The chat will start when you send the first message.
1Yeye anayeishi milele ameviumba vitu vyote pia.
2BWANA peke yake atahesabiwa
3kuwa ni haki,
4Hakumjalia mtu yeyote kuzieleza kazi zake; naye ni nani awezaye kuyakagua matendo yake makuu?
5Nani atakayeuhubiri uweza wa adhama yake? Naye ni nani atakayeitangaza jumla ya rehema zake?
6Haiwezekani kuyapunguza wala kuyaongeza, wala kuyachunguza mambo ya ajabu ya BWANA.
7Hata mtu atakapokwisha, huwa ndio mwanzo tu; naye pale atakapokoma ndipo atakapoingiwa na shaka.
8Mwanadamu ni kitu gani, anafaa wapi?
Jema lake lipi, na baya lake lipi?
9Jumla ya siku zake haizidi miaka mia;
10Kama tone la maji litokalo baharini,
Mfano wa mbwe iliyookotwa ufuoni,
Ndiyo miaka haba katika umilele.
11Kwa sababu hiyo BWANA alikuwa mvumilivu kwao, akawakirimia wingi wa rehema zake.
12Aliona akaufuahamu mwisho wao, ya kuwa ni mbaya; kwa hiyo akawaongezea masamaha yake.
13Rehema ya mwanadamu huwa juu ya jirani yake, bali rehema za BWANA zi juu ya wote wenye mwili. Huwakemea na kuwaelemisha na kuwafundisha, huwarudisha mfano wa mchungaji na kondoo zake.
14Huwarehemu wale wakubalio kuelimishwa, wazitafutao hukumu zake kwa bidii.
15Katika fadhili zako usitie hitilafu,
Wala kijicho katika upaji wako.
16Umande hupunguza joto ya kaskazi,
Nalo neno huwa zuri kuliko zawadi,
17Neno la hisani laongeza zawadi,
Na yote mawili yana mtu wa fadhili.
18Mpumbavu atashutumu bila ustahivu,
Na kipawa cha bahili hushusha macho.
19Mwanangu, ujifunze elimu kabla ya kunena, ujitunze afya yako kabla ya kuugua.
20Kabla hujahukumiwa ujihakikishe roho yako, nawe utaona masamaha wakati wa kujiliwa.
21Ujinyenyekeshe kabla ya kuugua, na endapo umetenda dhambi onesha toba.
22Neno lolote lisikuzuie hata usiiondoe nadhiri yako kwa majira yake, wala usingoje wewe mpaka kufa kuhesabiwa kuwa una haki.
23Kabla ya kuweka nadhiri ujiweke tayari, wala usiwe kama mtu amjaribuye Mungu.
24Uitafakari ghadhabu ya siku za mwisho, na wakati wa kisasi atakapogeuzia mbali uso wake.
25Wakati wa shibe kumbuka wakati wa njaa, na siku za utajiri fikiri umaskini na uhitaji.
26Tangu asubuhi hata jioni na wakati umebadilika, na mambo yote yanakwenda kasi mbele za BWANA.
27Mwenye hekima hutanadhari katika yote, na panapo nafasi ya kutenda dhambi atajihadhari na matatizo.
28Kila mtu wa ufahamu hutambua hekima, naye atamshukuru yeye aliyeivumbua.
29Pia wale waliokuwa welekevu wa maneno walionekana wenyewe kuwa wataalamu, wakakupua mithali za kufaa.
30Usizifuate tamaa za roho yako,
Bali ujizuilie uchu wake.
31Endapo utaipa roho yako ruhusa ya kuziridhisha tamaa zake kwa wingi, itakufanya mzaha kwa adui zako.
32Usichangamke katika wingi wa anasa,
Usije ukapata umaskini maradufu.
33Usifilisike kwa kula karamu za makope, maadamu huna kitu cha mali mfukoni mwako.