The chat will start when you send the first message.
1Baada ya hayo mfalme Ahasuero alimpandisha cheo Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, akamwinua, akamwekea kiti chake juu ya wakuu wote waliokuwapo pamoja naye.[#3:1 Agagi alikuwa mfalme wa Amaleki, wa Israeli.]
2Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi langoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo mfalme alivyoamuru wamfanyie. Lakini Mordekai hakumwinamia, wala kumsujudia.
3Basi watumishi wa mfalme walioketi langoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waivunja amri ya mfalme?
4Ikawa, waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi.
5Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hamwinamii wala kumsujudia, alighadhibika sana.
6Akaona haitoshi kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila lake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai.
7Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hadi mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari.
8Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna watu wa taifa moja waliotawanyika na kukaa kila mahali katikati ya watu wa mataifa walioko katika mikoa yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimetofautiana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao.
9Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta elfu kumi za fedha mikononi mwa watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme.
10Ndipo mfalme alipoivua pete yake ya kupigia mhuri kutoka mkononi, akampa Hamani mwana wa Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi.
11Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema.
12Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza; na barua zikaandikwa, kama vile Hamani alivyoagiza, kwa wakuu wa mfalme, na wakuu wa mikoa, na wakuu wa kila taifa; kila mkoa kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; zikaandikwa kwa jina la mfalme Ahasuero, na kutiwa mhuri kwa pete yake.
13Barua zikapelekwa kwa mikono ya matarishi mpaka mikoani yote ya mfalme kuwaangamiza Wayahudi wote, na kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee, watoto wachanga na wanawake pia, siku moja, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili ndio mwezi wa Adari; na kuyapora mali yao.