Ayubu 26

Ayubu 26

Ayubu ajibu: Ukuu wa Mungu hauchunguziki

1Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2Jinsi ulivyomsaidia huyo asiye na uwezo![#Mit 25:11]

Jinsi ulivyouokoa mkono usio na nguvu!

3Jinsi ulivyomshauri huyo asiye na hekima![#1 Kor 2:4]

Na kutangaza ujuzi wa kweli kwa wingi!

4Je! Umetamka maneno kwa nani?

Kisha ni roho ya nani iliyotoka kwako?

5Hao waliokufa watetemesha

Chini ya maji na hao wakaamo humo.

6Kaburi li wazi mbele yake,[#Zab 139:8; Mit 15:11; Isa 14:9; Amo 9:2; Ebr 4:13]

Uharibifu nao hauna kifuniko.

7Yeye hutandaza kaskazi juu ya nafasi isiyo na kitu,[#Zab 24:1,2]

Na kuutundika ulimwengu pasipo kitu.

8Huyafunga maji ndani ya mawingu yake mazito;[#Mit 30:4]

Na hilo wingu halipasuki chini yake.

9Husitiri uso wa kiti chake cha enzi,

Na kulitandaza wingu lake juu yake.

10Amepiga duara kuwa ni mpaka juu ya uso wa maji,[#Yer 5:22]

Hata hapo mwanga na giza vinapopakana.

11Nguzo za mbingu zatetemeka,

Na kustaajabu kwa kukemea kwake.

12Huichafua bahari kwa uwezo wake,[#Kut 14:21; Isa 51:15; Zab 29:10; 74:13]

Na kumtema Rahabu kwa akili zake.

13Hizo mbingu hupambwa kwa roho yake;[#Zab 33:6]

Mkono wake umemchoma nyoka aendaye mbio.

14Tazama, hivi ni viunga tu vya njia zake;

Na jinsi yalivyo madogo manong'ono tusikiayo katika habari zake!

Lakini ngurumo za uweza wake ni nani awezaye kuzielewa?

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya