The chat will start when you send the first message.
1Neno la BWANA lililomjia Yeremia, nabii, kuhusu mataifa.[#Yer 25:15]
2Kuhusu Misri; habari za jeshi la Farao Neko, mfalme wa Misri, lililokuwa karibu na mto Frati katika Karkemishi, ambalo Nebukadneza, mfalme wa Babeli, alilipiga katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda.[#2 Fal 23:29; 2 Nya 35:20; Yer 25:9,19]
3Tengenezeni kigao na ngao, mkakaribie ili kupigana.[#Isa 8:9,10; Yer 51:11,12; Yoe 3:9,10; Nah 2:1]
4Watandikeni farasi; pandeni, enyi mpandao farasi; simameni na chapeo zenu, isugueni mikuki; zivaeni dirii.
5Nimeyaona haya kwa sababu gani? Wamefadhaika, wamerudi nyuma; mashujaa wao wamevunjikavunjika; wanakimbia upesi sana, hawatazami nyuma; hofu iko pande zote; asema BWANA.[#Yer 6:25; 20:4; Ufu 6:15-17]
6Mtu mwepesi asikimbie, wala shujaa asiokoke; pande za kaskazini karibu na mto Frati wamejikwaa na kuanguka.[#Dan 11:19]
7Nani huyu ajiinuaye kama mto Nile,[#Dan 11:22]
Ambaye maji yake yanajirusha kama mito?
8Misri anajiinua kama mto Nile,
Na maji yake yanajirusha kama mito;
Asema, Nitajiinua, nitaifunika nchi;
Nitauharibu mji na hao wakaao ndani yake.
9Haya! Pandeni, enyi farasi;
Jihimizeni, enyi magari ya vita;
Mashujaa nao na watoke nje
Kushi na Puti, watumiao ngao;
Nao Waludi, washikao uta na kuupinda.
10Maana hiyo ni siku ya Bwana, BWANA wa majeshi,[#Yoe 1:15; Kum 32:42; Isa 34:6]
Siku ya kisasi, ili ajilipize kisasi juu ya adui zake;
Nao upanga utakula na kushiba,
Utakunywa damu yao hata kukinai;
Maana Bwana, BWANA wa majeshi, ana sadaka yake
Katika nchi ya kaskazini karibu na mto Frati.
11Panda uende Gileadi, ukatwae zeri, Ee binti, bikira wa Misri; unatumia dawa nyingi bure tu; hupati kupona kamwe.[#Yer 8:22; Isa 47:1]
12Mataifa wamesikia habari za aibu yako, nayo dunia imejaa kilio chako; maana shujaa amejikwaa juu ya shujaa mwenzake, wameanguka wote wawili pamoja.
13Neno hili ndilo ambalo BWANA alimwambia Yeremia, nabii, kueleza jinsi Nebukadneza, mfalme wa Babeli, atakavyokuja na kuipiga nchi ya Misri.[#Yer 43:10-13; Isa 19:1; Eze 29:20]
14Tangazeni habari hii katika Misri, mkaihubiri katika Migdoli, na kuihubiri katika Nofu, na Tapanesi; semeni, Simama, ujitayarishe kwa maana upanga umekula pande zako zote.
15Mbona mashujaa wako wamechukuliwa mbali? Hawakusimama kwa sababu BWANA aliwafukuza.
16Aliwakwaza wengi, naam, wakaangukiana wao kwa wao; wakasema, Haya! Na tuondoke, tukarudi kwa watu wetu wenyewe, hadi nchi tuliyozaliwa, tuukimbie upanga unaotuonea.[#Law 26:37]
17Wakalia huko, Farao, mfalme wa Misri, ni kishindo tu; muda alioandikiwa ameuacha upite.
18Kama mimi niishivyo, asema Mfalme, ambaye jina lake ni BWANA wa majeshi, hakika yake, kama Tabori katika milima, na kama Karmeli karibu na bahari, ndivyo atakavyokuja.[#Isa 48:2; Mal 1:14; Yer 10:10; 44:26; 1 Tim 1:17; Hes 23:19]
19Ee binti ukaaye katika Misri,[#Yer 48:18]
Ujiweke tayari kwenda zako hali ya kufungwa;
Kwa maana Nofu utakuwa ukiwa,
Utateketezwa, usikaliwe na watu.
20Misri ni mtamba mzuri sana, lakini uharibifu umekuja,[#Hos 10:11; Yer 1:14]
Umekuja utokao pande za kaskazini.
21Na askari wake waliojiwa, walio kati yake,
Ni kama ndama walionona malishoni;
Maana wao nao wamerudi nyuma,
Wamekimbia wote pamoja, wasisimame;
Maana siku ya msiba wao imewafikia,
Wakati wa kujiliwa kwao.
22Sauti yake ni kama nyoka, wajapo kwa nguvu,[#Isa 29:4]
Watamjia na mashoka, kama wachanja kuni.
23Wataukata msitu wake, asema BWANA, ingawa haupenyeki;
Kwa maana ni wengi kuliko nzige, hawahesabiki.
24Binti ya Misri ataaibishwa;
Atatiwa mikononi mwa watu wa kaskazini.
25BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitamwadhibu Amoni wa No, na Farao, na Misri, pamoja na miungu yake, na wafalme wake, naam, Farao, na hao wanaomtumainia;[#Eze 30:13]
26nami nitawatia katika mikono ya hao wanaowatafuta roho zao, na katika mikono ya Nebukadneza, mfalme wa Babeli, na katika mikono ya watumishi wake; na baada ya hayo itakaliwa na watu, kama katika siku za kale, asema BWANA.[#Yer 44:30; 48:47; 49:39]
27Lakini usiogope wewe, Ee Yakobo, mtumishi wangu; wala usifadhaike, Ee Israeli; kwa maana, tazama, nitakuokoa toka mbali, na wazao wako toka nchi ya uhamisho wao; na Yakobo atarudi, naye atatulia na kustarehe, wala hapana mtu atakayemtia hofu.[#Yer 30:10-11; Isa 44:2]
28Usiogope wewe, Ee Yakobo, mtumishi wangu, asema BWANA; kwa maana mimi ni pamoja nawe; maana nitawakomesha kabisa mataifa yote huko nilikokufukuza, bali sitakukomesha wewe kabisa; lakini nitakurudi kwa hukumu, wala sitakuacha bila adhabu.