The chat will start when you send the first message.
1Basi nilisikitika, nikalia; na katika huzuni yangu niliomba, nikasema,
2Ee BWANA, Wewe ndiwe mwenye haki, na matendo yako yote na njia zako zote ni rehema na kweli, nawe unahukumu kwa kweli na kwa haki milele.
3Unikumbuke, unitazame; usiniadhibu kwa ajili ya dhambi zangu na makosa yangu; wala kwa ajili ya dhambi za baba zangu walioasi mbele zako.
4Kwa maana hawakuzitii amri zako; kwa hiyo umetutoa tuwe mateka, hata na kuuawa; kuwa mithali ya shutumu kwao mataifa yote, ambao kwamba tumetawanyika katikati yao.
5Na sasa hukumu zako ni nyingi na za kweli; hata uje unitende kwa kadiri ya dhambi zangu na za baba zangu; kwa kuwa hatukuzishika amri zako; wala kuenenda kwa kweli mbele zako.
6Basi sasa unitende kama uonavyo vema; uniamuru niondolewe roho yangu, ili niruhusiwe na kuwa udongo tena; maana yanifaa kufa kuliko kuishi, kwa sababu nimesikia mashutumu yasiyo haki, nami naona huzuni nyingi. Uamuru basi nitolewe katika msiba huu niende mahali pa milele; wala usiugeuzie mbali nami uso wako.
7Ikawa siku ile ile huko Ekbatana, mji wa Media. Sara binti Ragueli naye alishutumiwa na wajakazi wa baba yake.
8Maana alikuwa ameolewa na waume saba, bali Asmodeo, yule jini, aliwaua kabla hawajalala naye. Wakamwambia, Wewe hujui ya kuwa umewanyonga waume zako? Umekuwa na waume saba, wala hata mmoja wao hukupata faida naye. Mbona waturudia sisi?
9Ikiwa wao wamekufa, nenda zako nawe ukawafuate; tusikuone kabisa una mwana wala binti.
10Alipoyasikia hayo alifanya huzuni nyingi, akaona afadhali kujinyonga. Akafikiri, Mimi ni binti pekee wa baba yangu; basi nikitenda hivi nitamwia shutumu; nitamshushia uzee wake kwa huzuni hata kaburini.
11Kwa hiyo aliomba, akielekea kwenye dirisha, akasema, Ee BWANA, Mungu wangu, umehimidiwa, na jina lako takatifu tukufu limehimidiwa, matendo yako yote na yakuhimidi milele.
12Na sasa, Ee BWANA, nakuelekezea macho yangu na uso wangu;
13uamuru ili niondolewe duniani, nisizidi kusikia mashutumu.
14Ee BWANA, Wewe unajua kwamba nimekuwa safi mimi; sijafanya dhambi na mwanamume;
15wala sijalinajisi jina langu wakati wowote, wala jina la baba yangu, katika nchi ya kufungwa kwetu. Mimi ni binti pekee wa baba yangu, wala hana mtoto yeyote kuwa mrithi wake, wala ndugu aliye karibu; wala mwana wa ndugu yake, ambaye kwa ajili yake nijilinde ili niolewe naye. Waume zangu saba sasa wamekwisha kufa; mbona basi niishi mimi? Lakini ikiwa haikupendezi nife, uamuru niangaliwe na kuhurumiwa, nisizidi kusikia mashutumu.
16Basi ikawa sala zao wote wawili zilisikiwa mbele za enzi yake Mungu Aliye Juu.
17Rafaeli akatumwa ili awaponye wote wawili, yaani, kuviambua vyamba vyeupe kutoka macho ya Tobiti; na kumwongoza Sara binti Ragueli aolewe na Tobia mwana wa Tobiti; tena kumfunga Asmodeo, yule jini; kwa sababu ni haki yake Tobia kumwoa Sara, maana yu mrithi. Hivyo wakati ule ule mmoja Tobiti alirudi akaingia nyumbani mwake, naye Sara binti Ragueli alishuka katika chumba chake cha juu.[#Hes 36:6-9; Tob 6:10-12]