The chat will start when you send the first message.
1Utakapoketi kwa chakula pamoja na mtawala,
Mwangalie sana yeye aliye mbele yako.
2Tena ujitie kisu kooni,
Kama ukiwa mlafi.
3Usivitamani vyakula vyake vya anasa;
Kwa maana ni vyakula vya hila.
4Usijitaabishe ili kupata utajiri;[#Mit 28:20; 3:5; Yn 6:27; 1 Tim 6:9; Rum 12:16]
Acha kuzitegemea akili zako mwenyewe.
5Je! Utavikazia macho vile ambavyo si kitu?
Maana bila shaka mali hujifanyia mabawa,
Kama tai arukaye mbinguni.
6Usile mkate wa mtu mwenye husuda;[#Zab 141:4; Kum 15:9; Mt 20:15; Mk 7:22]
Wala usivitamani vyakula vyake vya anasa;
7Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.
Akuambia, Haya, kula, kunywa;
Lakini moyo wake hauwi pamoja nawe.
8Tonge lile ulilokula utalitapika,
Na maneno yako matamu yatakupotea.
9Usiseme masikioni mwa mpumbavu;[#Mt 7:6]
Maana atadharau hekima ya maneno yako.
10Usiiondoe alama ya mpaka wa zamani;
Wala usiingie katika mashamba ya yatima;
11Kwa sababu mkombozi wao ana nguvu;[#Ayu 31:21; Yer 50:34]
Atawatetea juu yako.
12Elekeza moyo wako kusikiliza mafundisho;
Tega masikio yako kusikia maneno ya maarifa.
13Usimnyime mtoto wako mapigo;
Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa.
14Utampiga kwa fimbo,[#1 Kor 5:5]
Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu.
15Mwanangu, kama moyo wako una hekima,
Moyo wangu utafurahi, naam, moyo wangu;
16Naam, viuno vyangu vitafurahi,
Midomo yako inenapo maneno mema.
17Moyo wako usiwahusudu wenye dhambi;
Bali mche BWANA mchana kutwa;
18Maana bila shaka iko thawabu;[#Lk 16:25]
Na tumaini lako halitabatilika.
19Sikia, mwanangu, uwe na hekima,
Na kuuongoza moyo wako katika njia njema.
20Usiwe miongoni mwao wanywao mvinyo;[#Isa 5:22; Mt 24:49; Lk 21:34; Rum 13:13; Efe 5:18]
Miongoni mwao walao nyama kwa pupa.
21Kwa maana mlevi na mlafi huingia umaskini,
Na utepetevu humvika mtu nguo mbovu.
22Msikilize baba yako aliyekuzaa,[#Efe 6:1]
Wala usimdharau mama yako akiwa mzee.
23Inunue kweli, wala usiiuze;[#Mt 13:44]
Naam, hekima, na mafundisho, na ufahamu.
24Baba yake mwenye haki atashangilia;
Naye amzaaye mtoto mwenye hekima atamfurahia.
25Na wafurahi baba yako na mama yako;
Na afurahi aliyekuzaa.
26Mwanangu, nipe moyo wako;
Macho yako yapendezwe na njia zangu.
27Kwa maana kahaba ni shimo refu;
Na malaya ni mtego wa shimo jembamba.
28Naam, huotea kama mnyang'anyi;
Huwaongeza wenye hila katika wanadamu.
29Ni nani apigaye, Yowe? Ni nani aliaye, Ole?[#1 Fal 20:16; Mit 20:1; Isa 5:11; Nah 1:10; Mt 24:49,50; Efe 5:18]
Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye mguno?
Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu?
Ni nani aliye na macho mekundu?
30Ni wale wakaao sana kwenye mvinyo;
Waendao kutafuta divai iliyochanganyika.
31Usiutazame mvinyo iwapo ni mwekundu;
uitiapo bilauri rangi yake, ushukapo taratibu;
32Mwisho wake huuma kama nyoka;
Huchoma kama fira.
33Macho yako yataona mambo mageni;
Na moyo wako utatoa yaliyopotoka.
34Naam, utakuwa kama alalaye katikati ya bahari;
Au kama yeye asinziaye juu ya mlingoti.
35Utasema, Wamenichapa wala sikuumia;[#Mit 27:22; Yer 5:3; Kum 29:19; Isa 56:12; 2 Pet 2:22]
Wamenipiga wala sina habari;
Nitaamka lini, nitazidi kuitafuta tena.