Wakolosai 2

Wakolosai 2

1Ninataka mfahamu ni kwa kiwango gani ninawajali ninyi pamoja na ndugu waishio Laodikia na wengine ambao hawajawahi kuniona.

2Ninataka ninyi nyote pamoja na wao mtiwe moyo na kuunganishwa pamoja katika upendo na kupata uhakika unaoletwa kwa kuielewa ile kweli. Pia, ninataka waijue kweli iliyokuwa siri ambayo sasa imefunuliwa na Mungu. Kweli hiyo ni Kristo mwenyewe.

3Yeye peke yake ndiye ambaye ndani yake watu wanaweza kupata hazina zote za hekima na ufahamu zilizofichwa katika Kristo.

4Nawaambia hili ili asiwepo yeyote atakaye wadanganya kwa maneno na hoja zinazoonekana kuwa ni nzuri, lakini ni mbaya.

5Ingawa niko mbali kimwili, niko pamoja nanyi katika roho. Ninafurahi kuona jinsi mnavyofanya kazi vizuri pamoja na jinsi imani yenu ilivyo thabiti katika Kristo.

Endeleeni Kumfuata Kristo Yesu

6Mlimpokea Kristo Yesu kama Bwana, hivyo mwendelee kumfuata yeye.

7Na mizizi yenu ikue hata ndani ya Kristo, na maisha yenu yajengwe juu yake. Kama mlivyofundishwa imani ya kweli mwendelee kuwa imara katika ufahamu wenu katika hilo. Na msiache kumshukuru Mungu.

8Angalieni msichukuliwe mateka na mafundisho ya uongo kutoka kwa watu wasio na chochote cha maana kusema, bali kuwadanganya tu. Mafundisho yao hayatoki kwa Kristo bali ni desturi za kibinadamu tu na zinatoka katika nguvu za uovu zinazotawala maisha ya watu.

9Nasema hili kwa sababu Mungu mwenyewe kama alivyo, ukamilifu wa uungu wake unaishi ndani ya Kristo. Hii ni hata wakati wa maisha yake hapa duniani.

10Na kwa sababu ninyi ni wa Kristo basi mmekamilika, na mna kila kitu mnachohitaji. Kristo ni mtawala juu ya kila nguvu na mamlaka zingine zote.

11Mlitahiriwa katika Kristo kwa namna tofauti, si kwa mikono ya kibinadamu. Hii ni kusema ya kwamba, mlishiriki katika kifo cha Kristo, ambacho kilikuwa aina ya tohara kwa namna ya kuuvua mwili wake wa kibinadamu.[#2:11 Kwa maana ya kawaida, “katika kuuvua mwili kwenye tohara ya Kristo”. Tazama katika Orodha ya Maneno.]

12Na mlipobatizwa, mlizikwa na kufufuka pamoja naye kutokana na imani yenu kwa nguvu za Mungu aliyemfufua Kristo kutoka katika kifo.

13Mlikuwa wafu kiroho kwa sababu ya dhambi zenu na kwa sababu hamkuwa sehemu ya watu wa Mungu. Lakini Mungu amewapa ninyi uhai mpya pamoja na Kristo na amewasamehe dhambi zenu zote.[#2:13 Kwa maana ya kawaida, “na kwa sababu ya kutokutahiriwa kwa miili yenu”.]

14Kwa sababu tulizivunja sheria za Mungu, tunalo deni. Kumbukumbu ya deni hilo imeorodhesha amri zote tulizoshindwa kuzifuata. Lakini Mungu ametusamehe deni hilo. Ameiondoa kumbukumbu yake na kuipigilia msalabani.

15Pale msalabani, aliwanyang'anya watawala wa ulimwengu wa roho nguvu na mamlaka. Aliwashinda pale. Na akawafukuza kama wafungwa ili ulimwengu wote uone.

Msizifuate Sheria Zilizowekwa na Watu

16Hivyo msimruhusu mtu yeyote awahukumu katika masuala yanayohusu kula au kunywa au kwa kutofuata desturi za Kiyahudi (kusherehekea siku takatifu, sikukuu za Mwandamo wa Mwezi, au siku za Sabato).[#2:16 Siku ya kwanza ya Mwezi kwa Waisraeli au Wayahudi, ambayo waliisherehekea kama siku maalum ya kupumzika na kumwabudu Mungu. Walikusanyika pamoja na kutoa sadaka za imani kama zile zinazoainishwa katika Law 7:16-21.]

17Zamani mambo hayo yalikuwa kama kivuli cha yale yaliyotarajiwa kuja. Lakini mambo mapya yaliyotarajiwa kuja yanapatikana katika Kristo.

18Watu wengine hufurahia kutenda mambo yanayowafanya wajisikie kuwa ni wanyenyekevu na kisha kushirikiana na malaika katika ibada. Nao wanazungumza juu ya kuyaona mambo hayo katika maono. Msiwasikilize wanapowaambia kuwa mnakosea kwa sababu hamfanyi mambo haya. Ni ujinga kwao kujisikia fahari kwa kufanya hivyo, kwa sababu mambo hayo yote yanatokana na namna mwanadamu anavyofikiri.[#2:18 Au “kuabudu pamoja na malaika” au “huona maono ya malaika”.]

19Hawajafungamanishwa na kichwa; Kristo ndiye kichwa, na mwili wote humtegemea Yeye. Kwa sababu ya Kristo viungo vyote vya mwili vinatunzana na kusaidiana kila kimoja na kingine. Hivyo mwili hupata nguvu zaidi na kufungamana pamoja kadri Mungu anavyouwezesha kukua.

20Mlikufa pamoja na Kristo na kuwekwa huru kutoka katika nguvu zinazotawala dunia. Hivyo kwa nini mnaishi kama watu ambao bado mngali wa ulimwengu? Nina maana kuwa, kwa nini mnafuata sheria hizi:

21“Usile hiki”, “Usionje kile”, “Usiguse kile”?

22Sheria hizi zinazungumzia vitu vya kidunia, vitu vinavyotokomea baada ya kutumiwa. Ni amri na mafundisho ya kibinadamu tu.

23Sheria hizi zinaweza kuonekana za busara kama sehemu ya dini zilizoundwa na watu ambamo watu huiadhibu miili yao na kutenda mambo yanayowafanya wajisikie wanyenyekevu. Lakini sheria hizi haziwasaidii watu kuthibiti tamaa zao za udhaifu wa kibinadamu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International