Yakobo 3

Yakobo 3

Kuuchunga ulimi

1Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi.[#Yak 1:19]

2Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.[#Yak 1:26]

3Angalieni, twatia lijamu katika vinywa vya farasi, ili watutii, hivi twageuza mwili wao wote.

4Tena angalieni merikebu; ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, kokote anakoazimia kwenda nahodha.

5Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivunia matendo makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana.

6Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfululizo wa maumbile, nao huwashwa moto na Jehanamu.[#Mt 15:11,18,19; 12:36,37]

7Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu.

8Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.[#Zab 140:3]

9Kwa huo tunamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo unwawalaani wanadamu walioumbwa kwa mfano wa Mungu.[#Mwa 1:26]

10Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.

11Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu?

12Ndugu zangu, Je! Mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Kadhalika chemchemi haiwezi kutoa maji ya chumvi na maji matamu.

Aina mbili za hekima

13Ni nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aoneshe kazi zake kwa mwenendo wake mzuri, katika upole wa hekima.[#Yak 2:18; 1 Pet 2:12]

14Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli.[#Efe 4:31]

15Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya kidunia, ya tabia ya kibinadamu, na ya kishetani.[#Yak 1:5,17]

16Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya.

17Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki.[#Ebr 12:11]

18Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.[#Isa 32:17; Mt 5:9]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya