Yoshua Mwana wa Sira 6

Yoshua Mwana wa Sira 6

1Yaani, sifa mbaya itarithi aibu na lawama, kwa mfano wa mkosefu aliye mnafiki.

2Tena usione fahari juu ya nguvu za tamaa yake, isije ikaharibu nguvu zako kama fahali.

3Maadamu inakula majani yako, na kuyaharibu matunda yako, na kukuacha wewe mwenyewe mti mkavu.

4Roho ya ufisadi itamharibu yeye aliye nayo, hata kumfanya mzaha kwa adui zake.

Urafiki, Uongo na Kweli

5Maneno matamu yatamzidishia mtu rafiki, na midomo yenye neema itamwongezea wamsalimuo.

6Wale wenye amani nawe na wawe wengi; bali washauri wako mmoja katika elfu.

7Ukitaka kujipatia rafiki, umpate kwa kumjaribu, wala usiwe na haraka katika kumwamini;

8yaani, kuna rafiki wakati wa kufaa, ambaye yeye hatadumu wakati wa msiba wako.

9Tena kuna rafiki ageukaye kuwa adui, naye atakukashifia fitina iletayo lawama.

10Pia kuna rafiki tena, ambaye anakula mezani pako, bali siku ya mabaya haonekani;

11wakati wa kufanikiwa kwako atakuwa sawa nawe, na kupiga domo juu ya watumishi wako;

12lakini ukipatwa na masaibu atakugeuka, na kujificha mbali nawe na uso wako.

13Basi ujitenge na adui zako; tena ujihadhari na rafiki zako.

14Walakini rafiki aliye amini ndiye ngome; naye aliyempata amepata tunu.

15Hakuna badala ya rafiki amini, wala uzuri wake hauna bei.

16Rafiki amini ni kufunga uzima; naye amchaye Mungu atampata.

17Mcha Mungu hunyosha urafiki wake, kwa maana alivyo yeye mwenyewe ndivyo alivyo na jirani yake.

Baraka za Hekima

18Mwanangu, uchume maarifa tangu ujana hata kuwa mwenye mvi, nawe utapata hekima.

19Uijilie kama alimaye na kupanda, uyasubiri matunda yake mazuri; maana kazi yako ya ulimaji itakuwa haba nawe utakula matunda yake mara.[#Yak 5:7-8]

20Ni ajabu ilivyoparuza njia yake kwake asiyefundishwa, wala asiye na ufahamu hatakaa ndani yake;

21kama jiwe zito lemevu itakuwa juu yake, wala hatakawia kuitupa.

22Yaani, hekima ni sawasawa na jina lake, wala haikufunuliwa kwa watu wengi.

23Mwanangu, tega sikio uikubali hukumu yangu, wala usilikatae shauri langu.

24Uitie miguu yako katika pingu zake, pia na shingo yako katika minyororo yake;

25weka bega lako chini uichukue nira yake; wala usione uchungu kwa vifungo vyake.

26Uijilie kwa roho yako yote, uzishike njia zake kwa nguvu zako zote.

27Kutafuta uitafute nayo itadhihirika kwako; wala usiiache ukiisha kuipata.

28Kwa maana mwishowe utaiona raha yake, nayo itakugeukia changamko;

29pingu zake zitakuwia kifuniko cha nguvu, na minyororo yake vazi la utukufu.

30Kwa maana nira yake ni pambo la dhahabu, na vifungo vyake ni nyuzi za samawi;

31utaivaa kama vazi la utukufu, na kama taji la uzuri utajivika nayo.

32Mwanangu, ukitaka utafahamishwa; ukitia moyo wako utakuwa mwerevu;

33ukipenda kusikia utapokea ukitega sikio lako utapata kuwa na hekima.

34Usimame, basi, katika mkutano wa wakuu na yeyote aliye na hekima uambatane naye.

35Uwe tayari kusikiliza kila hotuba ya utauwa, wala usipitiwe na mithali za ufahamu.

36Umwonapo mtaalamu umwendee mapema, hata kwa miguu yako uyachakaze madaraja ya mlango wake.

37Moyo wako uyafikiri maagizo ya BWANA, uzitafakari daima amri zake; naye atakufundisha moyo wako, na tamaa yako ya hekima utapewa.[#Yos 1:8; Zab 1:2]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya