Tobiti 6

Tobiti 6

Safari ya kwenda Rage

1Basi akaacha kulia.

2Hata walipokuwa wakisafiri walifika jioni kwenye mto Tigri, wakatua huko.

3Yule kijana akateremka mtoni ili kuoga; kumbe! Samaki akaruka kutoka mtoni akitaka kummeza yule kijana.

4Malaika akamwambia, Mkamate yule samaki! Yule kijana akamkamata samaki akamkokota katika nchi kavu.

5Malaika akamwambia, Sasa mpasue samaki huyu, ukachukue moyo na ini na nyongo, ukaviweke salama.

6Yule kijana akafanya kama malaika alivyomwagiza; tena wakamwoka samaki wakamla. Asubuhi wakaenda zao wote wawili mpaka waukaribie Ekbatana.

7Yule kijana akamwuliza malaika, Ndugu yangu Azaria, vya nini hivi moyo na ini na nyongo vya samaki?

8Akamwambia, Kwa habari ya moyo na ini, ikiwa jini au pepo mbaya anamsumbua mtu, yatupasa kumfukizia moshi wa vitu hivi, akiwa ni mwanamume au mwanamke, naye hataudhika tena.

9Na kwa habari ya nyongo, yafaa kumpaka mtu mwenye vyamba vyeupe katika macho, naye atapona.

Maelezo ya Rafaeli

10Ndipo walipoukaribia mji,

11malaika alimwambia yule kijana, Ndugu yangu, leo tutatua kwa Ragueli, aliye jamaa yako; naye ana binti yake pekee, jina lake Sara.

12Huenda nikuposee, ili aolewe nawe. Kwa maana haki ya kumwoa ina wewe, kwa kuwa wewe peke yako ni wa jamaa yake. Naye huyu mwanamwali ni mzuri mwenye busara.

13Basi sasa unisikilize, nami nitasema na baba yake; hata tutakaporudi kutoka Rage tutafanya arusi. Kwa maana najua ya kwamba Ragueli hawezi kumwoza kwa mwingine, kama iamuruvyo Torati ya Musa, ila itampasa kufa; kwa sababu ni haki yako kuupokea urithi huu kuliko mtu mwingine wote.

14Kisha yule kijana akamjibu malaika, Ndugu yangu Azaria, mimi nimesikia ya kama mwanamwali huyu ameolewa na waume saba, nao wote wameangamia katika chumba cha arusi.

15Nami ni mwana pekee wa baba yangu; nami naogopa nisije nikaingia, nikafa kama wale walionitangulia; maana jini ampenda, ambaye hamdhuru mtu ila wale wamkaribiao. Na sasa naogopa nisije nikafa, nikaleta maisha ya baba yangu na mama yangu kaburini kwa huzuni kwa ajili yangu; wala hawana mwana mwingine wa kuwazika.

16Malaika akamwambia, Je! Huyakumbuki mausia aliyokuusia baba yako, ya kuwa uchukue mke wa jamaa yako? Na sasa, ndugu yangu, unisikilize, madhali yapasa awe mke wako; wala usimjali yule jini; kwa maana hata usiku huu huyu ataozwa kuwa mke wako.

17Huku ukiingia katika chumba cha arusi, utatwaa majivu ya ubani, na juu yake utatia vipande vya moyo na ini vya samaki, nawe utafukiza moshi wake.

18Basi yule jini ataisikia harufu yake na kukimbia, wala hatakuja tena kamwe. Lakini utakapomkaribia mkeo, ondokeni wote wawili na kumlilia Mungu mwenye rehema. Naye atawaokoa na kuwarehemuni. Nawe usiogope, kwa sababu umewekewa huyu tangu mwanzo. Nawe utamwokoa, naye atafuatana nawe; tena naona ya kuwa atakuzalia watoto. Basi alipoyasikia hayo, Tobia alimpenda, hata na roho yake ikaambatana naye kabisa.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya