Waamuzi 12

Waamuzi 12

Makabila yazozana

1Kisha watu wa Efraimu walikusanyika na kuvuka hadi Zafoni; wakamwambia Yeftha, Kwa nini ulivuka kwenda kupigana na wana wa Amoni, nawe hukutuita sisi kwenda pamoja nawe? Tutaichoma nyumba yako juu yako.[#Amu 8:1]

2Yeftha akawaambia, Mimi na watu wangu tulikuwa na mzozo mkali na wana wa Amoni; nami hapo nilipowaita ninyi, hamkuniokoa na mikono yao.

3Nami nilipoona ya kuwa ninyi hamniokoi, niliuhatarisha uhai wangu, na kuvuka ili nipigane na wana wa Amoni, BWANA naye akawatia mkononi mwangu; basi kwa nini ninyi kunijia hivi leo kutaka kupigana nami?[#1 Sam 19:5; 28:21; Ayu 13:14; Zab 119:109; Rum 16:4; Ufu 12:11]

4Ndipo Yeftha akawakutanisha watu wote wa Gileadi, na kupigana na Efraimu; na hao watu wa Gileadi wakawapiga Efraimu, kwa sababu walisema, Ninyi Wagileadi ni watoro mliotoroka Efraimu, na kukaa kati ya Efraimu na Manase.[#1 Sam 25:10; Zab 78:9]

5Nao Wagileadi wakavitwaa vivuko vya Yordani kinyume cha hao Waefraimu; kisha kila mmoja wa watoro walitoroka Efraimu aliposema “Niache nivuke”, hao watu wa Gileadi walimuuliza, “Je! Wewe ni Mwefraimu?” Alijibu, la;[#Yos 22:11; Amu 3:28; 7:24]

6ndipo walipomwambia, Haya, tamka sasa neno hili, Shibolethi; naye akasema, Sibolethi; kwa maana hakuweza kufanya midomo yake kutamka neno hilo sawasawa; ndipo wakamshika, na kumwua hapo penye vivuko vya Yordani; basi wakaanguka watu elfu arubaini na mbili wa Efraimu wakati huo.

7Huyo Yeftha akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka sita. Ndipo akafa Yeftha, Mgileadi, akazikwa katika miji ya Gileadi mmojawapo.

Ibzani, Eloni na Abdoni

8Baada ya Yeftha, Ibzani wa Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli.

9Alikuwa na watoto thelathini wa kiume; na binti thelathini aliwaoza nje ya ukoo wake, kisha akaleta wanawake thelathini kutoka mahali pengine kwa ajili ya hao wanawe. Akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka saba.

10Huyo Ibzani akafa, akazikwa huko Bethlehemu.

11Baada ya Ibzani, Eloni, Mzabuloni, akawa mwamuzi wa Israeli akawaamua Israeli muda wa miaka kumi.

12Huyo Eloni, Mzabuloni, akafa, akazikwa katika Aiyaloni katika nchi ya Zabuloni.

13Baada ya Eloni, Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akawa mwamuzi wa Israeli.

14Naye alikuwa na wana arubaini, na wajukuu thelathini, waliokuwa wakipanda wanapunda sabini; akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka minane.[#Amu 5:10; 10:4]

15Huyo Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akafa, akazikwa huko Pirathoni katika nchi ya Efraimu, katika nchi ya vilima ya Waamaleki.[#Mwa 14:7; Kut 17:8; Amu 3:13; 5:14]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya