa ufalme wao, wakosaji watakapotimia kilele cha uovu wao, mfalme mwenye uso mkali, afahamuye mafumbo, atasimama.[#Kum 28:50]
24Na nguvu zake zitakuwa nyingi mno, lakini si kwa uwezo wake mwenyewe; naye ataharibu kiasi cha kustaajabisha watu, na kufanikiwa, na kutenda apendavyo; naye atawaangamiza hao walio hodari na watu watakatifu.[#Ufu 13:7]
25Na kwa mashauri yake atafanikisha hila mkononi mwake; naye atajitukuza nafsi yake moyoni mwake; naye atawaangamiza wengi katika hali yao ya salama; naye atasimama kushindana naye aliye Mkuu wa wakuu; lakini atavunjika, bila kazi ya mikono.[#Ayu 34:20; Omb 4:6]
26Na maono ya hizo nyakati za jioni na asubuhi yaliyosemwa ni kweli; lakini wewe yafunike maono hayo; maana ni ya wakati ujao baada ya siku nyingi.[#Eze 12:27; Dan 10:14; Ufu 22:10]
27Na mimi, Danieli, nikazimia, nikaugua siku kadhaa; kisha nikaondoka, nikatenda shughuli za mfalme; nami niliyastajabia yale maono, ila hakuna aliyeyafahamu.[#Dan 2:48,49]