Kutoka 15

Kutoka 15

Wimbo wa Musa

1Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia BWANA wimbo huu wakanena, na kusema,[#Ufu 15:3; Amu 5:1; 2 Sam 22:1]

Nitamwimbia BWANA, kwa maana ametukuka sana;

Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.

2BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu;[#Zab 118:14; Isa 12:2; 2 Sam 22:47; Zab 99:5; #15:2 ‘Au uwezo’.]

Naye amekuwa wokovu wangu.

Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu;

Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.

3BWANA ni mtu wa vita,[#Ufu 19:11; Zab 83:18]

BWANA ndilo jina lake.

4Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini,

Maofisa wake wateule wamezama katika Bahari ya Shamu.

5Vilindi vimewafunikiza,

Walizama vilindini kama jiwe.

6BWANA, mkono wako wa kulia umepata fahari ya uwezo,[#Zab 118:15]

BWANA, mkono wako wa kulia wawasetaseta adui.

7Kwa wingi wa ukuu wako wawaangusha chini wanaokupinga,[#Zab 59:13; Kum 4:24; Ebr 12:20; Isa 5:24]

Huwatumia hasira yako nayo huwateketeza kama mabua makavu.

8Kwa upepo wa mianzi ya pua yako maji yalipandishwa,[#Ayu 4:9; Hab 3:10]

Mawimbi yakasimama juu wima mfano wa kilima,

Vilindi vikagandamana katikati ya bahari.

9Adui akasema, Nitafuata, nitapata, nitagawanya nyara,[#Isa 53:12; Lk 11:22]

Nafsi yangu itashibishwa na wao;

Nitaufuta upanga wangu, mkono wangu utawaangamiza.

10Ulivuma kwa upepo wako, bahari ikawafunikiza;

Wakazama kama risasi ndani ya maji makuu.

11Ee BWANA, katika miungu ni nani aliye kama wewe?[#2 Sam 7:22; 1 Fal 8:23; Zab 86:8; Yer 49:19]

Ni nani aliye kama wewe, mtukufu katika utakatifu,

Mwenye kuogopwa katika sifa zako, mfanya maajabu?

12Ulinyosha mkono wako wa kulia,

Nchi ikawameza.

13Wewe kwa rehema zako umewaongoza watu uliowakomboa,[#Zab 78:54]

Kwa uweza wako uliwaelekeza hata makao yako matakatifu.

14Makabila ya watu wamesikia, wanatetemeka,[#Yos 2:9; Zab 48:6]

Wakazi wa Ufilisti uchungu umewashika.

15Ndipo majumbe wa Edomu wakashangaa,[#Hab 3:7]

Watu wa Moabu wenye nguvu tetemeko limewapata,

Watu wote wakaao Kanaani wameyeyuka.

16Hofu na woga zimewaangukia;[#Kum 2:25; 1 Sam 25:37; Kum 32:9; Isa 43:1; Yer 31:11; Tit 2:14; 1 Pet 2:9; 2 Pet 2:1]

Kwa uweza wa mkono wako wanakaa kimya kama jiwe;

Hata watakapovuka watu wako, Ee BWANA,

Hata watakapovuka watu wako uliowanunua.

17Utawaingiza, na kuwapanda katika mlima wa urithi wako,[#Zab 44:2]

Mahali pale ulipojifanyia, Ee BWANA, ili upakae,

Pale patakatifu ulipopaweka imara, BWANA, kwa mikono yako.

18BWANA atatawala milele na milele.

19Kwa maana farasi wa Farao na magari yake na wapanda farasi wake waliingia ndani ya bahari, BWANA akayarudisha maji ya bahari juu yao; bali wana wa Israeli walikwenda katika nchi kavu katikati ya bahari.

Wimbo wa Miriamu

20Na Miriamu, nabii mwanamke, dada yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza.[#Amu 11:34; 21:21; 1 Nya 15:16; 1 Sam 18:6; Zab 68:25; 81:2; Yer 31:4]

21Miriamu akawaitikia,

Mwimbieni BWANA kwa maana ametukuka sana;

Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.

Maji machungu yafanywa kuwa matamu

22Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.

23Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara[#Hes 33:8; Rut 1:20; #15:23 Katika Kiebrania maana yake ni ‘Uchungu’.]

24Ndipo watu wakamnung'unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?

25Naye akamlilia BWANA; BWANA akamwonesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawajaribu huko;[#Kut 14:10; 17:4; Zab 50:15; 2 Fal 2:21; 4:41; Yos 24:25; Kut 16:4; Kum 8:2,16; Zab 66:10; 81:7]

26akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya BWANA, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yoyote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi BWANA nikuponyaye.[#Kum 7:12; 28:27; Kut 23:25; Zab 103:3; 147:3]

27Wakafika Elimu, palipokuwa na chemchemi kumi na mbili, na mitende sabini; wakapiga kambi hapo, karibu na maji.[#Hes 33:9]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya