Waamuzi 15

Waamuzi 15

Samsoni awashinda Wafilisti

1Lakini ikawa baadaye, wakati wa mavuno ya ngano Samsoni akaenda kumtazama mkewe, akamchukulia mwana-mbuzi; akasema, Nitaingia chumbani kwa mke wangu. Lakini baba yake mwanamke hakumwacha kuingia.[#Mwa 38:17; 1 Sam 16:20; Lk 15:29]

2Baba yake akasema, Hakika mimi nilidhani ya kuwa umemchukia kabisa; basi nilimpa rafiki yako. Je! Si dada yake mdogo ni mzuri kuliko yeye? Tafadhali, mtwae huyo badala yake.[#Amu 14:20]

3Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia kwa hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru.

4Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa mienge ya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia mwenge kati ya kila mikia miwili.[#Wim 2:15; Eze 13:4]

5Alipokwisha kuiwasha moto ile mienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni.

6Ndipo Wafilisti wakasema, Ni nani aliyetenda hivi? Wakasema, Ni huyo Samsoni, mkwewe yule Mtimna, kwa sababu alimchukua mkewe akampa mwenzake. Wafilisti wakaenda wakamteketeza yeye na baba yake kwa moto.[#Amu 14:15]

7Samsoni akawaambia, Ikiwa ninyi mnafanya mambo kama hayo, hakika sitakoma hadi nitakapojilipizia kisasi juu yenu.

8Ndipo akawashambulia vikali na kuwaua wengi, kisha akateremka na kukaa katika ufa wa jabali la Etamu.[#1 Nya 4:3; 2 Nya 11:6]

9Basi Wafilisti wakapanda wakapiga kambi yao katika Yuda, wakashambulia Lehi.

10Watu wa Yuda wakasema, Mbona mmekuja kupigana nasi? Wakasema, Tumepanda ili kumfunga Samsoni, kumtenda yeye kama alivyotutenda sisi.

11Ndipo watu elfu tatu wa Yuda wakateremka hadi katika ule ufa wa jabali la Etamu, wakamwambia Samsoni, Je! Hujui ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hii, basi, uliyotutenda? Akawaambia, Kadiri ile walivyonitenda mimi, ndivyo nilivyowatenda wao.[#Law 26:25; Kum 28:43,44; Amu 2:13,14; 14:4; Neh 9:26,27; Zab 78:58,61,62; 106:40-42; Omb 1:5]

12Wakamwambia, Tumeshuka ili kukufunga, tupate kukutia katika mikono ya Wafilisti. Samsoni akawaambia, Niapieni ya kwamba ninyi wenyewe hamtaniua.

13Wakamwambia, wakisema, Vema, lakini tutakufunga sana, na kukutia katika mikono yao; lakini hakika hatutakuua. Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya, wakamchukua kutoka huko jabalini.

14Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo Roho ya BWANA ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake.

15Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akaua watu elfu moja kwa mfupa huo;[#Law 26:8; Kum 32:30; Yos 23:10; Amu 3:31; 1 Sam 14:6,12-16; 2 Sam 23:8]

16Samsoni akasema,

Kwa taya ya punda, chungu juu ya chungu,

Kwa taya ya punda nimeua watu elfu moja.

17Ikawa, alipokuwa amekwisha kunena akautupa ule mfupa wa taya mkononi mwake; na mahali pale pakaitwa Ramath-lehi.[#15:17 maana yake ni Kilima cha taya.]

18Kisha akaona kiu sana, akamwita BWANA akasema, Wewe umetupa wokovu huu kwa mkono wa mtumishi wako; na sasa nitakufa kwa kiu, na kuanguka katika mikono ya watu wasiotahiriwa.[#Zab 3:7]

19Lakini Mungu akapasua mahali penye shimo palipo katika Lehi, pakatoka maji; naye alipokunywa, roho yake ikamrudia, akaburudika; kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Enhakore, napo pa katika Lehi hata hivi leo.[#Mwa 45:27; Isa 40:29; 57:15; #15:19 maana yake ni Kijicho cha mwombaji.]

20Naye akawa mwamuzi wa Israeli: katika siku za Wafilisti muda wa miaka ishirini.[#Amu 13:1]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya