Yoshua Mwana wa Sira 21

Yoshua Mwana wa Sira 21

Dhambi Mbalimbali

1Mwanangu, umetenda dhambi? Usizidi;

Tena omba dua kwa dhambi za kale.

2Uikimbie dhambi kama mbele ya uso wa nyoka; mradi itakuuma ukikaribia; meno yake ni kama meno ya simba; inazifisha roho za watu.

3Udhalimu wote ni upanga ukatao kuwili;

Ukipigwa nao hakuna kupona.

4Tisho na ukatili huangamiza makao;

Hivyo nyumba ya mwenye kiburi itafanywa gofu.

5Mungu husikia dua ya maskini,[#Sira 35:17-19]

Tena hukumu yake haikawii kufika.

6Mchukia kemeo yupo njiani pa mkosaji;

Bali amchaye BWANA atageuka moyoni.

7Mtaalamu humtambua aliye mbele yake,

Na kumchunguza mwenye dhambi mara.

8Aijengaye nyumba kwa mali za watu,

Ni kama akusanyaye mawe kwa kaburi.

9Makusanyiko ya wadhalimu ni kama kitani iliyofungamana; na mwisho wake ni moto wa miali.

10Njia ya wenye dhambi imelainika haina mawe; na mwisho wake ni shimo la Jehanamu!

Hekima na Upumbavu

11Mwenye kuishika torati hupata kutawala tamaa;

Na mwisho wa kumcha BWANA ndio hekima.

12Asiye mwerevu hatapata kuelimishwa;

Bali upo werevu uongezao uchungu tele.

13Maarifa ya mwenye hekima yatajaa kama kisima;

Na shauri lake kama chemchemi ya uzima.

14Mtima wa mpumbavu ni chombo kilichovunjika:

Hataweza kuchukua maarifa maisha yake.

15Mtu wa maarifa akisikia neno la hekima,

Atalitukuza, pia na kuliongeza.

Mtu mpotovu hulisikia na kudhihaki,

Na kulitupa nyuma ya mgongo wake.

16Mazungumzo ya mpumbavu ni mzigo njiani;

Bali neema imo midomoni mwa wataalamu.

17Kinywa cha mwekevu kitatafutwa kwenye mkutano;

Nao watatafakari maneno yake mioyoni mwao.

18Hekima kwa mpumbavu hufanana na magofu;

Na maarifa ya mjinga ni maneno pasipo maana.

19Mafundisho ni pingu miguuni pa mjinga,

Naam, pingu katika mkono wake wa kuume.

20Mpumbavu hupaaza sauti yake katika kucheka;

Bali mwerevu aona shida hata ya kuchekelea.

21Mafundisho ni pambo la dhahabu kwa mwelekevu,

Naam, vikuku katika mkono wake wa kuume.

22Mguu wa mjinga mno upesi nyumbani mwa mtu;

Bali mwelekevu atasita katika kuingia.

23Mpumbavu atachungulia mlangoni pa nyumba;

Bali mwenye adabu husimama nje.

24Ni kukosa adabu ya mtu kusikiliza mlangoni; lakini mtu wa busara angeona haya kutenda hivi.

25Midomo ya wenye kiburi ni mizito ya kulaani; bali maneno ya wenye busara yapimwa katika mizani.

26Moyo wa mpumbavu u kinywani mwake; bali kinywa cha mwenye hekima ni moyo wake.

27Mwovu anapomlaani yule mwovu

Huilaani roho yake mwenyewe.

28Msingiziaji huinajisi roho yake.

Atachukiwa popote akaapo.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya