Mika 1

Mika 1

1Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Mika, mwenyeji wa Moreshethi, wakati Yothamu, Ahazi na Hezekia walipokuwa wafalme wa Yuda. Mika aliona mambo yote haya kuhusu Samaria na Yerusalemu.

Mwenyezi-Mungu aja kuhukumu

2Sikilizeni enyi watu wote;

sikiliza ewe dunia na vyote vilivyomo.

Mwenyezi-Mungu anakuja kuwashtaki,

Bwana anena kutoka hekalu lake takatifu.

3Naam! Mwenyezi-Mungu yuaja kutoka makao yake;

atashuka na kutembea juu ya vilele vya dunia.

4Milima itayeyuka chini ya nyayo zake,

kama nta karibu na moto;

mabonde yatapasuka,

kama maji yaporomokayo kwenye mteremko.

5Haya yote yatatukia

kwa sababu ya makosa ya wazawa wa Yakobo,

kwa sababu ya dhambi za wazawa wa Israeli.

Je, uhalifu wa Yakobo waonekana wapi?

Katika mji wake mkuu Samaria!

Je, uhalifu wa Yuda waonekana wapi?

Katika Yerusalemu kwenyewe!

6Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Mji wa Samaria nitaufanya magofu nyikani,

shamba ambalo watu watapanda mizabibu.

Mawe yaliyoujenga nitayatupa bondeni,

na misingi yake nitaichimbuachimbua.

7Sanamu zake zote zitavunjwavunjwa,

kila kilichochumwa kitateketezwa kwa moto.

Vinyago vyake vyote nitaviharibu.

Vilirundikwa kutokana na ujira wa malaya,

navyo vitatumiwa tena kulipia umalaya.”

Nabii anaomboleza juu ya Yerusalemu na Yuda

8Kwa sababu hiyo, mimi nitalia na kuomboleza;

nitatembea uchi na bila viatu.

Nitaomboleza na kulia kama mbweha,

nitasikitika na kulia kama mbuni.

9Majeraha ya Samaria hayaponyeki,

nayo yameipata pia Yuda;

yamefikia lango la Yerusalemu,

mahali wanapokaa watu wangu.

10Msiitangaze habari hii huko Gathi,

wala msilie machozi!

Huko Beth-leafra mgaegae mavumbini kwa huzuni.

11Nendeni enyi wakazi wa Shafiri,

mkiwa uchi na wenye haya.

Wakazi wa Zaanani msitoke nje ya mji wenu.

Watu wa Beth-ezeli wanalia;

msaada wao kwenu umeondolewa.

12Wakazi wa Marothi wanangojea msaada kwa hamu kubwa,

lakini maangamizi yaja kutoka kwa Mwenyezi-Mungu

karibu kabisa na lango la Yerusalemu.

13Enyi wakazi wa Lakishi,

fungeni farasi wepesi na magari ya vita.

Nyinyi mlikuwa mmeiga dhambi ya watu wa Siyoni,

makosa ya Waisraeli yalikuwa kwenu.

14Hivyo, mnapaswa kuagana na kuwaacha wakazi wa Morasheth-gathi.

Nao mji wa Akzibu hautawasaidia wafalme wa Israeli,

15Enyi wakazi wa Maresha,

Mungu atawaleteeni tena adui atakayewateka.

Viongozi waheshimiwa wa Israeli

watakimbilia pangoni huko Adulamu.

16Enyi watu wa Yuda, nyoeni upara

kuwaombolezea watoto wenu wapenzi;

panueni upara wenu uwe mpana kama wa tai,

maana watoto wenu watawaacha kwenda uhamishoni.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania