Waebrania 9

Waebrania 9

Ibada Chini ya Patano la Kale

1Patano la kwanza lilikuwa na kanuni kwa ajili ya kuabudu na mahali pa kuabudia hapa duniani.

2Mahali hapa palikuwa ni ndani ya hema. Eneo la kwanza ndani ya hema liliitwa Patakatifu. Katika Patakatifu kulikuwepo taa na meza iliyokuwa na mikate maalumu iliyotolewa kwa Mungu.

3Nyuma ya pazia la pili kilikuwepo chumba kilichoitwa Patakatifu pa Patakatifu.

4Katika Patakatifu pa Patakatifu kulikuwepo madhabahu ya dhahabu kwa ajili ya kuchoma uvumba. Pia lilikuwepo Sanduku la Agano. Sanduku lilifunikwa kwa dhahabu. Ndani ya hilo Sanduku kulikuwemo birika la mana na fimbo ya Haruni; fimbo ambayo iliwahi kuchipusha matawi. Vilevile ndani ya Sanduku yalikuwemo mawe bapa yaliyoandikwa Amri Kumi za agano la kale kwao.

5Juu ya Sanduku walikuwepo viumbe wenye mbawa walioonesha utukufu wa Mungu. Viumbe hawa wenye mbawa walikuwa juu ya sehemu ya rehema. Lakini hatuwezi kusema chochote kuhusu hili hivi sasa.[#9:5 Au “kiti cha rehema”, mahali juu ya “sanduku la Agano”, ambapo kuhani mkuu alinyunyizia damu ya mnyama mara moja kwa mwaka kufidia dhambi za watu.]

6Kila kitu ndani ya hema kilikuwa kimewekwa tayari kwa namna nilivyoeleza. Kisha makuhani waliingia ndani ya chumba cha kwanza kila siku kutekeleza shughuli zao za ibada.

7Lakini ni kuhani mkuu tu aliweza kuingia kwenye chumba cha pili, na aliingia mara moja tu kwa mwaka. Pia, asingeweza kuingia ndani ya chumba hicho bila kuchukua damu pamoja naye. Aliitoa damu hiyo kwa Mungu kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya dhambi walizotenda watu bila kujua kwamba walikuwa wanatenda dhambi.

8Roho Mtakatifu hutumia vyumba hivi viwili tofauti kutufundisha kwamba njia ya kuelekea Patakatifu pa Patakatifu haikuwa wazi wakati chumba cha kwanza kilipokuwepo.

9Huu ni mfano kwetu leo. Inaonyesha sadaka na sadaka ambazo makuhani walizitoa kwa Mungu haziwezi kufanya dhamiri za wanaoabudu ziwe safi kabisa.

10Sadaka na sadaka hizi ni kwa ajili tu ya vyakula na vinywaji na aina maalumu ya kuoga. Ni sheria kuhusu mwili tu. Mungu alizitoa kwa watu wake wazifuate hadi wakati wa njia yake mpya.

Ibada Chini ya Patano Jipya

11Lakini Kristo tayari amekuja awe kuhani mkuu. Yeye ni kuhani mkuu wa mambo mema tuliyonayo sasa. Lakini Kristo hatumiki ndani ya eneo kama hema ambalo makuhani wale walitumika ndani yake. Anatumika katika eneo bora zaidi. Tofauti na hema lile, hili ni kamilifu. Halikutengenezwa hapa duniani. Siyo la ulimwengu huu.

12Kristo aliingia Patakatifu Zaidi mara moja tu; hii ilitosha kwa nyakati zote. Aliingia Patakatifu Zaidi kwa kutumia damu yake mwenyewe, siyo damu ya mbuzi au ya ng'ombe wadogo. Aliingia hapo na kutuweka huru milele kutoka katika dhambi.

13Damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ng'ombe zilinyunyizwa juu ya wale ambao hawakuwa safi vya kutosha tena kuweza kuingia katika eneo la kuabudia. Damu na majivu viliwafanya wawe safi tena, lakini katika miili yao tu.

14Hivyo hakika sadaka ya damu ya Kristo inaweza kufanya mambo bora zaidi. Kristo alijitoa mwenyewe kupitia Roho wa milele kama sadaka kamilifu kwa Mungu. Damu yake itatutakasa kabisa sisi kutoka katika maovu tuliyotenda. Itatupa sisi dhamiri safi ili tuweze kumwabudu Mungu aliye hai.

15Hivyo Kristo huwaletea watu wake agano jipya kutoka kwa Mungu. Huleta agano hili ili wale walioteuliwa na Mungu waweze kuzipata baraka ambazo Mungu aliwaahidi, baraka zinazodumu milele. Hili laweza kutokea tu kwa sababu Kristo alikufa ili awaweke huru watu kutokana na dhambi zilizotendwa dhidi ya amri za agano la kwanza.

16Mtu anapofariki na akaacha usia, ni lazima uwepo uthibitisho kwamba yule aliyeandika usia amefariki.

17Usia haumaanishi chochote wakati aliyeuandika bado yuko hai. Unaweza kutumika mara tu baada ya kifo cha mtu huyo.

18Ndiyo sababu ili kuthibitisha kifo damu ilihitajika ili kuanza agano la kwanza baina ya Mungu na watu wake.

19Kwanza, Musa aliwaeleza watu kila agizo katika sheria. Kisha akachukua damu ya ndama dume na kuichanganya na maji. Alitumia sufu nyekundu na tawi la hisopo kunyunyiza damu na maji katika kitabu cha sheria na kwa watu.[#9:19 Nakala zingine za kale za toleo la Kiyunani zina “ng'ombe dume na mbuzi.”]

20Kisha akasema, “Hii ni damu inayoweka agano liwe zuri agano ambalo Mungu aliwaagiza mlifuate.”[#Kut 24:8]

21Kwa jinsi hiyo hiyo, Musa alinyunyiza damu katika Hema Takatifu. Aliinyunyiza damu juu ya kila kitu kilichotumika katika ibada.

22Sheria inasema kwamba karibu kila kitu kinapaswa kutakaswa kwa damu. Dhambi haziwezi kusamehewa bila sadaka ya damu.

Yesu Kristo ni Dhabihu yetu kwa Ajili ya Dhambi

23Mambo haya ni nakala ya mambo halisi yaliyoko mbinguni. Nakala hizi zinapaswa kutakaswa kwa sadaka ya wanyama. Lakini mambo halisi yaliyoko mbinguni yanapaswa kuwa na sadaka zilizo bora zaidi.

24Kristo alienda katika Patakatifu pa Patakatifu. Lakini hapakuwa mahali palipotengenezwa na mwanadamu, ambapo ni nakala tu ya ile iliyo halisi. Alienda katika mbingu, na yuko huko sasa mbele za Mungu ili atusaidie sisi.

25Kuhani mkuu huingia katika Patakatifu pa Patakatifu mara moja tu kila mwaka. Huchukua pamoja naye damu ya sadaka. Lakini hatoi damu yake kama alivyofanya Kristo. Kristo alienda mbinguni, lakini siyo kujitoa mwenyewe mara nyingi kama ambavyo kuhani mkuu hutoa damu tena na tena.

26Kama Kristo alijitoa mwenyewe mara nyingi, basi angehitaji kuteseka mara nyingi tangu wakati dunia ilipoumbwa. Lakini alikuja kujitoa mwenyewe mara moja tu. Na mara hiyo moja inatosha kwa nyakati zote. Alikuja katika wakati ambao ulimwengu unakaribia mwisho. Alikuja kuchukua dhambi zote kwa kujitoa mwenyewe kama sadaka.

27Kila mtu atakufa mara moja tu. Baada ya hapo ni kuhukumiwa.

28Hivyo Kristo alitolewa kama sadaka mara moja kuchukua dhambi za watu wengi. Na atakuja mara ya pili, lakini siyo kujitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi. Atakuja mara ya pili kuleta wokovu kwa wale wanaomngojea.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International