The chat will start when you send the first message.
1Neno la BWANA likamjia Yona mara ya pili, kusema,
2Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru.
3Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake ni mwendo wa siku tatu.
4Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arubaini Ninawi utaangamizwa.[#Kum 18:22; Mt 12:41; Lk 11:32]
5Basi watu wa Ninawi wakamwamini Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, kuanzia yeye aliye mkubwa hadi aliye mdogo.[#Mt 12:41; Lk 11:32]
6Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu.[#Ayu 2:8; Yer 6:26; Omb 3:29; Mik 1:10]
7Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji;[#2 Nya 20:3; Yoe 2:15]
8bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake.[#Isa 1:16; Eze 33:11; Dan 4:27]
9Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe?
10Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.