Mithali 12

Mithali 12

1Kila apendaye mafundisho hupenda maarifa;

Bali yeye achukiaye kulaumiwa ni kama mnyama.

2Mtu mwema atapata upendeleo kwa BWANA;

Bali mtu wa hila atahukumiwa naye.

3Mtu hatathibitika kwa njia ya uovu;

Shina la mwenye haki halitaondolewa kamwe.

4Mwanamke mwema ni taji la mumewe;[#Mit 31:23; 1 Kor 11:7; Mit 14:30]

Bali aaibishaye ni kama kuoza mifupani mwake.

5Mawazo ya mwenye haki ni adili;

Bali mashauri ya mtu mwovu ni hadaa.

6Maneno ya waovu huotea damu;

Bali kinywa cha wanyofu kitawaokoa.

7Waovu huangamia, hata hawako tena;[#Mt 7:24]

Bali nyumba ya mwenye haki itasimama.

8Mtu atasifiwa kwa kadiri ya akili zake;[#1 Sam 13:13; Mal 2:8,9; Mit 1:25,26; 3:35; Mt 27:4,5]

Bali mwenye moyo wa ukaidi atadharauliwa.

9Afadhali mtu anayedharauliwa, ikiwa ana mtumwa,

Kuliko ajisifuye, ikiwa anahitaji chakula.

10Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake;[#Kum 25:4]

Bali huruma za mtu mwovu ni ukatili.

11Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele;[#Mwa 3:19; Mit 28:19; Efe 4:28; 1 The 4:11]

Bali afuataye mambo ya upuzi hana ufahamu.

12Asiye haki hutamani nyavu za wabaya;[#Zab 1:3; Lk 8:15]

Bali shina lao wenye haki huleta matunda.

13Katika kosa la midomo kuna mtego kwa mbaya;[#2 Pet 2:9]

Bali mwenye haki atatoka katika taabu.

14Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake;[#Isa 3:10]

Na atarudishiwa matendo ya mikono yake.

15Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe;[#Lk 18:11]

Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.

16Ghadhabu ya mpumbavu hujulikana mara;

Bali mtu mwerevu husitiri aibu.

17Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki;

Bali shahidi wa uongo hutamka hila.

18Kuna anenaye bila kufikiri, kama kuchoma kwa upanga;

Bali ulimi wa mwenye haki ni afya.

19Mdomo wa kweli utathibitishwa milele;[#Zek 1:5,6]

Bali ulimi wa uongo ni wa kitambo tu.

20Hila imo mioyoni mwao wafikirio uovu;

Bali wafanyao mashauri ya amani, kwao kuna furaha.

21Mwenye haki hatapatikana na msiba wowote;[#Rum 8:28; 2 The 1:6; 2 Pet 2:9]

Bali wasio haki watajazwa mabaya.

22Midomo ya uongo ni chukizo kwa BWANA;[#Ufu 22:15]

Bali watendao uaminifu ndio furaha yake.

23Mwanadamu mwenye busara husitiri maarifa;

Bali moyo wa wapumbavu hutangaza upumbavu.

24Mkono wa mwenye bidii utatawala;[#1 Fal 11:28; Mit 10:4]

Bali mvivu atalipishwa kodi.

25Uzito katika moyo wa mtu huuinamisha;[#Isa 50:4]

Bali neno jema huufurahisha.

26Mwenye haki ni kiongozi wa mwenzake;

Bali njia ya wasio haki huwakosesha.

27Mtu mvivu hapiki mawindo yake;

Bali mwenye bidii anazo mali za thamani.

28Katika njia ya haki kuna uhai;[#Kum 30:15; Mt 19:17; Rum 5:21; 2 Kor 4:17; Ufu 2:7]

Wala hakuna mauti katika mapito yake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya