The chat will start when you send the first message.
1Wakafika Ekbatana, wakawasili kwenye nyumba yake Ragueli. Naye Sara akaja kuwapokea, akawasalimu, nao wakamsalimu; kisha akawapeleka ndani ya nyumba.
2Ragueli akamwambia mkewe Edna. Lo! Kijana huyu amefanana sana na Tobiti aliye jamaa yangu.
3Ragueli akawauliza, Ndugu, mmetoka wapi? Wakamwambia, Sisi ni wana wa Naftali, tulio wafungwa huko Ninawi.
4Akawaambia, Je! Mwamfahamu Tobiti, ndugu yetu? Wakasema, Naam, twamfahamu. Akawaambia, Je! Hajambo siku hizi?
5Wakasema, Yu mzima, tena hajambo, na hapa Tobia akasema, Kweli, ndiye baba yangu.
6Mara Ragueli akaruka, akambusu, akalia.[#Mwa 33:4; 45:14; Lk 15:20]
7Akambariki, akamwambia, Wewe u mwana wake mtu mzuri mwema. Lakini aliposikia ya kama Tobiti yu kipofu akahuzunika, akalia,
8kadhalika na mkewe Edna akalia, na binti yake Sara.
9Wakawakaribisha kwa ukunjufu, wakachinja kondoo dume katika kundi, wakawaandalia wingi wa nyama. Kisha Tobia akamwambia Rafaeli, Ndugu yangu Azaria, uziseme zile habari tulizoziongea njiani, ili shauri liishe.
10Akampasha Ragueli habari. Ragueli akamwambia Tobia, Ule, unywe, na kuchangamka, maana ni wajibu wako umwoe mtoto wangu. Lakini nitakuambia kweli.
11Nimemwoza mtoto wangu kwa wanaume saba, na kila walipomkaribia wakafa usiku ule ule. Lakini wewe kwa sasa ujifurahishe. Tobia akamwambia, Mimi sionji kitu hapa, hata mtakapofanya agano na kuagana nami. Ragueli akamjibu, Vema, wewe umtwae tangu sasa kama ilivyo desturi, maana wewe u ndugu yake, naye yu wako. Naye Mungu mwenye rehema awafanikisheni katika mambo yote.
12Akamwita binti yake Sara, akamshika mkono, akampa Tobia ili awe mke wake. Akasema, Tazama umtwae kama iamuruvyo Torati ya Musa, ukampeleke kwa baba yako. Akawabariki.
13Akamwita mkewe Edna, akatwaa kitabu, akaandika hati akaitia mhuri.
14Wakaanza kula.
15Ragueli akamwita mkewe Edna, akamwambia, Mwenzangu, uweke tayari chumba cha pili, ukamlete ndani.
16Akafanya kama alivyomwagiza, akamleta ndani. Akalia, akayapokea na machozi ya binti yake, akamwambia, Jipe moyo mkuu, mwanangu. BWANA wa mbingu na nchi akupe kibali badala ya hii huzuni yako. Jipe moyo mkuu, mwanangu.