The chat will start when you send the first message.
1Hapo, Mose pamoja na Waisraeli wakamwimbia Mwenyezi-Mungu wimbo huu,
“Nitamwimbia Mwenyezi-Mungu kwani ameshinda kwa fahari,
farasi na mpandafarasi wake amewatosa baharini.
2Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu na uwezo,[#15:2 Kiebrania ni “Yah”, kifupisho cha jina “Yahweh”. Taz Kut 3:15 maelezo.]
yeye mwenyewe ndiye anayeniokoa.
Yeye ni Mungu wangu nami nitamsifu,
ni Mungu wa baba yangu nami nitamtukuza.
3Mwenyezi-Mungu ni shujaa vitani;
Mwenyezi-Mungu ndilo jina lake.
4“Magari na majeshi ya Farao ameyatumbukiza baharini,
maofisa wake wateule wamezama katika bahari ya Shamu.
5Vilindi vya maji vimewafunika,
wameporomoka baharini kama jiwe.
6“Mkono wako wa kulia ee Mwenyezi-Mungu watukuka kwa nguvu;
kwa mkono wako wa kulia ee Mwenyezi-Mungu wawaponda adui.
7Kwa wingi wa ukuu wako wawaangamiza wapinzani wako;
wawapulizia ghadhabu yako nayo yawateketeza kama makapi.
8Kwa pumzi ya pua yako maji yalirundikana,[#15:8 Lugha ya kishairi ya kusema upepo mkali wa mashariki (taz pia 14:21).]
mawimbi yakasimama wima kama ukuta;
vilindi katikati ya bahari vikagandamana.
9Adui alijisemea, ‘Nitawafuata na kuwakamata;
nitagawanya nyara mpaka hamu yangu iishe.
Tutaufuta upanga wetu,
tutawaangamiza kwa mkono wetu.’
10Lakini wewe uliuvumisha upepo wako,
nayo bahari ikawafunika.
Walizama majini kama risasi.
11“Ewe Mwenyezi-Mungu,
ni nani kati ya miungu anayelingana nawe?
Ni nani aliye kama wewe uliye mtakatifu mkuu,
utishaye kwa matendo matukufu,
unayetenda mambo ya ajabu?
12Uliunyosha mkono wako wa kulia,
nayo nchi ikawameza maadui zetu.
13“Kwa fadhili zako kuu umewaongoza watu uliowakomboa,[#15:13-17 Kuhusu uongozi wa Mwenyezi-Mungu kama mchungaji taz Zab 23. Picha tunayopewa katika aya hizi hasa aya 17 ni ya hali ya baadaye, baada ya kutoka Misri na kuhamia nchini Kanaani.]
kwa nguvu yako umewaongoza kwenye makao yako matakatifu.
14Watu wa mataifa wamesikia hayo wakatetemeka;
wakazi wa Filistia wamekumbwa na kitisho.
15Wakuu wa Edomu wamefadhaishwa;
viongozi wa Moabu wamekumbwa na woga mkuu;
wakazi wote wa Kanaani wamevunjika moyo.
16Kitisho na hofu vimewavamia.
Kwa sababu ya ukuu wa nguvu zako,
wao wamenyamaza kimya kama jiwe,
mpaka watu wako ee Mwenyezi-Mungu, wapite,
naam, mpaka watu hao uliowakomboa wamewapita.
17Wewe utawaleta watu wako na kuwapanda mlimani pako;[#15:17 Mlima hapa yawezekana kuwa ni neno la kutaja Mlima Siyoni kule Yerusalemu. Mfalme Solomoni alimjengea Mwenyezi-Mungu hekalu huko yapata mwaka 350 baada ya Waisraeli kutoka Misri.]
pale ulipochagua ee Mwenyezi-Mungu pawe makao yako,
mahali patakatifu ee Mwenyezi-Mungu ulipojenga kwa mikono yako.
18Wewe, ee Mwenyezi-Mungu,
watawala milele na milele.”
19Wakati farasi wa Farao na magari yake pamoja na wapandafarasi wake walipoingia mahali pakavu baharini, Mwenyezi-Mungu aliyarudisha maji ya bahari yakawafunika. Lakini Waisraeli waliendelea kutembea pakavu katikati ya bahari.
20Basi nabii Miriamu, dada yake Aroni, akachukua kingoma mkononi, na wanawake wengine wote wakamfuata wakiwa na vingoma vyao wakicheza.[#15:20 Miriamu ambaye anatajwa pia kama nabii, yamkini alikuwa dada mkubwa wa Mose na ambaye alisaidia kumwokoa mtoto Mose na kumpatia mama Mwebrania (mama yao mwenyewe) wa kumnyonyesha na kumlea kwa niaba ya binti Farao ambaye alimgundua mtoni Nili (Kut 2:1-10). Kuhusu watu wanaoitwa manabii taz orodha ya manabii katika Utangulizi kwa Vitabu vya manabii.]
21Miriamu akawaongoza kwa kuimba,
“Mwimbieni Mwenyezi-Mungu kwani ameshinda kwa fahari,
farasi na mpandafarasi wake amewatosa baharini.”
22Kisha, Mose aliwaongoza Waisraeli kutoka bahari ya Shamu, wakaenda mpaka jangwa la Shuri. Walisafiri kwa muda wa siku tatu jangwani bila kuona maji yoyote.[#15:22 Jangwa hilo lilikuwa mashariki ya Gosheni, kwenye sehemu ya kaskazini ya Peninsula ya Sinai (taz ramani).]
23Walipofika mahali panapoitwa Mara, hawakuweza kuyanywa maji ya Mara kwa sababu yalikuwa machungu. Kwa sababu hiyo mahali hapo pakaitwa Mara.[#15:23 Kiebrania maana yake ni “chungu” (taz pia Rut 1:20).]
24Basi, watu wote wakamlalamikia Mose wakisema, “Sasa tutakunywa nini?”[#15:24 Kuhusu malalamiko ya Waisraeli taz 14:11-12 maelezo.]
25Hapo Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamwonesha kipande cha mti, na Mose akakitumbukiza katika maji; maji hayo yakawa mazuri.
Huko Mungu aliwapa Waisraeli amri na agizo, ili ajue uthabiti wao,
26akawaambia, “Ikiwa mtaisikiliza kwa makini sauti yangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kutenda yaliyo sawa mbele yangu, na kuheshimu amri na maagizo yangu yote, basi, mimi sitawaletea yale magonjwa niliyowaletea Wamisri. Kwa sababu, mimi ndimi Mwenyezi-Mungu ninayewaponya nyinyi.”[#15:26 Tamko muhimu katika Biblia juu ya Mungu na ambalo hutumika mara kwa mara (Kumb 7:15; 32:39; Yer 17:14; 30:17; Zab 41:3-4). Yahusu sio tu kuponya magonjwa ya mwili, bali pia msamaha wa dhambi na kuokolewa kwa jumla (taz Yak 5:15).]
27Kisha Waisraeli wakawasili huko Elimu ambako kulikuwa na chemchemi kumi na mbili na mitende sabini. Wakapiga kambi yao huko karibu na maji.[#15:27 Mahali penyewe siku hizi hapajulikani. Lakini yamkini ni Wadi Gharandel (taz pia 16:1; Hes 33:9-10), yapata kilomita mia moja na thelathini kusini-mashariki ya Mfereji wa Suezi. Katika Hes 33:9 inasemwa kuwa huko kulikuwa na chemchemi kumi na mbili na mitende kwa wingi.]