Yeremia 37

Yeremia 37

Tumaini la bure la Sedekia

1Na Sedekia, mwana wa Yosia, akamiliki baada ya Konia, mwana wa Yehoyakimu, ambaye Nebukadneza amemfanya mtawala katika nchi ya Yuda.[#1 Nya 3:16; Dan 1:1; 2 Fal 24:17; 2 Nya 36:10]

2Lakini yeye, wala watumishi wake, wala watu wa nchi, hawakuyasikiliza maneno ya BWANA aliyonena kwa kinywa cha nabii Yeremia.[#2 Fal 24:19,20; Mit 29:12]

3Sedekia, mfalme, akamtuma Yehukali, mwana wa Shelemia, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, kwa Yeremia, nabii, kusema, Utuombee sasa kwa BWANA, Mungu wetu.[#Yer 21:1,2]

4Basi Yeremia alikuwa akiingia na kutoka kati ya watu; kwa maana walikuwa hawajamfunga gerezani.

5Na jeshi la Farao lilikuwa limetoka nchi ya Misri; na Wakaldayo waliohusuru Yerusalemu, waliposikia habari zao, wakavunja kambi yao mbele ya Yerusalemu.[#2 Fal 24:7; Yer 34:21]

6Ndipo neno la BWANA likamjia nabii Yeremia, kusema,

7BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mtamwambia hivi mfalme wa Yuda, aliyewatuma kwangu kuniuliza; Angalieni, jeshi la Farao, ambalo linakuja kuwasaidia, litarudi Misri, nchi yao wenyewe.[#Yer 21:2]

8Na Wakaldayo watakuja tena, na kupigana na mji huu; nao watautwaa, na kuuteketeza.[#Zab 33:10; Mit 21:30; Isa 30:1-7; Yer 34:22]

9BWANA asema hivi, Msijidanganye mkisema, Bila shaka Wakaldayo watatuacha na kwenda zao; maana hawatawaacha.

10Maana mngelipiga jeshi lote la Wakaldayo wanaopigana nanyi, wakabaki kati yao watu waliojeruhiwa tu, hata hivyo wangeondoka kila mtu katika hema yake, na kuuteketeza mji huu.[#Law 26:36-38; Isa 30:17; Yer 21:4,5]

Yeremia atiwa gerezani

11Hata ikawa, jeshi la Wakaldayo lilipokuwa limevunja kambi yao mbele ya Yerusalemu, kwa kuliogopa jeshi la Farao,

12ndipo Yeremia akatoka Yerusalemu, ili aende mpaka katika nchi ya Benyamini, alipokee huko fungu lake kati ya watu.

13Naye alipokuwa katika lango la Benyamini, mkuu wa walinzi alikuwapo, jina lake Iriya, mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania; akamkamata Yeremia, nabii, akisema, Unakwenda kujiunga na Wakaldayo.

14Ndipo Yeremia akasema, Ni uongo, siendi kujiunga na Wakaldayo; lakini yeye asimwamini; basi Iriya akamkamata Yeremia, akamleta kwa wakuu.

15Nao wakuu wakamkasirikia Yeremia, wakampiga, wakamtia gerezani katika nyumba ya Yonathani, mwandishi; kwa maana ndiyo waliyoifanya kuwa gereza.[#Yer 20:1-3; Mt 21:35; Yn 18:22; Mdo 5:40; Mwa 30:20; Yer 38:26; Mdo 12:6; Ufu 2:10]

16Basi, Yeremia alipokuwa ameingia katika nyumba ya shimo, na katika vyumba vya ndani; na Yeremia alipokuwa amekaa humo siku nyingi;[#Yer 38:6]

17ndipo Sedekia, mfalme, akatuma watu wamlete; naye mfalme akamwuliza kwa siri ndani ya nyumba yake, akasema, Je! Liko neno lililotoka kwa BWANA? Yeremia akasema, Liko. Akasema pia, Utatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli.[#Mk 6:20]

18Pamoja na haya Yeremia akamwambia mfalme Sedekia, Nimefanya kosa gani juu yako, au juu ya watumishi wako, au juu ya watu hawa, hata mkanitia gerezani?

19Wako wapi sasa manabii wenu waliowatabiria, wakisema, Mfalme wa Babeli hatakuja juu yenu, wala juu ya nchi hii?

20Na sasa unisikilize, Ee bwana wangu mfalme; maombi yangu yakapate kibali mbele yako; usinirudishe nyumbani mwa Yonathani, mwandishi, nisije nikafa humo.

21Ndipo Sedekia mfalme akatoa amri, wakamtia Yeremia katika ukumbi wa walinzi; wakampa kila siku mkate mmoja uliotoka katika njia ya waokaji, hata mkate wote wa mji ulipokwisha. Basi Yeremia akakaa katika ukumbi wa walinzi.[#Yer 32:2; 1 Fal 17:6,9; 2 Fal 25:3; Yer 38:9; 2 Kor 6:4]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya