Kutoka 8

Kutoka 8

1BWANA akamwambia Musa, Ingia kwa Farao, ukamwambie, BWANA asema hivi, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia.[#Kut 3:12]

2Tena kama ukikataa kuwapa ruhusa, tazama, nitaipiga mipaka yako yote kwa kuleta vyura;[#Kut 7:14; 9:2; Ufu 16:13]

3na huo mto utafurika vyura, nao watakwea juu na kuingia ndani ya nyumba yako, na ndani ya chumba chako cha kulala, na juu ya kitanda chako, na ndani ya nyumba ya watumishi wako, na juu ya watu wako, na ndani ya meko yako, na ndani ya vyombo vyako vya kukandia unga.[#Zab 105:30]

4Kisha hao vyura watakwea juu yako wewe, na juu ya watu wako, na juu ya watumishi wako wote.

5BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha mkono wako na fimbo yako juu ya mito, juu ya vijito, na juu ya maziwa ya maji, ukawalete vyura waje juu ya nchi yote ya Misri.[#Kut 7:19]

6Basi Haruni akaunyosha mkono wake juu ya maji yote ya Misri; na hao vyura wakakwea juu, wakaifunika nchi ya Misri.[#Zab 78:45; 105:30]

7Waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na kuwaleta vyura juu ya nchi ya Misri.[#Kut 7:11]

8Ndipo Farao akawaita Musa na Haruni na kuwaambia, Mwombeni BWANA, ili awaondoe vyura hawa kwangu mimi na kwa watu wangu; nami nitawapa watu ruhusa waende zao, ili wamtolee BWANA dhabihu.[#Kut 9:28; 10:17; Hes 21:7; 1 Fal 13:6; Mdo 8:24]

9Musa akamwambia Farao, Haya, ujitukuze juu yangu katika jambo hili; sema ni lini unapotaka nikuombee wewe, na watumishi wako, na watu wako, ili hao vyura waangamizwe watoke kwako wewe na nyumba zako, wakae ndani ya mto tu.

10Akamwambia, Kesho, Akasema, Na yawe kama neno lako; ili upate kujua ya kwamba hapana mwingine mfano wa BWANA, Mungu wetu.[#Kut 9:14; Kum 33:26; 2 Sam 7:22; 1 Nya 17:20; Zab 86:8; Isa 46:9; Yer 10:6,7]

11Hao vyura wataondoka kutoka kwako wewe na nyumba zako, na watumishi wako, na watu wako; watasalia mtoni tu.

12Basi Musa na Haruni wakatoka kwa Farao; Musa akamlilia BWANA katika jambo la hao vyura aliokuwa amewaleta juu ya Farao.[#Kut 9:33; 10:18; 32:11; Yak 5:16-18]

13BWANA akafanya sawasawa na neno la Musa; na hao vyura wakafa kutoka katika zile nyumba, na katika viwanja, na katika mashamba.

14Wakawakusanya marundo marundo; na nchi ikatoa uvundo.

15Lakini Farao alipoona ya kuwa pana nafuu, akaufanya moyo wake kuwa mzito, asiwasikize; kama BWANA alivyonena.[#Mhu 8:11; Mit 21:29]

16BWANA akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Nyosha fimbo yako, ukayapige mavumbi ya nchi, ili kwamba yawe chawa katika nchi yote ya Misri.

17Nao wakafanya hivyo; Haruni akaunyosha mkono wake na fimbo yake, na kuyapiga mavumbi ya nchi, nayo yakawa chawa juu ya wanadamu na juu ya wanyama; mavumbi yote ya nchi yakawa ni chawa katika nchi yote ya Misri.[#Zab 105:31]

18Hao waganga nao wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao, ili kwamba walete chawa, lakini wasiweze; nako kulikuwa na chawa juu ya wanadamu, na juu ya wanyama.[#Kut 7:11; Lk 10:18; 2 Tim 3:8,9]

19Ndipo wale waganga wakamwambia Farao, Jambo hili ni kidole cha Mungu; na moyo wake Farao ukawa mgumu asiwasikize; vile vile kama BWANA alivyonena.[#Lk 11:20; 1 Sam 6:3,9; Ayu 27:11; Zab 8:3; Mt 12:28; Mdo 13:11; #8:19 Katika Kiebrania ina maana ya ‘Nguvu ya Kimungu’ au ‘mkono wa Mungu’.]

20BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi.[#Kut 7:15]

21Au kwamba huwapi ruhusa watu wangu, tazama, nitaleta inzi wengi sana juu yako wewe, na juu ya watumishi wako, na juu ya watu wako, nao wataingia ndani ya nyumba zako; na nyumba za Wamisri zitajawa na inzi wengi sana, na nchi nayo ambayo wa juu yake.

22Nami siku hiyo nitatenga nchi ya Gosheni, watu wangu wanayokaa, ili hao inzi wasiwe huko; ili kwamba upate kujua wewe ya kuwa mimi ndimi BWANA kati ya dunia.[#Kut 9:4,6,26]

23Nami nitatia mpaka kati ya watu wangu na watu wako; ishara hiyo italetwa kesho.[#8:23 Katika Kiebrania ‘nami nitaweka ukombozi’.]

24BWANA akafanya; wakaja inzi wengi kwa uzito sana, wakaingia nyumbani mwa Farao, na katika nyumba za watumishi wake, tena katika nchi yote ya Misri; nayo nchi iliharibiwa na wale inzi.[#Zab 78:45]

25Farao akawaita Musa na Haruni akawaambia, Endeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu ndani ya nchi hii.

26Musa akasema, Haitupasi kufanya hivyo; kwa kuwa tutamchinjia sadaka BWANA, Mungu wetu, na hayo machukizo ya Wamisri; je! Tutachinja sadaka ya hayo machukizo ya Wamisri mbele ya macho yao, wasitupige kwa mawe?

27La, tutakwenda safari ya siku tatu jangwani, tumchinjie dhabihu BWANA, Mungu wetu, kama atakavyotuagiza.[#Kut 3:12,18]

28Farao akasema, Mimi nitawapa ruhusa mwende, ili mmchinjie dhabihu BWANA, Mungu wenu, jangwani; lakini hamtakwenda mbali sana; haya niombeeni.[#Kut 9:28; 1 Fal 13:6; Ezr 6:10; Mdo 8:24]

29Musa akasema, Tazama, mimi natoka kwako, nami nitamwomba BWANA ili hao inzi wamtoke Farao, na watumishi wake, na watu wake kesho; lakini Farao asitende kwa udanganyifu tena, kwa kutowaacha watu waende kumchinjia BWANA dhabihu.

30Musa akatoka kwa Farao, akamwomba BWANA.

31BWANA akafanya kama neno la Musa, akawaondoa wale inzi wabaya kwake Farao, na kwa watumishi wake, na watu wake; hakusalia hata mmoja.[#Yak 5:17]

32Farao akaufanya moyo wake kuwa mzito mara hiyo nayo, wala hakuwapa ruhusa hao watu waende zao.[#Kut 4:21; Mit 28:14; Rum 9:17-23; Yak 1:13-17]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya