Hesabu 19

Hesabu 19

Kafara ya ng'ombe jike mwekundu

1BWANA akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

2Hii ndiyo amri ya sheria BWANA aliyoagiza, akisema, Waambie wana wa Israeli wakuletee ng'ombe jike mwekundu asiye na doa, mkamilifu, ambaye hajatiwa nira bado;[#Isa 53:4-6; Gal 4:4; Ebr 9:13,14; Ufu 1:5; Kum 21:3; 1 Sam 6:7; Yn 10:17; Flp 2:6,8]

3nanyi mtamleta kwa Eleazari kuhani, naye atakwenda naye nje ya kambi, na mtu mmoja atamchinja mbele yake;[#Law 4:12,21; 13:46; 16:27; 24:14; Ebr 13:11]

4kisha Eleazari kuhani atatwaa katika damu yake kwa kidole chake, na kuinyunyiza damu yake kuelekea upande wa mbele wa hema ya kukutania mara saba;[#Law 4:6,17; 16:14; Isa 52:15; Eze 36:25; Ebr 9:13,14; 12:24; 1 Pet 1:2]

5kisha mtu mmoja atamchoma moto huyo ng'ombe mbele yake; ngozi yake, na nyama yake, na damu yake, pamoja na mavi yake pia atachoma moto;[#Kut 29:14; Law 4:11,12; Isa 53:10]

6kisha kuhani atatwaa mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, na kuvitupa katika huo moto unaomchoma ng'ombe.[#Law 14:4,6]

7Ndipo kuhani atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, kisha baadaye ataingia kambini, naye kuhani atakuwa najisi hadi jioni.[#Law 11:25; 15:5]

8Na huyo aliyemchoma moto ng'ombe atazifua nguo zake majini, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hadi jioni.[#19:8 Katika Kiebrania ni ‘aliyemchoma’.]

9Kisha mtu mmoja aliye safi atayazoa majivu ya huyo ng'ombe, na kuyaweka yawe akiba katika mahali safi nje ya kambi, nayo yatatunzwa kwa ajili ya mkutano wa wana wa Israeli, kuwa ndiyo maji ya farakano; ni sadaka ya dhambi.[#Ebr 9:13; Hes 31:23; Zek 13:1; 2 Kor 7:1]

10Na yeye ayazoaye majivu ya huyo ng'ombe atazifua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni; na jambo hili litakuwa amri ya milele, kwa wana wa Israeli, na wa mgeni akaaye kati yao.

11Mtu agusaye maiti yeyote atakuwa najisi muda wa siku saba;[#Law 21:1; Hes 5:2; Isa 52:11; Rum 5:12; 2 Kor 6:17; Efe 2:1]

12naye atajitakasa kwa yale maji siku ya tatu, na siku ya saba atakuwa safi; lakini kama hajitakasi siku ya tatu, ndipo na siku ya saba hatakuwa safi.[#Hes 31:19]

13Mtu yeyote yule agusaye maiti ya mtu aliyekufa, asijitakase, analitia unajisi maskani ya BWANA; na mtu huyo atatupiliwa mbali na Israeli; maana, hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake, atakuwa najisi; unajisi wake ungali upo juu yake.[#Law 15:31; Hes 8:7; Law 7:20; 22:3]

14Hii ndiyo amri, mtu afapo ndani ya hema; kila mtu aingiaye ndani ya hema hiyo, na kila mtu aliye humo hemani, atakuwa najisi muda wa siku saba.

15Na kila chombo kilicho wazi, kisichofungwa na kifuniko, ni najisi.[#Hes 31:20; Law 11:32]

16Kisha mtu yeyote huko nje shambani atakayemgusa mtu aliyeuawa kwa upanga, au mzoga, au mfupa wa mtu, au kaburi, atakuwa najisi muda wa siku saba.

17Na kwa huyo aliye najisi watatwaa katika majivu ya kuchomwa kwake hiyo sadaka ya dhambi, na maji ya mtoni yatachanganywa na majivu katika chombo;

18kisha mtu mmoja aliye safi atatwaa hisopo, na kuitia katika hayo maji naye atayanyunyiza juu ya hema, na juu ya vyombo vyote, na juu ya watu waliokuwapo, na juu yake yeye aliyeugusa mfupa, au mtu aliyeuawa, au mzoga, au kaburi;[#Zab 51:7; Yn 15:2; 17:19; 1 Kor 1:30; Ebr 9:14; #19:18 Mmea mdogo ambao kitawi chake au jani lake huutumiwa kunyunyizia watu au vitu maji kuhusiana na utakaso katika ibada.]

19na yule aliye safi atamnyunyizia huyo aliye najisi siku ya tatu, na siku ya saba; na katika siku ya saba atamtakasa; naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa safi jioni.[#Law 14:9]

20Lakini mtu atakayekuwa najisi, naye hataki kujitakasa, mtu huyo atakatiliwa mbali katika mkutano, kwa sababu amepatia unajisi mahali patakatifu pa BWANA; hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake; yeye yuko najisi.[#Mwa 17:14; Mk 16:16; Mdo 13:39-41; Rum 2:4,5; Gal 3:10]

21Nayo itakuwa amri ya siku zote kwao; na yeye anyunyizaye maji ya farakano atazifua nguo zake; naye ayagusaye hayo maji ya farakano atakuwa najisi hadi jioni.

22Na kitu chochote atakachokigusa mtu aliye najisi kitakuwa najisi; na mtu atakayekigusa kitu hicho atakuwa najisi hadi jioni.[#Hag 2:13]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya