Matendo 14

Matendo 14

Paulo na Barnaba Wakiwa Ikonia

1Paulo na Barnaba walikwenda katika mji wa Ikonia. Kama walivyofanya Antiokia, waliingia katika sinagogi la Kiyahudi. Walizungumza na watu pale. Walizungumza kwa ushawishi sana kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wengi waliamini walichosema.

2Lakini Baadhi ya Wayahudi hawakuamini. Wayahudi hao walisema mambo yaliyowafanya wasio Wayahudi kukasirika na kuwa kinyume na waamini.

3Hivyo Paulo na Barnaba walikaa Ikonia kwa muda mrefu, na walihubiri kwa ujasiri kwa ajili ya Bwana. Waliwahubiri watu kuhusu neema ya Mungu. Bwana alithibitisha kwamba kile walichosema ni kweli kwa ishara na maajabu yaliyofanyika kufanyika kupitia wao.

4Lakini baadhi ya watu katika mji wakakubaliana na Wayahudi ambao hawakuwaamini Paulo na Barnaba. Baadhi walikubaliana na mafundisho ya mitume. Hivyo mji uligawanyika.

5Baadhi ya Wayahudi, viongozi wao na baadhi ya watu wasio wayahudi, walidhamiria kuwaumiza Paulo na Barnaba. Walitaka kuwaua kwa kuwapiga kwa mawe.

6Paulo na Barnaba walipotambua kuhusu hili, wakaondoka katika mji huo. Walikwenda Listra na Derbe, miji katika Likonia na maeneo yanayozunguka Likonia.

7Wakahubiri Habari Njema huko pia.

Paulo na Barnaba Wakiwa Listra na Derbe

8Katika mji wa Listra kulikuwa mtu aliyekuwa na tatizo katika mguu wake. Alizaliwa akiwa mlemavu wa miguu na hakuwahi kutembea.

9Alikuwa amekaa akimsikiliza Paulo akizungumza. Paulo alipomwangalia kwa kumkazia macho alitambua kuwa mtu huyo alikuwa na imani kuwa Mungu angemponya.

10Hivyo Paulo akapaza sauti na kumwambia, “Simama kwa miguu yako!” Mtu yule akaruka na kuanza kutembea.

11Watu walipoona alichofanya Paulo, walipaza sauti kwa lugha yao wenyewe ya Kilikaonia. Walisema, “Miungu wamekuja kwetu katika maumbo ya kibinadamu!”

12Watu wakaanza kumwita Barnaba “Zeusi”, na Paulo “Hermesi”, kwa sababu ndiye alikuwa mzungumzaji mkuu.

13Hekalu la Zeusi lilikuwa karibu na mji. Kuhani wa hekalu hili alileta mafahali ya ng'ombe kadhaa na mashada ya maua kwenye lango la mji. Kuhani na watu walitaka kuwatolea sadaka Paulo na Barnaba.[#14:13 Wanyama waliotakiwa kutolewa dhabihu walivalishwa mashada haya kuzunguka shingo zao.]

14Lakini mitume, Barnaba na Paulo walipoelewa jambo ambalo watu walikuwa wanafanya, walirarua mavazi yao. Kisha wakakimbia kuingia katikati ya watu na kuwaambia kwa kupaza sauti zao wakisema:[#14:14 Hii ilionesha kuwa hawakufurahishwa na kitendo hicho.]

15“Ndugu, kwa nini mnafanya hivi? Sisi si miungu. Ni wanadamu kama ninyi. Tulikuja kuwaambia Habari Njema. Tunawaambia mviache vitu hivi visivyo na thamani. Mgeukieni Mungu wa kweli aishiye, aliyeumba mbingu, nchi, bahari na vyote vilivyomo ndani yake.

16Huko nyuma Mungu aliyaacha mataifa yote yatende yale waliyotaka.

17Lakini daima Mungu alikuwepo na alitenda mambo mema yanayothibitisha kuwa yeye ni wa hakika na wa kweli. Huwapa mvua kutoka mbinguni na mavuno bora kwa wakati sahihi. Huwapa chakula tele na kuijaza mioyo yenu kwa furaha.”

18Hata baada Paulo na Barnaba kusema hayo, hawakuweza kuwazuia watu kuwatolea sadaka za kuteketezwa.

19Ndipo baadhi ya Wayahudi wakaja kutoka Antiokia na Ikonia na kuwashawishi watu ili wampinge Paulo. Hivyo wakamtupia mawe na kumburuza kumtoa nje ya mji. Wakidhani kuwa wamemwua.

20Lakini wafuasi wa Yesu walipokusanyika kumzunguka, aliamka na kuingia mjini. Siku iliyofuata yeye na Barnaba waliondoka na kwenda katika mji wa Derbe.

Kurudi Antiokia ya Shamu

21Walihubiri pia Habari Njema katika mji wa Derbe, na watu wengi wakawa wafuasi wa Yesu. Kisha Paulo na Barnaba walirudi katika miji ya Listra, Ikonia na Antiokia.

22Katika miji hiyo waliwasaidia wafuasi kukua na kuwa na nguvu katika imani yao na waliwatia moyo kuendelea kumwamini Mungu. Waliwaambia, “Ni lazima tuteseke kwa mambo mengi katika safari yetu ya kwenda katika ufalme wa Mungu.”

23Waliwachagua pia wazee katika kila kanisa na kuacha kula kwa muda ili kuwaombea. Wazee hawa walikuwa wanaume wanaomtumaini Bwana Yesu, hivyo Paulo na Barnaba wakamwomba Bwana awalinde.

24Paulo na Barnaba walipita katikati ya eneo la Pisidia. Kisha walifika katika jimbo la Pamfilia.

25Waliwahubiri watu ujumbe wa Mungu katika mji wa Perge, kisha wakateremka kwenda katika mji wa Attalia.

26Na kutoka huko wakatweka tanga kwenda katika mji wa Antiokia ya Shamu. Huu ni mji ambako waamini waliwaweka katika uangalizi wa Mungu na kuwatuma kufanya kazi hii. Na sasa walikuwa wameimaliza.

27Paulo na Barnaba walipofika, walilikusanya kanisa pamoja. Waliwaambia waamini yote ambayo Mungu aliwatumia kutenda. Walisema, “Mungu amefungua mlango kwa watu wasio Wayahudi kuamini!”

28Na walikaa pale pamoja na wafuasi wa Bwana kwa muda mrefu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International