The chat will start when you send the first message.
1Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye;[#1 Sam 2:25; Mit 9:7,8]
Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.
2Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake;
Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri.
3Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake;[#Zab 39:1]
Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu.
4Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu;
Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa.
5Mwenye haki huchukia kusema uongo;[#Kol 3:9; Rum 12:9]
Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu.
6Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake;[#Mit 11:3]
Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi.
7Kuna mtu anayejitajirisha, lakini hana kitu;
Kuna anayejifanya kuwa maskini, lakini ana mali nyingi.
8Fidia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake;
Bali mtu maskini hasikii ogofyo lolote.
9Nuru ya mwenye haki yang'aa sana;
Bali taa ya mtu mbaya itazimika.
10Kiburi huleta mashindano tu;
Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.
11Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka;[#Mit 20:21]
Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.
12Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua.
Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.
13Kila anayelidharau neno hujiletea uharibifu;[#2 Nya 36:16]
Bali yeye anayeiogopa amri atapewa thawabu.
14Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima,[#Mit 16:22; 15:24; 2 Sam 22:6; Zab 116:3]
Ili kuepukana na tanzi za mauti.
15Ufahamu mwema huleta upendeleo;
Bali njia ya muasi huangamiza.
16Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa;[#Mit 12:23]
Bali mpumbavu hueneza upumbavu.
17Mjumbe mbaya huanguka maovuni;
Bali mjumbe mwaminifu ni afya.
18Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa;[#Mit 15:5]
Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa.
19Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu;
Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu.
20Nenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima;
Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.
21Uovu huwafuatia wenye dhambi;[#Zab 32:10]
Bali mwenye haki atalipwa mema.
22Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi;[#Mhu 2:26]
Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki.
23Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini;[#Mit 12:11]
Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma.
24Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe;[#Mit 19:18; 22:15]
Bali yeye ampendaye humrudi mapema.
25Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake;
Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa.