Nehemia 9

Nehemia 9

Watu wanaungama dhambi zao

1Siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wa saba, watu wa Israeli walikusanyika, wakifunga na kuvaa mavazi ya magunia na kujipaka udongo kichwani kuonesha majuto yao.

2Wakati huo, walikuwa wamejitenga mbali na watu wa mataifa mengine, wakasimama na kuungama dhambi zao na maovu ya babu zao.

3Kwa muda wa kama masaa matatu, walisimama huku sheria ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, inasomwa. Na kwa masaa matatu yaliyofuata, walikuwa wakitubu na kumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.

4Kuliwekwa jukwaa la Walawi; hapo walisimama Yeshua, Bani, Kadmieli, Shebania, Buni, Sherebia, Bani na Kenani. Wakamwomba kwa sauti kubwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wao.

5Walawi, yaani: Yeshua, Kadmieli, Bani, Hashabuea, Sherebia, Hodia, Shebania na Pethahia wakawaambia watu;

“Simameni na kumsifu Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

Msifuni milele na milele!

Na watu walisifu jina lako tukufu,

ambalo hutukuka kuliko baraka na sifa zote.”

Sala ya toba

6Ezra akaomba kwa sala ifuatayo:

“Wewe peke yako ndiwe Mwenyezi-Mungu;

ndiwe uliyefanya mbingu na jeshi lake lote,

dunia na vyote vilivyomo,

bahari na vyote vilivyomo;

nawe ndiwe unayevihifadhi hai,

na jeshi lote la mbinguni lakuabudu wewe.

7Wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu,

Mungu uliyemchagua Abramu,

ukamtoa toka Uri ya Wakaldayo

na kumpa jina Abrahamu.

8Ukamwona kuwa yu mwadilifu mbele yako;

ukafanya agano naye kuwapa wazawa wake nchi ya Wakanaani,

Wahiti, Waamori, Waperizi, Wayebusi na Wagirgashi.

Na ahadi yako ukaitimiza;

kwani wewe u mwaminifu.

9“Uliyaona mateso ya babu zetu

walipokuwa nchini Misri,

na walipokuomba msaada kwenye Bahari ya Shamu

uliwasikia.

10Ulifanya ishara na maajabu dhidi ya Farao,

watumishi wake wote

na watu wote wa nchi yake;

kwani ulijua kuwa

waliwakandamiza babu zetu.

Ukajipatia umaarufu uliopo mpaka leo.

11Uliigawa bahari katikati mbele yao,

nao wakapita katikati ya bahari,

mahali pakavu.

Lakini ukawatupa Wamisri waliowafuatia

kama jiwe zito ndani ya maji mengi.

12Mchana uliwaongoza kwa mnara wa wingu,

na usiku uliwaongoza kwa mnara wa moto

ili kuwamulikia njia ya kuendea.

13Kule mlimani Sinai

ulishuka toka mbinguni na kuzungumza nao.

Ukawapa maagizo safi, sheria za kweli,

kanuni nzuri na amri.

14Kwa njia ya Mose, mtumishi wako,

ukawajulisha Sabato yako takatifu

na ukawaagiza kuzifuata amri,

kanuni na sheria ulizowaamrisha.

15Walipokuwa na njaa,

ukawapa chakula kutoka mbinguni.

Walipokuwa na kiu

ukawapa maji kutoka kwenye mwamba.

Ukawaagiza kuichukua nchi uliyokuwa umewaahidi.

16Lakini wao na babu zetu wakawa na kiburi

na wakawa na shingo ngumu

wakakataa kufuata maagizo yako.

17Wakakataa kutii;

wasiyakumbuke maajabu uliyofanya miongoni mwao.

Wakawa na shingo zao ngumu,

wakajichagulia kiongozi wa kuwarudisha

utumwani nchini Misri.

Bali wewe Mungu u mwepesi kusamehe,

mwenye neema na huruma,

wewe hukasiriki upesi.

U mwenye fadhili nyingi, na hukuwatupa.

18Hata walipojitengenezea sanamu ya ndama na kusema,

‘Huyu ndiye mungu wetu

aliyetutoa kutoka nchi ya Misri,’

wakawa wamefanya kufuru kubwa.

19Wewe kwa huruma zako nyingi

hukuwatupa kule jangwani.

Mnara wa wingu

uliowaongoza mchana haukuondoka,

wala mnara wa moto

uliowamulikia njia usiku, haukuondoka.

20Ukawapa roho yako njema kuwashauri;

ukawapa mana kuwa chakula chao na maji ya kunywa

ili kutuliza kiu chao.

21Ukawatunza jangwani kwa miaka arubaini

na hawakukosa chochote;

mavazi yao hayakuchakaa

wala nyayo zao hazikuvimba.

22“Ukawaruhusu kushinda falme na mataifa,

ukawafanyia mengi kila upande.

Wakaishinda nchi ya Heshboni

alikotawala mfalme Sihoni;

na tena wakaishinda nchi ya Bashani

alikotawala mfalme Ogu.

23Wazawa wao ukawafanya wawe wengi

kama nyota za mbinguni;

ukawaleta katika nchi

uliyowaahidi babu zao.

24Hivyo, hao wazawa wakaja na kuimiliki nchi;

uliwashinda wakazi wa nchi hiyo,

Wakanaani, ukawatia mikononi mwao,

pamoja na wafalme wao,

watu wao na nchi yao ili wawatende wapendavyo.

25Miji yenye ngome wakaiteka,

wakachukua nchi yenye utajiri,

majumba yenye vitu vingi vizuri,

visima vilivyochimbwa,

mashamba ya mizabibu na mizeituni

pamoja na miti yenye matunda kwa wingi.

Hivyo wakala,

wakashiba na kunenepa

na kuufurahia wema wako.

26Lakini hawakuwa waaminifu kwako.

Wakakuasi,

wakaiacha sheria yako

na kuwaua manabii waliowaonya

ili wakurudie wewe.

Wakakufuru sana.

27Hivyo, ukawatia katika mikono ya adui zao,

nao wakawatesa.

Lakini wakiwa katika mateso yao,

wakakulilia, nawe ukawasikia kutoka mbinguni.

Na kwa huruma zako nyingi,

ukawapelekea viongozi wa kuwaokoa;

nao wakawakomboa toka mikononi mwao.

28Lakini amani ilipopatikana

wakatenda dhambi tena mbele yako,

nawe ukawaacha watiwe katika

mikono ya adui zao wawatawale.

Hata hivyo, walipotubu na kukulilia

ukawasikiliza kutoka mbinguni.

Na kwa kulingana na huruma zako nyingi,

ukawaokoa mara nyingi.

29Ukawaonya ili wairudie sheria yako.

Hata hivyo, kwa kiburi chao,

wakaacha kuzitii amri zako.

Wakayaasi maagizo yako,

ambayo kwayo mtu akiyatii, ataishi.

Wakawa wajeuri

pia wakafanya shingo zao ngumu,

na wakakataa kuwa watiifu.

30Ukawavumilia kwa miaka mingi,

na kuwaonya kwa njia ya roho yako

kwa kupitia manabii wako;

hata hivyo hawakusikiliza.

Basi ukawaacha

ukawatia mikononi mwa mataifa mengine.

31Hata hivyo,

kutokana na huruma zako nyingi,

hukuwaacha waangamie kabisa au kuwatupa,

kwani wewe u Mungu mwenye neema

na huruma.

32Kwa hiyo, ee Mungu wetu,

Mungu Mkuu,

mwenye nguvu na wa kutisha,

wewe unalishika agano lako

na una fadhili nyingi.

Mateso yaliyotupata, sisi,

wafalme wetu, wakuu wetu,

makuhani wetu, manabii wetu,

babu zetu na watu wako wote

tangu wakati wa wafalme wa Ashuru mpaka leo,

usiyaone kuwa ni madogo.

33Hata hivyo,

unayo haki kwa kutuadhibu hivyo;

kwani wewe umekuwa mwaminifu

ambapo sisi tumekuwa watenda maovu.

34Wafalme wetu, wakuu wetu,

makuhani wetu na babu zetu

hawajaishika sheria yako

wala kujali amri yako

na maonyo yako uliyowapa.

35Hawakukutumikia katika ufalme wao,

wala walipoyafurahia mema yako mengi uliyowajalia kwa wingi,

katika nchi kubwa na yenye rutuba uliyowapa

hawakuyaacha matendo yao maovu.

36Na leo tumekuwa watumwa;

tu watumwa katika nchi uliyowapa babu zetu

wafurahie matunda na vipawa vyake vyema.

37Kwa sababu ya dhambi zetu,

utajiri wa nchi hii

unawaendea wafalme uliowaleta kututawala.

Wanatutawala wapendavyo

hata na mifugo yetu

wanaitendea wapendavyo,

tumo katika dhiki kuu.”

Watu wanatia sahihi mapatano

38Kutokana na haya yote yaliyotokea, sisi tunaweka agano imara na wakuu wetu kwa maandishi; Walawi na makuhani wanatia sahihi zao na mhuri wao.[#9:38]

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania