The chat will start when you send the first message.
1Ikawa njaa katika nchi hiyo, mbali na njaa ile ya kwanza iliyokuwa siku za Abrahamu. Isaka akamwendea Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, huko Gerari.[#Mwa 12:10; 20:2]
2BWANA akamtokea, akasema, Usishuke kwenda Misri, kaa katika nchi nitakayokuambia.[#Mwa 12:1; Zab 37:3]
3Kaa ugenini katika nchi hiyo, nami nitakuwa pamoja nawe, na kukubariki, maana nitakupa wewe na uzao wako nchi hizi zote. Nami nitakifanya imara kiapo nilichomwapia Abrahamu baba yako.[#Mwa 22:16-18; Mwa 20:1; 28:15; Zab 39:12; Ebr 11:9; Mwa 12:2; 13:15; Zab 105:9]
4Nitazidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, nami nitawapa uzao wako nchi hizi zote, na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia.[#Zab 72:17]
5Kwa sababu Abrahamu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na amri zangu, na hukumu zangu, na sheria zangu.[#Mwa 22:16]
6Isaka akakaa katika Gerari.
7Watu wa mahali hapo wakamwuliza habari za mkewe. Akasema, Ni dada yangu huyu maana aliogopa kusema, Ni mke wangu, watu wa nchi wasije wakamwua kwa ajili ya Rebeka; kwa maana alikuwa mzuri wa uso.[#Mwa 12:13; 20:2; 24:16; Mit 29:25]
8Ikawa alipokuwa amekaa huko siku nyingi, Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, akachungulia dirishani, akamwona Isaka anachezacheza na Rebeka mkewe.
9Abimeleki akamwita Isaka, akasema, Yakini huyu ni mkeo, mbona ulisema, Ni dada yangu huyu? Isaka akamwambia, Kwa sababu nilisema, Nisife kwa ajili yake.
10Abimeleki akasema, Ni nini hii uliyotutendea? Labda mtu mmojawapo angalilala na mkeo bila kufikiri, nawe ungalitutia hatiani.[#Mwa 20:9]
11Basi Abimeleki akawaamuru watu wote, akisema, Amgusaye mtu huyu au mkewe lazima atauawa.[#Zab 105:15]
12Mwaka huo Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, naye akapata mavuno mara mia zaidi. BWANA akambariki.[#Mt 13:8; Mk 4:8; Ayu 42:12; Mt 6:33]
13Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana.[#Mit 10:22]
14Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu.[#Mwa 37:11; Mhu 4:4]
15Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Abrahamu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza udongo.[#Mwa 21:30]
16Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi.[#Kut 1:9]
17Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko.
18Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Abrahamu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Abrahamu; naye akaviita majina kufuata majina aliyoviita babaye.[#Mwa 21:31]
19Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika.
20Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye.[#Mwa 21:25]
21Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna.
22Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.[#Mwa 17:6; Kut 1:7]
23Akapanda kutoka hapo mpaka Beer-sheba.
24BWANA akamtokea usiku uleule, akasema, Mimi ni Mungu wa Abrahamu baba yako, usiogope, maana mimi ni pamoja nawe, nami nitakubariki, na kuzidisha uzao wako kwa ajili ya Abrahamu mtumishi wangu.[#Mwa 15:1; 24:12; 26:3; Kut 3:6; Mdo 7:32; Rum 8:31]
25Akajenga madhabahu huko, akaliitia jina la BWANA. Akapiga hema yake huko, na watumwa wa Isaka wakachimba kisima huko.[#Mwa 12:7; 13:18; Zab 116:17]
26Ndipo Abimeleki akamwendea kutoka Gerari, pamoja na Ahuzathi rafiki yake, na Fikoli, jemadari wa jeshi lake.[#Mwa 21:22]
27Isaka akawauliza, Mbona mwanijia, nanyi mmenichukia, mkanifukuza kwenu?[#Amu 11:7]
28Wakasema, Hakika tuliona ya kwamba BWANA alikuwa pamoja nawe; nasi tukasema, Na tuapiane, sisi na wewe, na kufanya mapatano nawe[#Mwa 21:22,23]
29ya kuwa hutatutenda mabaya, iwapo sisi hatukukugusa wewe, wala hatukukutendea ila mema, tukakuacha uende zako kwa amani; nawe sasa u mbarikiwa wa BWANA.[#Mwa 24:31; Zab 115:15]
30Basi akawafanyia karamu, nao wakala, wakanywa.[#Mwa 19:3]
31Wakaondoka asubuhi na mapema, wakaapiana wao kwa wao, kisha Isaka akawapa ruhusa, nao wakaenda zao kwa amani.[#Mwa 21:31]
32Ikawa siku ileile, watumwa wa Isaka wakaja wakampasha habari za kile kisima walichokuwa wamekichimba, wakamwambia, Tumeona maji.
33Naye akakiita jina lake Shiba; kwa hiyo jina la mji huo ni Beer-sheba, hata leo.[#Mwa 21:31]
34Esau alipokuwa mwenye miaka arubaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, Mhiti, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti.[#Mwa 36:2]
35Roho zao Isaka na Rebeka zikajaa uchungu kwa ajili yao.[#Mwa 27:46; 28:1,8]