The chat will start when you send the first message.
1Palikuwa na mtu, jina lake Yoakimu, akikaa Babeli,
2naye ameoa mke jina lake Susana binti Hilkia, mwanamke mzuri sana na mcha Mungu.
3Wazee wake nao walikuwa wenye haki, pia wamemfundisha binti yao sawasawa na Torati ya Musa.
4Basi Yoakimu alikuwa muungwana tajiri, na karibu na nyumba yake alikuwa na bustani nzuri; hivyo Wayahudi humwendea, maana alikuwa mwenye heshima kupita wengineo wote.
5Mwaka ule ule wakaamriwa wawili miongoni mwa wazee wa watu ili kuamua, watu wa namna ile ambao BWANA aliwanena, kama ufisadi ulitoka Babeli kwa wazee waamuzi waliohesabiwa kuwa wanatawala watu.
6Hao walikuwa wakienda mara nyingi kuzuru kwenye nyumba yake Yoakimu; na wote wenye mashtaka yoyote desturi yao wakawajia huko.
7Basi watu walipoondoka kwenda zao panapo saa sita, Susana huingia katika bustani ya mumewe ili kutembea.
8Nao wale wazee wawili humwona kila siku anakwenda kutembea; hata wakawaka tamaa kwa sababu yake.
9Ndipo walipozipotosha nia zao, wakayageuza upande macho yao, wasiweze kutazama mbinguni wala kukumbuka hukumu za haki.
10Na ingawa wote wawili walichomwa kwa kumtamani, lakini hawakuthubutu kujulishana taabu zao;
11mradi waliona haya kuzidhihirisha tamaa zao mbaya, walivyotamani kumpata.
12Lakini siku kwa siku wakachungulia kwa husuda ili wamwone,
13hata mmoja wao akamwambia mwenzake, Twende zetu nyumbani, maana ni saa ya chakula. Nao walipotoka wakaachana,
14walirudi nyuma tena kila mtu, wakafika pale pale; ndipo walipoulizana sababu wakakiri tamaa zao, nao wote wawili walijiwekea wakati watakapoweza kumpata yu peke yake.
15Ikawa, walipongoja wakati wa kufaa, yeye aliingia bustanini kama ilivyokuwa desturi yake pamoja na wajakazi wawili, naye alitaka kuoga kwa sababu kulikuwa na joto.
16Wala hapo hapakuwa na mtu yeyote isipokuwa wale wazee wawili, ambao wamejificha wakimvizia.
17Basi akawaambia wajakazi wake, Nileteeni mafuta na sabuni, mkaifunge milango ya bustani, ili nioge.
18Wakafanya kama vile alivyowaagiza, wakaifunga milango ya bustani, wakatoka wenyewe kwa milango ya nyuma ili kuvileta vile vitu alivyoviagiza; wala hawakuwaona wale wazee, kwa maana wamejificha.
19Mara, wale wajakazi walipokwisha kutoka, wale wazee wawili waliondoka wakamwendea mbio, wakasema,
20Tazama, milango ya bustani imefungwa asiweze kutuona mtu yeyote, nasi tunakupenda sana; haya! Basi, utukubali ulale nasi.
21La! Hutaki; tutakushuhudia ya kuwa hapa palikuwapo kijana pamoja nawe, ndiyo sababu uliwaruhusu wajakazi wako.
22Basi Susana aliugua, akasema, Nimesongwa pande zote; maana nikilitenda hilo ni mauti yangu; nisipolitenda siwezi kuokoka mikononi mwenu.[#Law 20:10; Kum 22:22]
23Ni afadhali nianguke katika mikono yenu na kukataa, kuliko kutenda dhambi machoni pa Mungu.
24Mara Susana akapiga kelele kwa sauti kuu; nao wale wazee wawili wakampigia kelele pia.
25Kisha mmoja wao akakimbia, akaifungua milango ya bustani.
26Hivyo watumishi wa nyumbani waliposikia kelele bustanini, wao waliingia kwa kasi kwa mlango wa nyuma ili waone ni nini iliyompata.
27Lakini wale wazee waliisimulia hadithi yao nao watumishi wakaona aibu kabisa; kwa maana Susana hakuchongelewa habari ya namna hiyo wakati wowote.
28Ikawa, kesho yake, watu walipokusanyika kwa Yoakimu mumewe, wale wazee wawili wakaja nao, wamejaa kusudi lao ovu juu ya Susana la kumfisha;
29wakasema mbele ya watu, Mwiteni Susana binti Hilkia, mkewe Yoakimu aje hapa.
30Basi akaenda kuitwa; naye akaja pamoja na baba yake na mama yake, na watoto wake, na jamaa zake wote.
31Naye huyo Susana alikuwa mwanamke mwenye adabu, mzuri wa uso;
32basi hao watu wabaya waliamuru afunuliwe uso, maana alifunikwa utaji, ili washibe uzuri wake.
33Kwa hiyo rafiki zake na wote waliomtazama wakasikitika.
34Ndipo wale wazee wawili waliposimama katikati ya watu, wakaweka mikono yao juu ya kichwa chake.
35Naye akatoka machozi, akatazama juu mbinguni; kwa maana moyo wake alimtumaini Mungu.
36Wale wazee wakasema, Sisi tulipokuwa tukitembea bustanini peke yetu, huyu aliingia pamoja na wajakazi wawili, wakaifunga milango ya bustani, naye mara akawaruhusu wajakazi.
37Kisha, kukatokea kijana, ambaye amejificha humo, akamwendea akalala naye.
38Lakini sisi, tungaliko pembeni mwa bustani, tuliuona ubaya huo, tukawaendea mbio.
39Hata tukiwa tumewaona pamoja, yule kijana hatukuweza kumkamata; maana alikuwa mwenye nguvu kuliko sisi, akaifungua milango akatoroka.
40Bali huyu tulimkamata, tukauliza yule kijana yu nani,
41asikubali kutuambia. Hayo, basi, tunashuhudia. Basi, waliohudhuria wakawasadiki, wakiwa wazee wa watu na waamuzi; hivyo wakahukumu auawe.
42Mara Susana akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Mungu wa milele, Wewe wajua yaliyositirika, wajua mambo yote yasijekuwako.
43Wewe wajua ya kwamba wananishuhudia uongo, na, tazama, imenipasa kufa; lakini sikufanya kamwe mambo kama hayo, ambayo watu hawa wameyabuni juu yangu kwa ukorofi.
44Naye BWANA akaisikia sauti yake.
45Kwa hiyo, alipochukuliwa huyo kwenda kuuawa, Mungu alimchocheleza roho kijana mmoja, jina lake Danieli;
46naye akapaza sauti akasema, Mimi simo; mimi sina hatia kwa habari ya damu yake mwanamke huyu.
47Mara wote wakamgeukia, wakasema, Maneno hayo uyasemayo, maana yake nini?
48Akasimama katikati, akasema, Enyi wana wa Israeli, mmekuwa wapumbavu, hata kumhukumu binti Israeli bila kuhoji wala kupata hakika ya kweli?
49Rudini hukumuni; mradi hao wanamshuhudia uongo.
50Basi watu wote walirejea kwa haraka, nao wale wazee wakamwambia, Njoo uketi kati yetu, utujulishe habari hiyo, endapo Mungu amekupa wewe heshima ya mzee.
51Hapo Danieli aliwaambia, Watu hawa wawili watengwe, nami nitawahoji.
52Basi wakiisha kutengwa, akamwita mmoja wao akamwambia, Ewe uliyepata kuwa mzee katika uovu, sasa dhambi zako zimekukalia, ulizozitenda zamani
53kwa kuhukumu isivyo haki, kumpatiliza asiye na hatia na kumwachilia mwovu; lakini BWANA asema, asiye na hatia, mwenye haki, usimwue.[#Kut 23:7]
54Haya! Basi, wewe ulimwona kwa macho; useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya msandarusi.
55Danieli akasema, Hakika umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana sasa hivi malaika wa Mungu amepokea hukumu ya Mungu, akukate vipande viwili.
56Akamtenga huyo tena, akaamuru kumleta yule mwingine, akamwambia, Ewe mzao wa Kanaani, wala si wa Yuda, uzuri umekudanganya, na tamaa imeupotosha moyo wako.
57Hivyo ndivyo ulivyowafanyia binti za Israeli, na kwa hofu walitembea nawe; bali huyu binti Yuda hakuweza kuustahimili uovu wako.
58Haya! Basi, nawe useme; Chini ya mti gani ulipowaona wakikaa pamoja? Naye akajibu, Chini ya mkwaju.
59Danieli akamwambia, Hakika wewe nawe umesema uongo juu ya kichwa chako mwenyewe; maana malaika wa Mungu yu tayari, anakungoja mwenye upanga, akukate vipande viwili; ili awaangamize nyote wawili.
60Mara hiyo makusanyiko yote wakapaza sauti kwa nguvu, wakamhimidi Mungu awakoaye wamtumainio.
61Wakawaondokea wale wazee wawili, kwa maana Danieli ameuhakikisha ushuhuda wao wa uongo hata vinywani mwao wenyewe.
62Wakawatenda kwa Torati ya Musa kama vile walivyokusudia kwa ukorofi kumfanyia jirani yao; wakawaua; na mwenye damu isiyo na hatia aliokolewa siku ile.[#Kum 19:16-21]
63Kwa hiyo Hilkia na mkewe walimhimidi Mungu kwa ajili ya binti yao Susana, pamoja naye mumewe Yoakimu, na jamaa zao wote; madhali neno la aibu halikuonekana kwake.
64Na tokeapo Danieli alipata sifa kuu machoni pa watu.