The chat will start when you send the first message.
1Kitabu hiki kina maneno ambayo Mose aliwaambia watu wote wa Israeli wakati walipokuwa nyikani mashariki ya mto Yordani. Walikuwa katika bonde la Yordani karibu na Sufu, kati ya mji wa Parani upande mmoja na mji wa Tofeli, Labani, Hazerothi na Dizahabu, upande mwingine.[#1:1 Miji inayotajwa hapa haijulikani kwa yakini ulikuwa wapi.]
2(Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka mlima Horebu hadi Kadesh-barnea kwa njia ya mlima Seiri.)[#1:2 Jina lingine la mlima Sinai. Kitabu hiki kinatumia jina Horebu kuutaja mlima huo isipokuwa tu katika Kumb 33:2.]
3Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na moja, mwaka wa arubaini, baada ya kutoka Misri, Mose aliwaambia watu kila kitu ambacho Mwenyezi-Mungu alimwamuru awaambie.[#1:3 Huo ni mwezi uitwao katika Kiebrania “Shebati” kuanzia katikati ya mwezi Januari mpaka katikati ya mwezi Februari katika kalenda yetu.; #1:3 Idadi ya “arubaini” ni mojawapo ya idadi au hesabu zinazotumiwa mara kwa mara katika Biblia kwa maana za pekee. Hapa msemo “miaka arubaini” unaashiria muda mrefu. Taz kwa mfano: mvua ya gharika kuu ilinyesha kwa siku arubaini (Mwa 7:4,17,18); Mose alikaa mlimani Sinai siku arubaini (kut 24:17,18); Waisraeli walitangatanga jangwani kwa miaka arubaini (Hes 14:33-34; Kumb 2:7; 29:4-6); Yesu alifunga kwa siku arubaini (Mat 4:2; Marko 1:12-13; Luka 4:2).; #1:3 Habari juu ya Waisraeli kuondoka Misri na kusafiri jangwani chini ya uongozi wa Mose, inaelezwa kinaganaga katika Kut 13—40 na Hes 1—36.]
4Alifanya hivyo baada ya kumshinda mfalme Sihoni wa Waamori ambaye alikuwa anakaa mjini Heshboni, na mfalme Ogu wa Bashani ambaye alikuwa anakaa mjini Ashtarothi na Edrei.[#1:4 Kuangamizwa kwa wafalme hao kunatajwa katika Hes 21:21-35.]
5Mose alichukua jukumu la kuwaelezea watu sheria ya Mungu wakati walipokuwa ng'ambo ya pili ya mto Yordani.
Aliwaambia hivi:
6“Tulipokuwa mlimani Sinai, Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu alituambia hivi: ‘Mmekaa muda wa kutosha kwenye mlima huu;[#1:6 Fungu hili la maneno hutumiwa zaidi ya mara mia tatu katika kitabu hiki. Kuhusu “Mwenyezi-Mungu” taz Kut 3:15 maelezo. Kwa kutamka kwamba Mwenyezi-Mungu, ni “Mungu wetu” kuna kukubali kwamba nafasi ya miungu mingine katika imani na utamaduni wa kidini wa Waisraeli haipo na haitakiwi.; #1:6 Hapa linaanza simulizi la kwanza la Mose katika kitabu hiki. Simulizi hili lina sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni muhtasari wa matukio yaliyowasibu Waisraeli tangu walipoondoka eneo la mlima Horebu, yaani mlima Sinai, mpaka walipofika eneo la Moabu (1:6—3:29); na katika sehemu ya pili Mose anawatia moyo na kuwahimiza Waisraeli wasikilize sauti ya Mwenyezi-Mungu na kuzingatia amri zake (4:1-40).]
7sasa vunjeni kambi yenu mwendelee na safari. Nendeni kwenye nchi ya milima ya Waamori na maeneo ya nchi jirani katika Araba, kwenye milima na mabonde, huko Negebu na sehemu za pwani; naam, nendeni mpaka nchi ya Kanaani, na nchi ya Lebanoni, hadi kwenye ule mto mkubwa wa Eufrate.
8Nchi hii yote nimeiweka mbele yenu. Basi, nendeni mkaimiliki nchi hiyo ambayo mimi Mwenyezi-Mungu niliapa kuwapa wazee wenu Abrahamu, Isaka, Yakobo na wazawa wao.’”[#1:7-8 Aya hizi, kwa mara ya kwanza, zinaeleza juu ya nchi ya Kanaani na mipaka yake. Mataifa mengi tangu kale na kale yalikuwa na masimulizi yao kuhusu malimbuko yao na nchi walizozijua kama zao. Hapa mwandishi anatamka kwamba Waisraeli waliahidiwa nchi hiyo na Mungu wao (Mwa 15:18-21).]
9Mose akawaambia watu, “Tulipokuwa bado mlimani Sinai, mimi niliwaambieni hivi: ‘Jukumu la kuwaongozeni ni kubwa mno kwangu mimi peke yangu.
10Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, amewafanya muwe wengi; leo mmekuwa wengi kama nyota za mbinguni.
11Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu, na awafanye mzidi kuongezeka mara elfu zaidi ya mlivyo sasa na kuwabariki kama alivyoahidi!
12Lakini mimi peke yangu nitawezaje kuchukua jukumu hilo zito la kusuluhisha ugomvi wenu?
13Chagueni kutoka katika kila kabila watu wenye hekima, busara na ujuzi ili niwateue wawe viongozi wenu.’
14Nyinyi mlikubali, mkanijibu hivi: ‘Jambo ulilosema ni la busara’.
15Hivyo niliwachukua wale viongozi wenye hekima, busara na ujuzi ambao mliwachagua kutoka katika makabila yenu, nikawaweka kuwa viongozi wenu. Niliwaweka wengine kuwa makamanda wa makundi ya watu elfuelfu, ya watu miamia, ya watu hamsinihamsini na ya watu kumikumi. Nilichagua pia maofisa wengine wa kuchunga kila kabila.[#1:9-15 Taz Kut 15:13-25. Hawa viongozi walikuwa watu wa umri mzima au wazee ambao walikuwa na jukumu la kuongoza koo katika kila kabila.]
16“Wakati huohuo niliwapa waamuzi wenu maagizo yafuatayo: ‘Sikilizeni kesi za watu wenu. Toeni hukumu za haki katika visa vya watu wenu, kadhalika na mizozo ya wageni waishio pamoja nanyi.
17Msimpendelee mtu yeyote katika kutoa hukumu; mtawasikiliza bila upendeleo, wakubwa kwa wadogo. Msitishwe na mtu yeyote, maana hukumu mnayotoa inatoka kwa Mungu. Kesi yoyote ikiwa ngumu zaidi kwenu, ileteni kwangu, nami nitaisikiliza.’[#1:17 Taz 2Nya 19:6-7; Meth 16:33.]
18Wakati huohuo, niliwaagizeni mambo yote mnayopaswa kufanya.
19“Basi, kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru, tulianza safari yetu kutoka mlima Horebu, tukapita katika lile jangwa kubwa la kutisha mnalolijua, kwa kufuata njia inayoelekea nchi ya milima ya Waamori. Tulipofika Kadesh-barnea,
20mimi niliwaambieni: ‘Sasa mmefika katika nchi ya milima ya Waamori ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ametupatia.
21Tazameni, Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ameiweka nchi hii mbele yenu. Haya! Ingieni, mkaimiliki kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wa wazee wenu alivyowaambia. Msiogope wala msifadhaike!’
22“Kisha nyote mlikuja karibu nami mkaniambia, ‘Tutume watu watutangulie, waipeleleze nchi, halafu warudi kutujulisha njia bora ya kufuata na miji ipi tutaikuta huko.’
23Jambo hilo lilionekana kuwa jema kwangu, nikawateua watu kumi na wawili, mtu mmoja kutoka katika kila kabila.
24Watu hao walikwenda katika nchi ile ya milima, wakafika kwenye bonde la Eshkoli na kulipeleleza.
25Waliporudi, walituletea baadhi ya matunda ya nchi hiyo na wakatuarifu kwamba nchi hiyo anayotupatia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, ni nzuri.
26“Lakini nyinyi hamkufuata agizo la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa kukataa kwenda katika nchi hiyo.
27Mlinung'unika ndani ya mahema yenu mkisema, ‘Mwenyezi-Mungu anatuchukia na ndiyo maana alitutoa nchini Misri. Alitaka kututia mikononi mwa Waamori, atuangamize.
28Kwa nini tuende huko hali tumevunjika moyo kwa hofu? Wametuambia kuwa watu wa huko ni wakubwa na warefu kuliko sisi, na kwamba miji yao ni mikubwa na yenye kuta zifikazo mawinguni. Tena wamesema kwamba waliwaona wale wazawa wa Anaki!’[#1:28 Tafsiri nyingine yamkini: “yenye kuta ndefu mno”.; #1:28 Yamkini yahusu watu warefu ambao waliishi ndani au karibu na nchi ya Kanaani kabla ya Waisraeli. Taz Hes 13:33; Kumb 2:20-21.]
29“Lakini mimi niliwaambieni hivi: ‘Msiwe na hofu wala msiwaogope watu hao.’
30Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambaye huwatangulia, yeye mwenyewe atapigana kwa ajili yenu kama alivyofanya mbele yenu kule Misri na
31kule jangwani ambako mliona jinsi alivyowabeba safari hiyo yote kama vile baba amchukuavyo mwanawe mpaka mkafika hapa.
32Lakini japo nilisema hayo yote, nyinyi hamkumwamini Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu,
33ambaye aliwatangulia njiani na kuwatafutia mahali pa kupiga kambi zenu. Usiku aliwatangulieni kwa moto na mchana kwa wingu, ili kuwaonesha njia.[#1:33 Katika Biblia mara kwa mara wingu na moto vinatumiwa kuashiria kuweko kwake Mwenyezi-Mungu (Mwa 15:17-18; Kut 3:1-6; 19:16-19; 24:15-18; Amu 13:20) Taz pia 13:21-22; Hes 9:15-23.]
34“Mwenyezi-Mungu aliyasikia manung'uniko yenu, akakasirika, akaapa akisema:
35‘Hakuna hata mmoja wenu katika kizazi hiki kiovu atakayeingia katika nchi ile nzuri niliyoahidi kuwapa wazee wenu.
36Kalebu mwana wa Yefune, ndiye tu atakayeiona; nami nitampatia nchi hiyo aliyoikanyaga iwe yake yeye na wazawa wake kwa kuwa amekuwa mwaminifu kabisa kwangu.’
37Mwenyezi-Mungu alinikasirikia mimi pia kwa sababu yenu, akasema, ‘Hata wewe Mose hutaingia katika nchi hiyo.
38Lakini msaidizi wako Yoshua mwana wa Nuni, ataingia humo. Basi, mtie moyo kwani yeye atawaongoza watu wa Israeli waimiliki nchi hiyo’.[#1:36-38 Kati ya wale wapelelezi ambao Mose aliwatuma, Kalebu na Yoshua ndio peke yao waliowahimiza watu na kuwatia moyo wamtegemee Mungu na kuingia nchini Kanaani (Hes 13:25-33; 14:1-10). Kwamba Mungu alimkasirikia Mose pia taz Kumb 4:21.]
39Kisha Mwenyezi-Mungu akatuambia sisi sote, ‘Hao watoto wenu mnaoogopa kwamba watakuwa nyara za adui zenu, naam hao walio wadogo ambao hawajui bado kupambanua kati ya mema na mabaya, hao ndio watakaoingia huko, nami nitawapa wao nchi hiyo iwe yao.
40Lakini nyinyi, geukeni na kurudi jangwani kuelekea Bahari ya Shamu.’[#1:40 Kiebrania ni “yam suf”, maana yake “Bahari ya Mafunjo”. (Taz Kut 14:1-31, 15:1-21).]
41“Kisha mkanijibu, ‘Sisi tumemtendea dhambi Mwenyezi-Mungu, lakini sasa tutakwenda na kupigana kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, alivyotuamuru’. Hivyo, kila mmoja wenu akajitayarisha kupigana vita; maana mlifikiri kwamba lingekuwa jambo rahisi kuivamia nchi hiyo ya milima.
42Naye Mwenyezi-Mungu akaniambia, ‘Waambie hao watu wasiende kupigana kwa sababu sipo pamoja nao; wasiende, wasije wakashindwa na adui zao’.
43Basi, mimi niliwaambieni hivyo, lakini nyinyi hamkusikia. Badala yake mlikataa kufuata agizo la Mwenyezi-Mungu, bila kujali mkaingia katika nchi hiyo ya milima.
44Hapo, Waamori waliokuwa wanaishi katika eneo hilo la milimani wakateremka kuwashambulia na kama wafanyavyo nyuki wakawapiga huko Seiri mpaka Horma.
45Ndipo mliporudi, mkamlilia Mwenyezi-Mungu, lakini Mwenyezi-Mungu hakuwasikiliza wala hakuwajali.
46Basi, mkabaki huko Kadeshi kwa muda mrefu ambao mlikaa huko.