Waefeso 2

Waefeso 2

Kutoka Mauti hadi Uzima

1Zamani mlikuwa wafu kiroho kwa sababu ya dhambi na mambo mliyotenda kinyume na Mungu.

2Ndiyo, zamani maisha yenu yalijaa dhambi hizo. Mliishi kwa namna ya ulimwengu; mkimfuata mkuu wa nguvu za uovu zilizo katika anga, roho hiyo hiyo inatenda kazi sasa ndani ya watu wasiomtii Mungu.[#2:2 Tazama katika Orodha ya Maneno.]

3Tuliishi hivyo zamani, tukijaribu kuzifurahisha tamaa zetu za mwili. Tulitenda mambo ambayo miili na akili zetu zilitaka. Kama ilivyo kwa kila mtu ulimwenguni, tulistahili kuteseka kutokana na hasira ya Mungu kwa sababu ya jinsi tulivyokuwa.

4Lakini Mungu ni mwingi wa rehema na anatupenda sana.

5Tulikuwa wafu kiroho kwa sababu ya matendo maovu tuliyotenda kinyume naye. Lakini yeye alitupa maisha mapya pamoja na Kristo. (Mmeokolewa na neema ya Mungu.)

6Ndiyo, ni kwa sababu sisi ni sehemu ya Kristo Yesu, ndiyo maana Mungu alitufufua pamoja naye kutoka kwa wafu na akatuketisha pamoja naye mbinguni.

7Mungu alifanya hivi ili wema wake kwetu sisi tulio wa Kristo Yesu uweze kuonesha nyakati zote zinazokuja utajiri wa ajabu wa neema yake.

8Nina maana ya kuwa mmeokolewa kwa neema kwa sababu mliweka imani yenu kwake. Hamkujiokoa ninyi wenyewe; bali ni zawadi kutoka kwa Mungu.[#2:8 Au “kwa sababu ya uaminifu wake”.]

9Msijisifu kwa kuwa hamkuokolewa kutokana na matendo yenu.

10Mungu ndiye aliyetufanya hivi tulivyo. Ametuumba wapya katika Kristo Yesu ili tutende mambo mema katika maisha yetu. Mambo aliyokwisha kutupangia.

Wamoja Katika Kristo

11Hamkuzaliwa mkiwa Wayahudi. Ninyi ni watu ambao Wayahudi huwaita “Wasiotahiriwa”, na wao wakijiita “Waliotahiriwa” (Tohara yao ni ile inayofanyika kwenye miili yao kwa mikono ya binadamu.)[#2:11 Watu wasio na alama ya tohara kama Wayahudi.]

12Kumbukeni ya kwamba zamani hamkuwa na Kristo. Hamkuwa raia wa Israeli na hamkujua kuhusu maagano ya maagano ambayo Mungu aliyaweka kwa watu wake. Hamkuwa na tumaini na hamkumjua Mungu.[#2:12 Maagano au ahadi maalum ambazo Mungu alizitoa nyakati tofauti kwa watu katika Agano la Kale. Tazama katika Orodha ya Maneno.]

13Lakini sasa mmeungana na Kristo Yesu. Ndiyo, wakati fulani hapo zamani mlikuwa mbali na Mungu, lakini sasa mmeletwa karibu naye kupitia sadaka ya damu ya Kristo.

14Kristo ndiye sababu ya amani yetu. Yeye ndiye aliyetufanya sisi Wayahudi nanyi msio Wayahudi kuwa wamoja. Tulitenganishwa na ukuta wa chuki uliokuwa kati yetu, lakini Kristo aliubomoa. Kwa kuutoa mwili wake mwenyewe,

15Kristo aliisitisha sheria pamoja na kanuni na amri zake nyingi. Kusudi lake lilikuwa ni kuyafanya makundi mawili yawe wanadamu wamoja waliounganishwa naye. Kwa kufanya hivi alikuwa analeta amani.

16Kupitia msalaba Kristo alisitisha uhasama kati ya makundi mawili. Na baada ya makundi haya kuwa mwili mmoja, alitaka kuwapatanisha wote tena kwa Mungu. Alifanya hivi kwa kifo chake msalabani.

17Kristo alikuja na kuwaletea ujumbe wa amani ninyi msio Wayahudi mliokuwa mbali na Mungu. Na aliwaletea pia ujumbe huo wa amani watu waliokaribu na Mungu.

18Ndiyo, kupitia Kristo sisi sote tuna haki ya kumjia Baba katika Roho mmoja.

19Hivyo ninyi msio Wayahudi si wageni wala wahamiaji, lakini ninyi ni raia pamoja na watakatifu wa Mungu. Ninyi ni wa familia ya Mungu.

20Ninyi mnaoamini ni kama jengo linalomilikiwa na Mungu. Jengo hilo limejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii. Kristo Yesu mwenyewe ndiye jiwe kuu la muhimu sana katika jengo hilo.[#2:20 Kwa maana ya kawaida, “Jiwe na msingi kwenye pembe”. Jiwe la kwanza na la muhimu sana katika jengo.]

21Jengo lote limeunganishwa katika Kristo, naye hulikuza na kuwa hekalu takatifu katika Bwana.[#2:21 Nyumba ya Mungu, mahali ambapo watu wa Mungu humwabudu. Hapa, inamaanisha kuwa waamini ndiyo hekalu la kiroho ambamo Mungu anaishi.]

22Na katika Kristo mnajengwa pamoja na watu wake wengine. Mnafanywa kuwa makazi ambapo Mungu anaishi katika Roho.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International