Hekima ya Sulemani 17

Hekima ya Sulemani 17

Mapigo yaliyowapiga Wamisri usiku

1Kwa kuwa hukumu zako zi kuu nazo ni ngumu za kusimulia, ndiyo maana watu ovyo hupotea.

2Kwa maana wale wakorofi walipodhania ya kuwa wanashika taifa takatifu kwa nguvu, wao wenyewe walikuwa wamefungwa gizani, na kukazwa kwa minyororo ya usiku mrefu, wakitiwa sharti nyumbani mwao na kufukuzwa mbali na maongozi yako.

3Pindi walipodhania ya kwamba hawakuonekana katika dhambi zao za siri walitawanyika kila mmoja na mwenzake kwa pazia jeusi la usahaulifu wakashikwa na hofu ya kutisha, na kufadhaika kwa matokeo ya kivuli.

4Nyumba zao zenye giza walipokaa hawa kuzilinda na hofu, ila sauti za kuwafadhaisha ziliwazunguka kwa kishindo, na vituko vilitokea, vya kuhuzunisha, vyenye nyuso za kukunjamana.

5Wala moto haukuwa na nguvu ya kutosha ili kuwaangaza, wala mwanga wa nyota haukuwa na uwezo wa kumulika katika usiku ule wa giza;

6ila walitokewa tu na kimoto kama wa moto uliojiwasha, na cha kutisha kabisa; na wakitishwa na matokeo hayo wasiyoweza kuyatazama walihesabu yale waliyoyaona kuwa ya kutisha zaidi.

7Tena hila za uchawi zilishindwa, na majisifu ya akili zao yakakemewa kwa aibu nyingi;

8maana wale walioahidi kufukuza hofu na fadhaa mbali na mwenye ugonjwa walikuwa wagonjwa wenyewe kwa woga wa kuchekesha.

9Ingawa hawakutishwa na kitu cha kuwataabisha, walitiwa hofu ya viumbe vitambaavyo na ya sauti ya nyoka, wakaangamia kwa kutetemeka, wakikataa hata kuitazama hewa isiyoepukika pande zote.

10Kwa maana ubaya asili yake ni woga, unahukumiwa kuwa mbaya na yule shahidi aliye ndani, na kwa kufuatiwa na dhamiri unatabiri yaliyo mabaya kabisa.

11Madhali woga ni kuitupa misaada iliyoletwa na akili,

12na kwa kuwa moyoni kutumaini kumepungua, kutokujua sababu iletayo udhia kumezidishwa.

13Lakini wao, usiku kucha usio na nguvu, uliowajia kutoka ahera ya chini isiyo na nguvu, walikuwa wakilala usingizi sawasawa;

14pengine wakaogofishwa kwa matokeo ya kutisha, pengine, wakafadhaishwa kwa jinsi walivyokata tamaa; maana hofu isiyotazamiwa iliwajia kwa ghafla.

15Kwa hiyo kila mtu, awaye yote, akijilaza pale alipo, akafungwa katika gereza ile isiyokuwa na fito za chuma;

16kwamba ni mkulima, au mchungaji, au kibarua mwenye kazi za nyikani, akapatwa na kushikwa na sharti isiyoepukika, kwa maana walifungwa wote kwa mnyororo mmoja wa giza.

17Endapo walisikia baridi ivumayo, au sauti nzuri ya ndege katika matawi yaeneayo, au mabomoko ya maji yakienda kasi, au kuanguka miamba iliyovurumishwa,

18au wanyama wasioonekana wakikimbia ghafla na kuruka, au sauti ya hayawani wakinguruma kwa ukali, au mwangwi ukitoka katika mivungu ya milimani; hayo yaliwaduwaza kwa hofu kuu.

19Maana penginepo pote ulimwengu uliangazwa nuru nakawa, watu wakijishughulisha na kazi bila mgogoro;

20ila juu yao peke yao umetandikwa usiku mzito, kielelezo cha giza lile litakalowapokea baadaye; naam, nafsini mwao hao wakawa wazito kuliko giza lenyewe.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya