Zaburi 29

Zaburi 29

Sauti ya Mungu katika dhoruba

1Mpeni Mwenyezi-Mungu heshima enyi viumbe vya mbinguni,[#Taz Zab 96:7-9]

semeni Mwenyezi-Mungu ni mtukufu na mwenye nguvu.

2Semeni jina la Mwenyezi-Mungu ni tukufu.

Mwabuduni katika mahali pake patakatifu.

3Sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya maji;

Mungu mtukufu angurumisha radi,

sauti ya Mwenyezi-Mungu yasikika juu ya bahari!

4Sauti ya Mwenyezi-Mungu ina nguvu,

sauti ya Mwenyezi-Mungu imejaa fahari.

5Sauti ya Mwenyezi-Mungu huvunja mierezi;

Mwenyezi-Mungu avunja mierezi ya Lebanoni.

6Huirusha milima ya Lebanoni kama ndama,

milima ya Sirioni kama mwananyati.

7Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutoa miali ya moto.

8Sauti ya Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa,

Mwenyezi-Mungu hutetemesha jangwa la Kadeshi.

9Sauti ya Mwenyezi-Mungu huitikisa mivule,[#29:9 Kiebrania: Humfanya paa azae.]

hukwanyua majani ya miti msituni,

na hekaluni mwake wote wasema:

“Utukufu kwa Mungu!”

10Mwenyezi-Mungu ameketi juu ya gharika;

Mwenyezi-Mungu ni mfalme atawalaye milele.

11Mwenyezi-Mungu na awape watu wake nguvu!

Mwenyezi-Mungu na awabariki watu wake kwa amani!

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania