Zab 80

Zab 80

Sala ya Kurejeshwa kwa Israeli

1Wewe uchungaye Israeli, usikie,[#Kut 25:22; Kum 33:2; 1 Sam 4:4; Zab 89:1]

Wewe umwongozaye Yusufu kama kundi;

Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.

2Mbele ya Efraimu, na Benyamini, na Manase,

Uziamshe nguvu zako,

Uje, utuokoe.

3Ee Mungu, uturudishe,[#1 Fal 18:37]

Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

4Ee BWANA, Mungu wa majeshi, hata lini

Utayaghadhibikia maombi ya watu wako?

5Umewalisha mkate wa machozi,

Umewanywesha machozi kwa kipimo kikuu.

6Unatufanya sababu ya ugomvi kwa jirani zetu,

Na adui zetu wanacheka wao kwa wao.

7Ee Mungu wa majeshi, uturudishe,

Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

8Ulileta mzabibu kutoka Misri,[#Isa 5:1,7; Yer 2:21; Eze 15:6]

Ukawafukuza mataifa ukaupanda.

9Ulitengeneza nafasi mbele yake,

Nao ukatia mizizi sana ukaijaza nchi.

10Milima ilifunikwa kwa uvuli wake,

Matawi yake ni kama mierezi ya Mungu.

11Nao uliyaeneza matawi yake hata baharini,[#Kut 23:31; Zab 72:8]

Na vichipukizi vyake hata kunako Mto.

12Kwa nini umezibomoa kuta zake,[#Isa 5:5]

Wakauchuma wote wapitao njiani?

13Nguruwe wa msituni wanauharibu,

Na hayawani wa kondeni wanautafuna.

14Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,[#Zek 1:12,16,17; Isa 63:15]

Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.

15Na mche ule ulioupanda[#Isa 49:5]

Kwa mkono wako wa kuume;

Na tawi lile ulilolifanya

Kuwa imara kwa nafsi yako.

16Umechomwa moto; umekatwa;

Kwa lawama ya uso wako wanapotea.

17Mkono wako na uwe juu yake[#Zab 89:21; Kut 4:22; Zab 110:1; Dan 7:13,14; Yn 5:21-27]

Mtu wa mkono wako wa kuume;

Juu ya mwanadamu uliyemfanya

Kuwa imara kwa nafsi yako;

18Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma;

Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.

19Ee BWANA, Mungu wa majeshi, uturudishe,[#Hes 6:25; Zab 27:4,9]

Uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania