Wakolosai 2

Wakolosai 2

1Napenda mjue jinsi ninavyofanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, kwa ajili ya watu wa Laodikea na kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona kwa macho.[#2:1 Huo ulikuwa mji, yapata kilomita 17 kutoka Kolosai (rejea Kol 4:13,15-16; Ufu 3:14-22). Hatuna habari yoyote inayoonesha kama Paulo alifika huko au la.]

2Nafanya hivi kusudi mioyo yao ifarijiwe na kuvutwa pamoja katika upendo, ili wajazwe uthabiti mwingi uletwao na elimu ya kweli. Hapo wataijua siri ya Mungu ambayo ni Kristo mwenyewe.[#2:2 Efe 1:9, maelezo.]

3Ndani yake zimefichika hazina zote za hekima na elimu.[#2:3 1Kor 1:24,30; Efe 3:19; rejea Meth 2:4-6; Isa 45:3.Wakolosai walikuwa katika hatari ya kupendelea ujuzi au elimu ya kibinadamu badala ya ujuzi ambao unaletwa na Kristo mwenyewe (taz Kol 2:8 maelezo).]

4Basi, nawaambieni, msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa maneno ya uongo hata kama ni ya kuvutia sana.

5Maana, ingawa mimi niko mbali nanyi kwa mwili, lakini niko pamoja nanyi kwa roho, na ninafurahi kuona uthabiti kamili mnaosimama nao pamoja katika imani yenu kwa Kristo.[#2:5 Rejea 1Kor 5:3.]

Maisha kamili katika Kristo

6Maadamu nyinyi mmemkubali Kristo Yesu aliye Bwana, basi, ishini katika muungano naye.

7Muwe na mizizi ndani yake, mjijenge juu yake na kuwa imara katika imani kama mlivyofundishwa. Muwe na shukrani tele.[#2:7 Rejea Efe 2:20-22.]

8Angalieni, basi, mtu asiwapotoshe kwa udanganyifu mtupu wa hekima ya kibinadamu, ambayo chanzo chake ni mafundisho ya mapokeo ya watu na ya pepo watawala, na wala si Kristo mwenyewe![#2:8 Wakolosai walijaribu kuchanganya imani yao kwa Yesu Kristo na baadhi ya imani nyingine.]

9Maana, ndani yake Kristo katika ubinadamu wake, umo ukamilifu wote wa Mungu,[#2:9 Rejea Yoh 1:14. Kwa kuanzia na aya hii mpaka aya ya 15 Paulo anawaonesha waumini kwamba wanapaswa kuwa waangalifu wasije wakakumbwa na mafundisho ya uongo.]

10nanyi mmepewa uhai kamili katika kuungana naye. Yeye yuko juu ya pepo watawala wote na wakuu wote.

11Katika kuungana na Kristo nyinyi mlitahiriwa, lakini si kwa tohara ifanywayo na watu, bali inayofanywa na Kristo mwenyewe, na ambayo inahusikana na kukombolewa kutoka katika utu wa dhambi.

12Maana, mlipobatizwa mlizikwa pamoja na Kristo, na katika ubatizo mlifufuliwa pia pamoja naye kwa kuamini katika nguvu ya Mungu ambaye alimfufua Kristo kutoka kwa wafu.[#2:12 Aya hii sasa inaeleza wazi zaidi ni nini kutahiriwa kwa kuungana na Kristo, msemo ambao umetajwa kimfano katika aya iliyotangulia. Yaani, yahusu mageuzi mapya kabisa ya kiroho; rejea Yer 4:4; Rom 2:28-29.]

13Wakati mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu nyinyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa nyinyi uhai pamoja na Kristo. Mungu ametusamehe dhambi zetu zote;

14alifutilia mbali ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta kabisa kwa kuipigilia msalabani.[#2:14 Mwandishi anatumia hapa lugha ya picha ya deni lililoandikwa katika hati.; #2:14 Namna hii ya kusema si wazi. Hata hivyo, yahusu kifo cha Yesu msalabani, kifo ambacho kiliondoa au kufutilia mbali yale madeni yetu (Mat 6:12) yaani dhambi zetu (Efe 2:15-16; 1Pet 2:24; rejea 2Kor 5:21; Gal 3:13).]

15Huko Kristo aliwapokonya nguvu zao hao pepo watawala na wakuu; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwaburuta kama mateka katika msafara wa ushindi wake.[#2:15 Taz Kol 1:16, maelezo.; #2:15 Taz 2Kor 2:14-17, maelezo.]

16Kwa hiyo, basi, msikubali kupewa masharti na mtu yeyote kuhusu vyakula au vinywaji, siku za sherehe, sikukuu ya mwezi mpya au Sabato.[#2:16 Miongoni mwa mafundisho yaliyoenea kule Kolosai lilikuwa fundisho la kukataza kula vyakula fulani fulani na kuzithamini siku fulani za kalenda kuwa za maana zaidi kuliko nyingine. Taz Gal 4:3 maelezo; rejea Rom 14:1-6.]

17Mambo ya aina hiyo ni kivuli tu cha yale yatakayokuja; ukweli wenyewe ndiye Kristo.

18Msikubali kuhukumiwa na mtu yeyote anayejitakia kuwa wa maana kwa sababu ya maono ya pekee na ambaye anasisitiza juu ya unyenyekevu wa uongo na ibada kwa malaika. Mtu wa namna hiyo amepumbazika kwa fikira danganyifu za kidunia[#2:18 Hiyo nayo ni sehemu ya mkosi uliotajwa katika 2:8.]

19na amejitenga na Kristo aliye kichwa cha huo mwili. Chini ya uongozi wa Kristo, mwili wote unalishwa na kuunganishwa pamoja kwa viungo na mishipa yake, nao hukua kama atakavyo Mungu.[#2:19 Taz Efe 4:16 maelezo. Katika Efe picha au mfano wa “mwili” ambao ni kanisa, unatumiwa kusisitiza uhusiano kati ya viungo hivyo; hapa uhusiano kati ya hivyo viungo na Kristo ndio unaotiliwa mkazo.]

Kufa na kuishi pamoja na Kristo

20Nyinyi mmekufa pamoja na Kristo na kukombolewa katika nguvu za pepo watawala wa ulimwengu. Kwa nini, basi, kuishi tena kama vile mngekuwa wa ulimwengu huu? Ya nini kuwekewa masharti:[#2:20 Rejea aya ya 12 na Rom 6:6-11; Gal 4:3-5,9.]

21“Msishike hiki,” “Msionje kile,” “Msiguse kile!”

22Mambo hayo yote yanahusika na vitu vyenye kuharibika mara tu vinapotumiwa; hayo ni maagizo na mafundisho ya kibinadamu tu.[#2:22 Rejea Isa 29:13; Mat 15:9; Marko 7:8.]

23Kweli, masharti hayo yaonekana kuwa ya hekima kwa namna ya ibada wanayojishurutishia, unyenyekevu, na kuutendea mwili kwa ukali; lakini hayafai chochote kuzuia tamaa za mwili.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania