Matendo 26

Matendo 26

1AGRIPPA akamwambia Paolo, Una rukhusa kusema mimeno yako. Ndipo Paolo akanyosha mkono wake, akajitetea.

2Najiona nafsi yangu kuwa na kheri, ee mfalme Agrippa, kwa kuwa nitajitetea mbele yako leo, katika mambo yale niliyoshitakiwa na Wayahudi.

3Khassa kwa sababu wewe unajua sana desturi na maswali yote waliyo nayo Wayahudi: kwa sababu hiyo nakuomba unisikilize kwa uvumilivu.

4Kwa maana Wayahudi wote wanajua maisha yangu tangu ujana, yaliyokuwa tangu mwanzo katika taifa langu Yerusalemi,

5wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nalikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa.

6Na sasa ninasimama hapa nihukumiwe kwa ajili ya tumaini la ahadi waliyopewa baba zetu na Mungu,

7ambayo kabila zetu thenashara wanataraja kuifikia, wakimkhudumu Mungu kwa bidii mchana na usiku. Nami ninashitakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hilo, ee Mfalme.

8Kwa nini limedhaniwa nanyi kuwa neno lisilosadikika, kwamba Mungu awafufua wafu?

9Kweli, mimi mwenyewe naliona ndani ya nafsi yangu kwamba yanipasa kutenda mambo mengi yaliyopingamana na jina lake Yesu Mnazareti;

10nikayafanya Yerusalemi: niliwafunga wengi miongoni mwa watakatifu ndani ya magereza, nikiisha kupewa amri na makuhani wakuu; na walipouawa nalitoa idhini yangu.

11Na marra nyingi katika masunagogi mengi naliwaadhibu, nikawashurutisha kukufuru; nikawaonea hasira kama nina wazimu, nikawaudhi hatta katika miji ya ugenini.

12Bassi katika kazi hiyo nalikuwa nikienda Dameski, nimepewa mamlaka na maagizo na makuhani wakuu.

13Ee Mfalme, wakati wa adhdhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote.

14Tukaanguka chini sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya Kiebrania, Saul! Saul! ya nini kunindhi? ni vigumu kwako kunpiga mateke mchokoo.

15Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambae wewe unaniudhi.

16Lakini inuka, usimame, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke nwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo kwayo nitajidhihirisha kwako;

17nikikuokoa na watu wako, na watu wa mataifa, ambao nakutuma kwao;

18uwafumhue macho yao, waiache giza na kuielekea nuru, na waziache nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu, na wapate masamaha ya dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu.

19Kwa hiyo, ee Mfalme Agrippa, sikuiasi ile njozi ya mbinguni,

20hali kwanza niliwakhubiri wale wa Dameski na Yerusalemi, na katika inchi yote ya Yahudi, na watu wa mataifa, watubu wakamwelekee Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao.

21Kwa sababu ya hayo Wayahudi wakanikamata ndani ya hekalu wakajaribu kuniua.

22Bassi nikiisha kuupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hatta leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, wala sisemi neno illa yale ambayo manabii na Musa waliyasema, kwamba yatakuwa;

23ya kwamba Kristo hana buddi kuteswa na ya kwamba yeye kwanza kwa kufufuliwa katika wafu atatangaza khabari za nuru kwa watu wake na kwa watu wa mataifa.

24Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paolo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugenza akili zako.

25Lakini Paolo akasema, Sina wazimu, ee Festo il-aziz, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili.

26Kwa maana mfalme anajua khabari za mambo haya, na naweza kusema nae bila khofu, kwa sababu najua sana ya kuwa hapana neno moja katika hayo asilolijua; kwa maana jambo hilo halikutendeka pembeni.

27Mfalme Agrippa, wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini.

28Agrippa akamwambia Paolo, Kwa maneno machache wataka kunifanya kuwa Mkristo.

29Paolo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi si wewe tu illa na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi pasipo vifungo hivi.

30Na alipokwisha kusema haya mfalme na liwali na Bereniki na wale walioketi pamoja nao wakasimama,

31wakaenda mbali kidogo wakasemezana, wakisema, ya kama, Mtu huyo hatendi neno linalostahili kifo wala kufungwa.

32Agrippa akamwambia Festo, Mtu huyo angeweza kufunguliwa kama asingalitaka rufaani kwa Kaisari.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania