Yoshua Mwana wa Sira 15

Yoshua Mwana wa Sira 15

1Kwa maana amchaye BWANA atayafanya hayo, naye aishikaye torati atapata hekima.

2Naye Hekima atakutana naye kama mama, na mfano wa mke aliye mwanamwali.

3Atamlisha mkate wa ufahamu, atamnywesha maji ya utambuzi.

4Huyo naye atathibitishwa juu yake asitikisike, na kumtegemea asifadhaike.

5Naye Hekima atamtukuza kupita jirani zake, na kumfumbulia kinywa chake katikati ya kusanyiko.

6Huyo ataona furaha na shangwe, na kurithishwa jina la milele.

7Bali wapumbavu hawatampata, wala wakosaji hawatamwona;

8yu mbali na watu wa dhihaka, wala wasemao uongo hawamkumbuki.

9Kinywani mwa mwenye dhambi himidi hazifai, madhali hakupewa na BWANA.

10Kinywani mwa mwenye hekima himidi hutolewa, naye mtu aliyehitimu hekima atajifunza kuhimidi.

Uhuru wa Kuchagua

11Usiseme, Ni juu ya BWANA nilivyoasi;[#Sira 17:1-12]

Maana usitende yanayomchukiza.

12Usiseme, Ndiye aliyenikosesha;

Maana hana haja ya mkosaji.

13BWANA hukirihi kila linalochukiza;

Wala wamchao hawalipendi hilo.

14Hapo mwanzo Mungu alimuumba mwanadamu,

Akamwacha aifuate nia yake.

15Ukipenda, utazishika amri zake,

Na kutenda amini ni shauri lako.

16Ameweka mbele yako moto na maji;

utanyosha mkono wako uchaguavyo.

17Mbele ya mwanadamu upo uzima na mauti,

Naye atapewa apendavyo.

18Mradi hekima ya BWANA yatosha,

Mkuu mwenye uweza hutazama vyote,

19Macho yake ni juu yao wamchao,

Naye atapeleleza kila kazi ya watu.

20Hakumwamuru mtu yeyote awe asi,

Wala humruhusu atende dhambi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya