Yoshua Mwana wa Sira 32

Yoshua Mwana wa Sira 32

Adabu Karamuni

1Je! Umechaguliwa mkuu wa meza? Usiinuke; uwe miongoni mwao kama mmoja wao; uwaangalie na kuwaketisha vizuri.

2Ukiisha kufanya kazi yako ukipokee kiti chako; uifurahie heshima yao na kuvishwa shada kwa uangalifu wako.

3Wewe uliye mzee, useme, maana yakupasa; lakini kwa maarifa yenye njia, wala usizuie kuimba.

4Usikupue maneno panapo mchezo wa kuimba; wala kutembeza hekima yako wakati usiofaa.

5Kama mhuri wa yakuti katika kijalizo cha dhahabu,

Ndivyo ilivyo tarabu penye karamu ya mvinyo;

6Kama mhuri wa zumaridi katika kazi ya dhahabu,

Ndivyo ilivyo tafrija pamoja na divai tamu.

7Wewe uliye kijana, useme, ikiwa unatakiwa; lakini kwa shida ukiulizwa mara mbili.

8Katiza maneno, mengi kwa machache, uwe kama ajuaye lakini akaa kimya;

9miongoni mwa wakuu usijifanye sawa nao, na mwingine asemapo usidukize maneno yako.

10Kutangulia ngurumo umeme hupita kasi, na mbele ya mwenye haya kibali hutokea.

11Basi uondoke mapema, usiwe wa mwisho, uende nyumbani kwako usikawie;

12ndipo utakapo starehe na kufanya mapenzi yako, lakini usifanye dhambi ya kujivuna.

13Kwa hayo yote umhimidi Yeye aliyekuumba, na kukumwagia mema yake.

Ulinzi wa Mungu

14Amchaye BWANA atakubali mapigo yake,

Nao wamtafutao mapema watapata kibali.

15Mtaali torati atashiba torati,

Bali mnafiki atajikwaa humo.

16Wamchao BWANA wataelewa na hukumu,

Na kuangaza matendo mema kama nuru.

17Mwenye jeuri hukataa kukemewa,

Ajivutia torati kama atakavyo.

18Mwenye shauri hatadharau dokezo;

Bali mwenye kiburi hapokei mafundisho.

19Pasipo shauri usifanye neno;

Kisha kulifanya usije ukajuta.

20Katika njia iliyoparuza usiende,

Wala kujikwaa katika jiwe mara mbili;

21Hata katika njia laini uangalie,

22Na kujihadhari mapito yako.

23Katika kila kazi uiamini roho yako,

Atendaye hayo huishika amri;

24Aishikaye torati huihifadhi roho yake,

Wala amwaminiye BWANA hapati hasara.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya