Yuda 1

Yuda 1

1Salamu kutoka kwa Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo na ndugu yake Yakobo. Kwa wale waliochaguliwa na kupendwa na Mungu Baba na kulindwa ndani ya Yesu Kristo.

2Rehema, amani na upendo viwe pamoja nanyi zaidi na zaidi.

Mungu Atawaadhibu Watendao Mabaya

3Rafiki wapendwa, nilitaka sana kuwaandikia kuhusu wokovu tunaoshiriki pamoja. Lakini nimejisikia kuwa ni muhimu niwaandikie kuhusu kitu kingine: Ninataka kuwatia moyo kuipigania kwa nguvu imani ambayo Mungu aliwapa watakatifu wake. Mungu alitoa imani hii mara moja na ni nzuri wakati wote.

4Baadhi ya watu wamejiingiza kwa siri kwenye kundi lenu. Watu hawa wamekwisha kuhukumiwa kuwa wakosaji kwa sababu ya matendo yao. Zamani zilizopita manabii waliandika kuhusu watu hao. Wako kinyume na Mungu. Wameigeuza neema ya Mungu kujihalalishia kutenda chochote wanachotaka. Wanakataa kumtii Mkuu aliye peke yake, Bwana wetu Yesu Kristo.

5Ninataka kuwasaidia mkumbuke baadhi ya vitu mnavyovifahamu tayari: Kumbukeni kwamba Bwana aliwaokoa watu wake kwa kuwatoa katika nchi ya Misri. Lakini baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini.[#1:5 Baadhi ya matoleo ya kale ya Kiyunani ya waraka huu wa Yuda yameandika “Yesu”. Baadhi ya matoleo ya hivi karibuni yana “Mungu”.]

6Na kumbukeni malaika waliopoteza mamlaka yao ya kutawala. Waliacha mahali pao pa kuishi. Hivyo Bwana amewaweka gizani, wamefungwa kwa minyororo ya milele, mpaka watakapohukumiwa siku iliyo kuu.

7Pia kumbukeni miji ya Sodoma na Gomora na miji mingine iliyoizunguka. Kama wale malaika, watu wa miji ile walikuwa na hatia ya dhambi ya uzinzi, hata wakataka kuzini na malaika. Na waliadhibiwa kwa moto wa milele. Miji hii ni mfano kwa waovu watakaoteseka kwa adhabu ya moto wa milele.

8Ni sawasawa na watu hawa waliojiingiza kwenye kundi lenu. Wanaongozwa na ndoto, wanajichafua wenyewe kwa dhambi. Wanapuuza mamlaka ya Bwana na kusema mambo mabaya kinyume na walio watukufu.[#1:8 Hapa inamaanisha viumbe wa mbinguni, malaika.]

9Hata malaika mkuu Mikaeli hakufanya hivi. Mikaeli alibishana na Ibilisi kuhusu nani angeuchukua mwili wa Musa. Lakini Mikaeli hakutamka hukumu kwa Ibilisi kwa mashitaka yake ya uongo. Badala yake, Mikaeli alisema, “Bwana mwenyewe akuadhibu!”

10Lakini watu hawa hukashifu mambo wasiyoyaelewa. Wanaelewa baadhi ya mambo, isipokuwa wanayaelewa mambo haya si kwa kufikiri bali kwa kuhisi, kama wanyama wasiofikiri. Na haya ni mambo yanayowaangamiza.

11Itakuwa vibaya kwao kwa kuwa wameifuata njia ambayo Kaini aliitumia. Kwa kutafuta fedha, wamejiingiza katika kosa lile lile la Balaamu. Wamepigana kinyume na Mungu kama alivyofanya Kora. Na wataangamizwa vile vile kama Kora.[#1:11 Tazama Mwa 4:1-16.; #1:11 Tazama Hes 25:1-4; 31:16.; #1:11 Tazama Hes 16:1-40.]

12Watu hawa ni kama madoa machafu miongoni mwenu, wanawatia aibu mnapokutanika pamoja kuonesha upendo miongoni mwenu na kula chakula kwa pamoja kama kanisa. Pasipo kuwa na aibu wanakula pamoja nanyi. Wanajijali wao wenyewe tu. Wao ni kama mawingu yasiyo na mvua yanayosukumwa na upepo kila upande. Wako kama miti isiyo na matunda wakati wa mavuno ambayo hung'olewa kutoka ardhini. Hivyo wamekufa mara mbili.

13Kama mapovu machafu juu ya mawimbi ya bahari, kila mtu anaweza kuona mambo ya aibu wanayoyafanya. Ni kama nyota zinazotangatanga angani. Nao wameandaliwa mahali penye giza kuu milele.

14Henoko, mtu wa kizazi cha saba kutoka Adamu, alisema hivi kuhusu watu hawa: “Tazama! Bwana anakuja pamoja na maelfu ya malaika watakatifu.

15Kumhukumu kila mmoja. Atawaadhibu wale wote walio kinyume naye kutokana na maovu waliyotenda kwa sababu ya kutokumheshimu. Ndiyo, Bwana atawaadhibu watenda dhambi wote hawa wasiomheshimu. Atawaadhibu kwa sababu ya mambo maovu waliyosema kinyume naye.”

16Watu hawa daima hulalamika na kutafuta ubaya kwa wengine. Daima hutenda mambo maovu wanayotaka kufanya. Hujisifu wenyewe. Huwatendea vyema baadhi ya watu kuliko wengine ili wapate vitu wanavyovitaka.

Tahadhari na Mambo ya Kufanya

17Rafiki wapendwa, kumbukeni mambo ambayo mitume wa Bwana Yesu Kristo walisema kuwa yatatokea.

18Walisema, “Katika nyakati za mwisho kutakuwa watu wanaomcheka Mungu na kufanya yale wanayotaka kufanya tu, mambo ambayo ni kinyume na Mungu.”

19Hawa ni watu wanaowagawa katika makundi. Si wa rohoni kwa sababu hawana Roho Mtakatifu.

20Lakini ninyi, rafiki wapendwa, itumieni imani yenu takatifu zaidi kusaidiana ninyi kwa ninyi ili muwe imara zaidi katika imani. Ombeni kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

21Jiwekeni salama katika upendo wa Mungu, kadri mnavyomsubiri Bwana Yesu Kristo kuionesha rehema yake kwenu kwa kuwapa uzima wa milele.

22Waonesheni rehema walio na mashaka.

23Waokoeni wale wanaoishi katika hatari ya moto wa jehanamu. Muwatendee wengine kwa rehema, lakini muwe waangalifu kuwa maisha yao maovu yasichafue mwenendo wenu mwema.[#1:23 Kwa maana ya kawaida, “kuchukia hata nguo ya ndani inayochafuliwa na mwili”.]

Msifuni Mungu

24Mungu ana nguvu na anaweza kuwafanya msianguke. Anaweza kuwaingiza katika uwepo wa utukufu wake bila makosa yoyote ndani yenu na akawapa furaha kuu.

25Ni Mungu peke yake, aliye Mwokozi wetu. Kwake uwepo utukufu, ukuu, nguvu na mamlaka kupitia Yesu Kristo kwa wakati uliopita, uliopo na milele. Amina.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International