Yoshua Mwana wa Sira 14

Yoshua Mwana wa Sira 14

Heri ya kweli

1Yu heri asiyejikwaa kwa kinywa chake,

Wala hakuchomwa na kusikitika kwa dhambi.

2Yu heri asiyehesabiwa hatia rohoni mwake,

Wala hakutindikiwa na tumaini lake.

Wajibu wa Kutumia Mali

3Mali hazimpasi bahili; mnyimivu atafanyaje na fedha?

4Achumaye kwa kujinyima roho yake awachumia wengine, na wengine watajifurahisha kwa mapato yake.

5Aliye mbaya wa nafsi yake atakuwa mwema kwa nani? Aidha, hatapata furaha katika vitu vilivyo vyake.

6Hakuna mbaya zaidi kuliko yeye anayejihusudu mwenyewe; na hii ndiyo thawabu ya ubaya wake.

7Hata akitoa fadhili hutoa kwa sababu ya usahaulifu; na mwishowe hufunua wazi ubaya wake.

8Ni mwovu aliye mwenye kijicho, akigeuzia mbali uso wake, na kuzidharau roho za watu.

9Mwenye choyo jicho lake haliridhiki na sehemu yake; na udhalimu ulio mbaya hukausha roho yake.

10Mwenye jicho ovu huwa mnyimivu wa chakula, na mwenye ubahili hata mezani pake.

11Mwanangu, kadiri ulivyo navyo, ujifanyizie mema, na kumletea BWANA sadaka kama ipasavyo.

12Kumbuka ya kwamba mauti haikawii, wala hukufunuliwa agizo la kaburi.

13Na umfanyizie mema rafiki yako asijekufa; na kadiri uwezavyo nyosha mkono wako ukampe.

14Usijinyime siku ya furaha, wala fungu la matakwa mema lisikupite.

15Je! Hutamwachia mwingine kazi zako? Na mapato yako ili yagawanyike kwa kura?

16Toa na kupokea, na ujiburudishe roho yako, kwa maana hakuna kutafuta anasa kaburini.

17Wote huchakaa kama vazi; agizo la tangu awali ni hili, Kufa utakufa.

18Katika majani yasitawiyo juu ya mti mkubwa, hupukutisha mengine, na mengine huyaotesha; vivyo hivyo katika vizazi vya mwili na damu, kimoja hukoma, kimoja huzaliwa.

19Hakika ya kila tendo huchakaa, na kuanguka; na mtendaji atawenda zake vivyo hivyo.

Furaha ya Kutafuta Hekima

20Yu heri mtu yule atakayetafakari hekima, na kuangalia ufahamu,[#Mit 8:32-35]

21na kukaza moyo wake katika njia zake, na kupata maarifa katika siri zake.

22Toka ukaende kumtafuta kama mwenye kuaua, na kumwotea katika mapito yake.

23Anayepeleleza dirishani pake atasikiliza mlangoni pake;

24anayetua karibu na nyumba yake atapiga kigingi ukutani mwake;

25ataisimika hema yake karibu naye, na kufanya kituo panapo mema.

26Atajenga kiota chake katika tanzu zake, na kupumzika chini ya matawi yake;

27kwake atapata kivuli katika joto, na kufanya kikao katika utukufu wake.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya