Hekima ya Sulemani 11

Hekima ya Sulemani 11

Hekima Iliwaongoza Waisraeli kupita jangwani

1Na kwa mkono wa yule Nabii mtakatifu ikayafanikisha matendo yao.[#Kut 15:22—17:16]

2Hawa Waisraeli walishika njia kupitia jangwa pasipokuwa na watu, na katika nchi isiyokuwa na mapito wakazipiga hema zao.

3Wakawapinga adui, na kuwafukuza wale walioshindana nao.

4Wakaona kiu, wakakulilia, wakapewa maji kutoka mwambani, na kuponywa kiu yao kutoka kwenye gumegume.

Maji yawaangamiza Wamisri na Waisraeli kuokoka

5Kwa maana katika uhitaji wao walifaidiwa kwa mambo yake, ambayo kwa hayo adui zao waliadhibiwa.

6Hapo adui zao waliposumbuka kwa kupata damu iliyowavilia badala ya maji hai ya mtoni (ndiyo adhabu ya amri ile ya kuwaua watoto wachanga),

7hao watu wako walipewa maji tele ya kupita tumaini lao;

8Wakiisha kuoneshwa kwa kiu ile iliyowapata jinsi ulivyowadhibisha watesi wao.

9Yaani, hao walipojaribiwa, ingawa wamerudiwa kwa rehema, walipata kufahamu jinsi wale wabaya walivyoteswa, ambao walihukumiwa kwa hasira;

10maana hao uliwaonya kama baba, na kuwapima; bali wale uliwachunguza kama mfalme mkali, na kuwahukumu kuwa na hatia.

11Naam, kwamba walikuwa wakikaa mbali na wenye haki, au kwamba walikuwa wakikaa karibu nao, walisumbuka vile vile.

12Kwa jinsi walivyoshikwa na majonzi marudufu, na kuugua kwa kuyakumbuka mambo yake yaliyopita.

13Kwa kuwa waliposikia ya kwamba kwa adhabu zao hao wengine wamepata faida, walimkiri BWANA kuwa amekuwapo;

14tena wakaacha kumdharau Musa aliyekuwa amekataliwa hapo kwanza katika chuki. Mwisho wa yote yaliyotukia wakastaajabu, kwa kuwa wameona kiu ya namna nyingine, mbali na hao wenye haki.

Mungu aadhibu waovu

15Walakini kuwa malipo ya mawazo yao mabaya yasiyo maana, ambayo yaliwapoteza, hata waabudu watambazi wasio na akili na kina panya, uliwaletea Wamisri kwa kisasi umati wa viumbe visivyo na akili;[#Kut 8:1-24; 10:12-15]

16ili wajifunze ya kwamba mtu huadhibiwa kwa vitu vile vile, ambavyo kwa hivyo ametenda dhambi.

17Madhali Wewe una uweza wote mkononi mwako, uliyeuumba ulimwengu katika yasiyo na umbo; wala kukosa njia ya kuwaletea wingi wa dubu, au simba wakali,

18au hayawani walioumbwa kigeni, wamejaa ukali, wa namna isiyojulikana, wakitoa kinywani uharibifu wa pumzi ya moto, au wakivuma puani moshi wenye kudhuru, au wakimemetesha machoni cheche za kutisha;

19wenye nguvu ya kuwameza katika ujeuri wao, hata na kuwaangamiza kwa utisho wa kuona tu sura zao.

20Naam, bila hao wangaliweza kuangushwa kwa pumzi moja tu, wakafuatiwa na Haki, na kutawanywa huku na huku kwa mvumo wa uweza wako. Lakini ni kwa kipimo, na kwa hesabu, na kwa uzani, Wewe ulivyoyaratibisha mambo yote.

Mungu ni mwenye nguvu na rehema

21Kwa maana ni sifa yako kuwa na uweza ulio mkuu wakati wote, naye ni nani awezaye kuzipinga nguvu za mkono wako?

22Ulimwengu wote mbele zako ni kama chembe moja katika mizani, na mfano wa tone moja la umande lishukalo asubuhi juu ya ardhi.

23Lakini Wewe unawahurumia watu wote, kwa sababu unao uweza wa kutenda mambo yote; nawe wawaachilia wanadamu dhambi zao, ili wapate kutubu.

24Kwa maana Wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu chochote ulichokiumba.

25Kwa kuwa hungalifanya kamwe kitu chochote kama ungalikichukia; tena kitu chochote kingaliwezaje kudumu, ila kwa mapenzi yako? Au kitu kisichoumbwa nawe kingaliwezaje kuhifadhika?

26Lakini Wewe unaviachilia vyote, kwa kuwa ni vyako, Ee Mfalme Mkuu mpenda roho za watu; maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya