Mithali 1

Mithali 1

KITABU CHA KWANZA

1Mithali za Sulemani, mwana wa Daudi, mfalme wa Israeli.[#1 Fal 4:32]

Utangulizi

2Kujua hekima na adabu; kutambua maneno ya ufahamu;

3kufundishwa matendo ya busara, katika haki na hukumu na adili.[#Mit 2:1]

4Kuwapa wajinga werevu, na kijana maarifa na tahadhari;

5mwenye hekima asikie na kuongezewa elimu, na mwenye ufahamu ayafikie mashauri yenye njia.

6Kufahamu mithali na kitendawili, na maneno ya wenye hekima na mafumbo yao.

7Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.[#Ayu 28:28; Zab 111:10; Mit 9:10]

Maonyo juu ya kushirikiana na waovu

8Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako,

Wala usiiache sheria ya mama yako,

9Kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako,

Na mikufu shingoni mwako.

10Mwanangu, wenye dhambi wakikushawishi,[#Mwa 39:7; Amu 16:16-21; Rum 16:18; Efe 5:11]

Wewe usikubali.

11Wakisema, Haya! Njoo pamoja nasi,[#Mit 12:6; Yer 5:26; Mik 7:2]

Na tuvizie ili kumwaga damu;

Tumwotee asiye na hatia, bila sababu;

12Tuwameze hai kama kuzimu,[#Zab 28:1]

Na wazima, kama wao washukao shimoni.

13Tutapata mali yote ya thamani,

Tutazijaza nyumba zetu mateka.

14Wewe utashirikiana nasi;

Tutakuwa na vitu vyote kwa shirika.

15Mwanangu, usiende njiani pamoja nao;[#Mit 4:14]

Uzuie mguu wako usiende katika mapito yao.

16Maana miguu yao huenda mbio maovuni,[#Isa 59:7]

Nao hufanya haraka ili kumwaga damu.

17Kwa kuwa mtego hutegwa bure,

Mbele ya macho ya ndege yeyote.

18Na hao hujiotea damu yao wenyewe,

Hujinyemelea nafsi zao wenyewe.

19Ndivyo zilivyo njia za kila mwenye tamaa ya mali;[#2 Fal 5:20-27; Mik 2:1-3; 1 Tim 6:10]

Huuondoa uhai wao walio nayo.

Wito wa hekima

20Hekima hulia kwa sauti katika njia kuu,[#Mit 8:1-3]

Hupaza sauti yake katika viwanja;

21Hulia penye mikutano mikubwa ya watu,

Mahali pa kuyaingilia malango,

Ndani ya mji hutamka maneno yake.

22Enyi wajinga, hata lini mtapenda ujinga?

Na wenye dharau kupenda dharau yao,

Na wapumbavu kuchukia maarifa?

23Geukeni kwa ajili ya maonyo yangu;[#Yoe 2:28; Yn 7:37]

Tazama, nitawamwagia roho yangu,

Na kuwajulisheni maneno yangu.

24Kwa kuwa nimeita, nanyi mkakataa;[#Isa 66:4; Yer 7:13; Zek 7:11]

Nimeunyosha mkono wangu, wala hakuna aliyeangalia;

25Bali mmeupuuza ushauri wangu,[#Lk 7:30]

Wala hamkutaka maonyo yangu;

26Mimi nami nitacheka siku ya msiba wenu,

Nitadhihaki hofu yenu ifikapo;

27Hofu yenu ifikapo kama tufani,

Na msiba wenu ufikapo kama kisulisuli,

Dhiki na taabu zitakapowafikia.

28Ndipo watakaponiita, lakini sitaitika;[#Isa 1:15; Yer 14:12; Mik 3:4; Yak 4:3]

Watanitafuta kwa bidii, wasinione.

29Kwa kuwa walichukia maarifa,[#Ayu 21:14; Zab 50:16,17; Isa 27:11; Yn 3:20; Mdo 7:51]

Wala hawakuchagua kumcha BWANA.

30Hawakukubali mashauri yangu,

Wakayadharau maonyo yangu yote.

31Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao,[#Isa 3:11]

Watashiba mashauri yao wenyewe.

32Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua,

Na kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza.

33Bali kila anisikilizaye atakaa salama,

Naye atatulia bila kuogopa mabaya.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya