The chat will start when you send the first message.
1Ampendaye mwanawe atafuliza kumpiga, apate kumfurahia hatimaye.
2Amrudiye mwanawe atapata faida kwake, na kuona fahari juu yake mbele ya rafiki zake.
3Amfundishaye mwanawe atamtia wivu adui yake, na mbele ya rafiki zake atamshangilia.
4Babaye yuafa, ila imekuwa kana kwamba hakufa; kwa maana ameacha nyuma yake mtu aliye kama yeye;
5katika maisha yake alimwona na kumfurahia, pia hapo alipofariki hakusikitika;
6aliacha nyuma yake mtu wa kuwalipiza kisasi adui zake, tena mtu wa kuwalipa rafiki zake hisani yao.
7Mwenye kumtundua mwanawe na afunge jeraha zake, hata na moyo wake atafadhaika kwa kila kilio.
8Farasi asiyefugwa huwa mkaidi; na mwana aliyeachwa huwa mkorofi.
9Ukimkinaisha mtoto wako atakutia fadhaa, ukicheza naye atakuhuzunisha.
10Usicheke pamoja naye usije ukapata huzuni kwake; hatimaye utasaga meno yako.
11Usimpe mamlaka yoyote wakati wa ujana wake, wala usiyaachilie mapumbavu yake.
12Uinamishe shingo yake maadamu yu kijana, umpige mbavuni wakati wa utoto wake; ili asije akawa mkaidi akakuasi, ikawemo huzuni moyoni mwako.
13Basi, umrudi mwanao na kujitahidi kwa ajili yake, ushupavu wake usije ukakuchukiza.
14Yu heri maskini aliye mzima mwenye siha njema, kuliko yeye aliye tajiri naye anasumbuka mwilini mwake.
15Afya na siha njema ni nzuri kuliko dhahabu safi, na roho iliyo hodari hupita mali isiyopimika.
16Hakuna utajiri kupita afya ya mwili, wala hakuna mali kupita changamko ya moyo.
17Kufa kwafaa zaidi kuliko kuishi bure, na raha ya milele kuliko maumivu ya daima.
18Mambo mema mbele ya kinywa kilichofumbwa ni kama vyakula vilivyowekwa juu ya kaburi.
19Sadaka huifaidia sanamu namna gani? Ambayo haili wala hainusi;
20ndivyo alivyo mtu mwenye mali asiyeweza kuzifurahia.
21Usijizamishe roho yako katika huzuni, wala kujikwaza katika shauri lako.[#Mhu 11:9-10]
22Changamko la moyo ndiyo uzima wa mtu, na shangwe huzidisha siku zake.
23Ujifurahishe roho yako na kuuburudisha moyo wako; uiondoe huzuni mbali nawe; kwa kuwa huzuni imewaangamiza wengi, wala ndani yake hamna faida.
24Wivu na hasira pia hupunguza maisha, na kujisumbua kwaleta uzee kabla ya wakati wake.
25Bali mtu mwenye moyo mkarimu hufurahi, na chakula chake chamfaa.